Habari za Punde

Mkutano wa Kikao cha Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ Inayoshughukia Masuala ya Muungano

Katibu Mkuu Kiongozi wa SMT Balozi John Kijazi Kushoto na Katibu Kiongozi mwenzake wa Zanzibar Dr. Abdulhamid Yahya Mzee wakitia saini hati ya Utaratibu wa Vikao Kamati yay a Pamoja na SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano.
Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Balozi Amina Salum Ali Kulia na Waziri Mwenzake wa Biashara wa SMT Mh. Inocent Mashugwa wakitia saini Hati ya Gharama za kushusha Mizigo ya Zanzibar kwenye Bandari ya Dar es salaam,
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Balozi Palamagamba Kabud Kushoto na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu Mh. Issa Haji Ussi Gavu wakitia saini Hati ya Ushiriki wa Zanzibar Kikanda na Kimataifa.
Waziri wa Ardhi, Makaazi Maji na Nishati Zanzibar Mh. Salama Aboud Kulia akipeana mkono na Waziri wa Nishati wa SMT Mh. Medak Kalemani mara baada ya kusaini Hati ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia.

Baadhi ya Viongozi wa Kitaifa walioshiriki Kikao cha kusaini Hati ya Makubaliano za kuondoa Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi hapo Ikulu Jijini Dar es salaam.

Wa kwanza kutoka Kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano Mh. Mussa Azzam Zungu, Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mohamed Aboud, Mgombea Urais wa Zanzibar kupitia CCM Dr. Hussein Ali Mwinyi, Katibu Mkuu Kiongozi SMT Balozi John Kijazi na Katibu Mkuu Kiongozi SMZ Nd. Abdulhamid Yahya Mzee.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa Taarifa kwenye Kikao hicho cha kusaini Hati Tano za Makubaliano za kuondoa Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi.
Waziri Mkuu wa Serikali Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Kassim Majaliwa  akitoa Taarifa kwenye Kikao hicho cha kusaini Hati Tano za Makubaliano za kuondoa Hoja za Muungano zilizopatiwa ufumbuzi.

Na.Othman Khamis.OMPR.

Kikao cha Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kushughulikia Masuala ya Muungano kimekutana  Ikulu Jijini Dar es salaam chini ya Mwenyekiti wake Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

Kikao hicho kimeitishwa mahsusi kwa lengo la kusaini hali za makubaliano za kuondoa Hoja  Tano za Muungano zilizokwishapatiwa ufumbuzi zinazohusu Ushirikishwaji wa SMZ kwenye Masuala ya Kikanda na Kimataifa na Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Nyengine ni Gharama za kushusha Mizigo Bandari ya Dar es salaam kwa Mizigo inayotoka Zanzibar, Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia, Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya pamoja na SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano mambo ambayo kwa pamoja yana mchango mkubwa katika kuimarisha Muungano wa Tanzania.

Saini ya  Hati ya Ushiriki wa SMZ kwenye masuala ya Kikanda na Kimataifa na ile ya Ushiriki wa Zanzibar katika Jumuiya ya Afrika Mashariki  iliwekwa na Waziri wa Mambo ya Nje Profesa Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa SMT Profesa Kilangi kwa upande wa SMT na ule wa SMZ ikawekwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mh. Issa Haji Ussi Gavu na Mwanasheria Mkuu wa SMZ Mh. Said Hassan Said.

Hati ya Gharama za kushusha Mizigo ya Wafanyabiashara katika Bandari ya Dar es salaam kutoka Zanzibar ilitiwa na Waziri wa Biashara wa SMT Mh. Inocent Mashungwa na Mwanasheria Mkuu wa SMT Profesa Kilangi kwa upande wa SMT na Waziri wa Biashara Zanzibar Balozi Amina Salum na Mwanasheria Mkuu wa SMZ Mh. Said Hassan Said.

Ile Hati ya Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia saini ikawekwa na Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Zanzibar Mh. Salama Aboud Talib na Mwanasheria Mkuu wa SMZ Mh. Said Hassan Said kwa upande wa Zanzibar na Mh. Madac Kalemani na Mwanasheria Mkuu wa SMT Profesa Kilangi kwa upande wa SMT.

Hati ya Utaratibu wa Vikao vya Kamati ya pamoja na SMT na SMZ ya kushughulikia Masuala ya Muungano ikawekwa saini na Katibu Kiongozi wa SMT Balozi John Kijazi na Mwanasheria Mkuu wa SMT Profesa Kilangi kwa upande wa SMT wakati upande wa Zanzibar ukawakilishwa na Katibu Mkuu Kiongozi Dr. Abdulhamid Yahya Mzee na Mwanasheria Mkuu wa SMZ Mh. Said Hassan Said.

Akizungumza katika Tukio hilo la Kihistoria Mwenyekiti wa Kamati hiyo Makamu wa Rais wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan alisema kitendo hichi ya utiaji saini hati hizo ni mwanzo mzuri wa Serikali zitakazokuja mara baada ya Uchaguzi kutekeleza kwa urahisi majukumu yake.

Mh. Samia alitoa rai kwamba changamoto zilizopo na zile zinazojichomoza sio sababu ya kuutia doa Muungano wa Tanzania  na kuwakumbusha baadhi ya Watendaji wenye kigugumizi cha utekelezaji wa mambo yaliyopatiwa ufumbuzi  wabadilike mara moja.

Alisema ipo kila sababu ya kuwaenzi Waasisi wa Taifa la Tanzania Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Mzee Abeid Amani Karume walioweka misingi imara ya Umoja na Mashikamano wa Wananchi wa Tanzania Bara na Zanzibar.

Alitanabahisha kwamba si vyema  Watu wakabeza juhudi na faida zilizopatikana ndani ya kipindi cha Miaka 56 ya uwepo wa Taifa la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambalo limeongeza chachu ya Udugu wa Damu.

Makamu wa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania aliwaagiza Watendaji wote wa Ofisi za Wanasheria Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutoa ushauri wa Kisheria pale inapohitajika ili kuwarahisishia utatuzi wale wanaopewa jukumu la kutatua changamoto zinazojitokeza ndani ya Muungano.

Mheshimiwa  Samia aliahidi kwamba akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya pamoja ya Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ataendelea kuongeza ushirikiano ili lile lengo la kudumika kwa Muungano wa Tanzania lifikiwe vyema.

Akitoa maelezo katika tukio hilo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Hati hizo zitaongeza faida na ustawi mkubwa kwa  Vizazi vya sasa na hata vijavyo endapo Viongozi watakabeba jukumu la kusimamia masuala hayo watazitumia kumbukumbu na miongozo iliyopo na kuepuka migongano isiyo la lazima baina ya pande mbili.

 Alisema hicho ni kielelezo tosha kwamba Sekretarieti ya Kamati ya Pamoja inayowajumuisha Wajumbe  kutoka SMT na SMZ ipo hai na kufanya Kazi zake kwa ueledi mkubwa uliosheheni kiwango cha ushirikiano unaoonekana dhahiri kupitia hatua hiyo iliyuofikiwa.

Balozi Seif  aliwapongeza Wajumbe wa Kamati hiyo ya Sekretarieti kwa utendaji wao imara na kuwanasihi waendelee na kasi ili waweze kuzimaliza hoja zilizochukuwa muda mrefu kupatiwa ufumbuzi wake ambazo ni Mapendekezo ya Tume ya Pamoja ya Fedha, Usajili wa Vyombo vya Moto pamoja na Mgawanyo wa Mapato.

Alisema tokea kuanzishwa kwa utaratibu wa kudhughulikia hoja za Muungano kupitia Vikao vya Kamati ya Pamoja hoja nyingi zimepatia ufumbuzi ingawa hazikuweza kuondolewa katika orodha ya Hoja za Muungano kutokana na utaratibu wa kusaini hati za makubaliano kutokuwa mzuri na kuleta mkanganyiko katika utekelezaji wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba kuimarika kwa Muungano ni Moja miongoni mwa Vipaumbele vya Serikali zote mbili Nchini Tanzania ile ya SMT na SMZ kwa kinajumuisha mambo mengi ndani yake likiwemo suala la Uchumi.

Alisema Dunia inatambua  kwamba Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania n ni miongoni mwa Mataifa machache  Barani Afrika ambayo Uchumi wake unakua kwa kasi kubwa jambo ambalo limeiwezesha  kufikia katika Nchi za Uchumi wa Kati.

Balozi Seif alibainisha wazi kwamba mafanikio hayo yamepatikana ndani ya Muungano huo wa Serikali Mbili ulioasisiwa Mnamo Tarehe 26 Aprili Mwaka 1964 ukidumu kwa Miaka 56 sasa katika Misingi ya Umoja, Amani na Utulivu miongoni mwa Wananchi wake.

Alitahadharisha kwamba ni vyema kwa Viongozi Waandamizi wa Serikali zote mbili hasa wale wanaowahudumia moja kwa moja Wananchi wakajenga tabia ya kuifikia Jamii ili iweze kupata uelewa na kutambua juu ya hatua muhimu iliyofikiwa ya kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu changamoto za Muungano jambo ambalo litaondoa malalamiko ya baadhi ya Wananchi.

Naye kwa upande wake Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh.Kassim Majaliwa Majaliwa alisema Utaratibu uliojengwa na Kamati ya pamoja ya SMT na SMZ wa kufanya mapitio ya changamoto na kuzibaini katika mueleko wa kuzipatia ufumbuzi unafaa kuendelezwa wakati wote.

Mh. Majaliwa alisema Viongozi na SWananzi walio wengi ndani ya Ardhi ya Tanzania bado wana nia na shauku ya kuona Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania unazidi kushamiri licha ya changamoto ziazojichomoza kutokana na mabadiliko ya wakati.

“ Muungano wanaojivunia Watanzania unatokana na kuimarika kwa Umoja, Mshikamano unaostahiki kudumishwa wakati wote na pande zote”.Alisisitiza Mh. Majaliwa.

Waziri Mkuu wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania alifahamisha kwamba aliwapongeza Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuonyesha nia ya kuomba ridhaa ya Wabunge na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kupitia CCM.

Alisema hatua yao hiyoinadhihirisha namna gani wako tayari kusimamia  muongozo unaoelekeza jinsi ya kustawisha Maisha ya Watanzania Bara na Zanzibar chini ya Kamati ya Sekriterieti ya Kamati ya Pamoja  na SMT na SMZ iliyoonyesha kupevuka katika Dira ya kuusimamia Muungano huo.

Akitoa salam na kuaga rasmi kwenye  Kikao hicho ambacho alikuwa Mjumbe Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa wa Serikli ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ambae pia ni Mgombea wa Urais wa Zanzibar kwa Tiketi ya CCM Dr. Hussein Ali Mwinyi alisema hafla hiyo ni kitendo mahsusi kinakacholeta mustakaba mwema wa Taifa la Tanzania.

Dr. Hussein ambae alikuwa Mjumbe wa Kikao hicho tokea Mwaka 2006 alipokuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano alieleza kwamba Serikali zote mbili endapo zitapata ridhaa ya Wananchi walio wengi katika uchaguzi Mkuu zitabeba dhima ya kukamilisha changamoto zilizobakia ndani ya Muungano.

Mapema Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Raia wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano anayesimamia Mazingira na Muungano Mh. Mussa Azzam Zungu alisema kuchelewa kusainiwa kwa Hati hiyo kunatokana na Taifa kukumbwa na Maambukuzi ya Virusi vya Corona pamoja na Kipindi cha Bajeti kwa Serikali zote Mbili.

Mh. Zungu alisema ikiachiliwa mbali Hoja Nne zilizokwisha patiwa Ufumbuzi na kuwekwa Saini Hati za Makubaliano lakini inatia moyo kuona zipo Hoja nyengine Sita nazo tayari zimeshapatiwa ufumbuzi zikisubiri Baraka kutoka kwa Kamati ya Pamoja ya SMT na SMZ ya kusimamia Kero za Muungano.

Alibainisha kwamba Viongozi wa Kamati hiyo wanaendelea na jitihada za za kumaliza changamoto zilizobakia mara tu baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ili changamotoi hizi zibakie kuwa Historia ndani ya Muungano wa Tanzania uliodumu kwa takriban kwa Miaka 56 sasa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.