Habari za Punde

Raius wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamade Shein Amelifungua Jengo Jipya la Mama na Mtoto Hospitali ya Kivunge Mkoa wa Kaskazini Unguja leo 13/10/2020.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akikata utepe kulifungua Jengo Jipya la Mama na Mtoto lilioko katika eneo la Hospitali ya Kivunge Wilaya ya Kaskazini "A" Unguja hafla hiyo imefanyika leo 13/10/2020 na (kulia kwa Rais) Waziri wa Afya Zanzibar Mhe. Hamad Rashid Mohammed na Daktari Dhamana wa Hospitali ya Kivunge Dkt. Tamim Hamad Said na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mhe Vuai Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka madaktari na wauguzi pamoja na watoa huduma za afya hapa nchini kuipenda kazi yao, kuwa na huruma, kuwa wastahamilivu na wenye kufuata maadili ya kazi yao.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika uzinduzi wa jengo la Mama na Mtoto katika hospitali ya Wilaya Kivunge, Mkoa wa Kaskazini Unguja, ambapo viongozi kadhaa walihudhuria akiwemo Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Mgeni Hassan Juma, Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Katibu Mkuu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee pamoja na viongozi wengine wa Serikali, vyama vya siasa na wananchi.

Katika maelezo yake, Rais Dk. Shein aliutaka uongozi wa Wizara hiyo kuhakikisha suala la kufuata na kutii maadili ya kazi hiyo linazingatiwa wakati wote na isitokezee kuona jambo la kawaida kwa daktari kutoa lugha isiyofaa kwa wananchi wanaofuata huduma hospitalini..

Aidha, Rais Dk. Shein alisema kuwa jukumu la Serikali ni kuhakikisha kwamba mipango yote iliyopangwa katika kuimarisha sekta ya afya inatekelezwa kwa ufanisi pamoja na huduma zinazotolewa katika hospitali na vituo vya afya zinakidhi mahitaji kwa wananchi.

Ambapo pia, Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuiikemea tabia ya Idara ya Upasuaji wa mifupa katika hospitali ya MnaziMmoja ya kuwatolesha wananchi pesa kwa ajili ya  kununulia dawa ama vifaa tiba kwani tayari Serikali imetangaza kuwa matibabu bure hivyo, Idara hiyo inaharibu dhana hiyo.

Kutokana na hali hiyo aliutaka uongozi wa Wizara ya Afya kulitafutia ufumbuzi wa haraka suala hilo na Idara hiyo ishughulikiwe kama zinavyoshughulikiwa Idara nyengine hasa ikizingatiwa kwamba suala la dawa si tatizo kwani Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa ajili ya kununulia dawa.

Aliongeza kuwa ndio maana Serikali imekuwa ikiongeza bejeti ya Wizara ya Afya kila mwaka pamoja na bajeti ya kununulia dawa ili kuondosha changamoto zilizokuwepo hapo kabla ambapo bajeti ya Wizara hiyo imeongezeka kutoka TZS bilioni 10.81 mwaka 2010/2011 hadi kufikia TZS bilioni 104.24 mwaka 2019/2020.

Alieleza kuwa bajeti ya kununulia dawa imeongezeka kutoka TZS bilioni 7.0 mwaka 2017/2018 hadi kufikia TZS bilioni 17.7 mwaka 2020/2021 ambapo kiwango hicho sawa na ongezeko la asilimia 152 ya bajeti ya dawa ya mwaka 2017/2018.

Kutokana na mafanikio hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa wananchi wanathamini juhudi hizi na wanafurahi kuona kwamba dawa nyingi zinapatikana katika hospitali za hapa nchini na zinatolewa bure hivi sasa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kuwepo kwa jengo hilo kubwa la ghorofa mbili na miundombinu bora ya barabara kutazidi kuziimarisha huduma za mama na mtoto pamoja na huduma nyengine zinazotolewa katika hospitali hiyo.

Alieleza kuwa kupandishwa daraja kwa hospitali hiyo kunatokana na wazo la ASP tangu mwaka 1963 na baada ya hapo iliendelea kupandishwa hadhi kutokana na hadhi na maendeleo ya hapo baadae huku akieleza kuwa mabadiliko hayo ni utekelezaji wa dhamira ya Waasisi wa Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 ya kutoa huduma za afya bora na bure kwa wananchi wote wa Zanzibar na kwa msingi wa usawa.

Sambamba na hayo, Rais Dk, Shein alieleza kuwa mafanikio yaliyopatikana katika hospitali ya Wilaya ya Kivunge na ile ya Makunduchi yamechangiwa na viongozi na watendaji wa Mradi wa Uimarishaji wa huduma za Afya Zanzibar (Health Imrovement Project Zanzibar-HIPZ) na kutumia fursa hiyo kumpongeza Dk Ru MackDonagh kutoka Uiengereza na viongozi wa Wizara ya Afya kwa masihrikiano yao katika kufanikisha mradi huo.

Aliongeza kuwa miongoni mwa mafanikio hayo yaliyopatikana katika mradi huo wa HIPZ ni kuweza kutoa na kuendelea kuziimarisha huduma za mama na mtoto ambapo mafanikio hayo yako wazi kwa wananchi wote wanaotumia hospitali hizo.

Alieleza kuwa takwimu zinaonesha kuwa katika mwaka wa fedha 2019/2020 jumla ya kina mama 5091 wamejifungulia Hospitali ikilinganishwa  na kina mama 2025 waliojifungulia hapa katika mwaka 2014/2015.

Alieleza kuwa Hospitali hiyo imeweza kupunguza wagonjwa wanaopelekwa Mnazi Mmoja kwa ajili ya matibabu zaidi hasa upasuaji wa mama wajawazito kutoka kumi kwa mwezi hadi watano.

Alieleza kuwa juhudi za makusudi zimechukuliwa na Serikali ya Awamu ya Saba na Awamu zote zilizopita katika kuhakikisha huduma za afya zinaimarika na Serikali hivi sasa imepata nguvu kufundisha madaktari wengine hatua ambayo pia, imesaidia kuongezeka kwa madaktari.

Alieleza kuwa ujenzi wa miundombinu ya barabara iliyo bora imesaidia katika kuimarisha sekta ya afya katika hospitali ya Wilaya Kivunge  na kuwawezesha wananchi wote wa Wilaya ya Kaskazini A, na Wilaya nyengine kufuata huduma zinazotolewa hospitalini hapo kwa urahisi.

Rais Dk. Shein pia, alieleza kuwa Serikali imeweza kupiga hatua kubwa katika kuendeleza sekta ya afya ndani ya miaka mitano kama ilivyotakiwa katika Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 102 (c) ikiwa ni pamoja na kuhakikisha hospitali ya Makunduchi na Kivunge zinafikia daraja na kiwango cha hospitali za Wilaya.

Rais Dk. Shein alitoa nasaha zake na kuwataka wananchi kuwachagua viongozi wenye sifa kutoka CCM na kutowachagua viongozi ving’ang’anizi ili huduma za afya ziendelee kama ilivyofanya Awamu zote huku akiwataka kuimarisha amani,umoja na utulivu kwa lengo la kuleta maendeleo.

Waziri wa Wizara ya Afya Hamad Rashid Mohammed  alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Shein kwa mafanikio makubwa yaliopatikana katika sekta ya afya.

Nae Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Halima Maulid Salum alieleza kuwa jengo hilo limejengwa na Kampuni ya Worlrd Class Engineerring Company Limited (WCEC Limited) kwa gharama ya TZS Bilioni 4 ambapo TZS bilioni 3.6 zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na milioni 400 zimetolewa na UNFPA kupitia Mradi wa Afya Bora.

Alisema kuwa lengo kuu la ujenzi wa jengo hilo ni kutoa huduma bora za afya kwa wananchi ili kupunguza vifo vya akinamama vinavyotokana na uzazi ambapo  mwanzo Hospitali ya Kivunge ilikuwa na vitanda 72 na hivi sasa jengo jipya la Mama na Mtoto pekee linauwezo wa vitanda 140 na kufanya jumla ya vitanda vya hospitali hiyo kufikia 212.

Alieleza kuwa jengo hilo lina ghorofa mbili ambapo sehemu ya chini ina wodi 4, wodi ya kwanza ya kinamama kabla ya kujifungua, wodi ya pili za kinamama baada ya kujifungua na wodi ya uangalizi baada ya upasuaaji.

Aidha alisema kuwa vipo vyumba vitano vya kujifungulia, vyumba vya wauguzi viwili, vyumba vya Daktari viwili na sehemu ya mapokezi ambapo pia ghorofa ya kwanza ni maalum kwa ajili ya watoto walio chini ya miaka mitano yenye wodi tano ambazo ni wodi ya watoto wachanga, wodi ya kangaroo, chumba cha Wagonjwa mahututi (ICU), na vyumba viwili kwa ajili ya kliniki.

Ghorofa ya pili ina wodi sita kwa ajili ya wanawake wenye matatizo yanayohusiana na uja uzito na ukumbi wa mkutano ambapo pia, Hospitali hiyo imeongeza madaktari kutoka 10 mwaka 2015 hadi 22, wauguzi 85 kutoka 52 na Anastersia 5, Daktari Bingwa wa wanawake mmoja, Daktari Bingwa wa watoto mmoja. Radioslogist wanne na wahuhudumu wa afya 35 kutoka 23.

Mapema Mwakilishi wa UNFPA Peter Matinga alitoa pongezi kwa uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa juhudi zake kubwa za kuendelea kuimarisha sekta ya afya na kuahidi kuwa Shirika hilo la Umoja wa Mataifa litaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya afya.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.