Habari za Punde

SERIKALI YATENGA BILIONI 1 KUTATUA CHANGAMOTO YA HUDUMA YA MAJI JIJINI DODOMA

Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge alipomtembelea ofisini kwake kabla ya ziara ya kukagua mojawapo ya kisima kinachojengwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma.

Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo (kushoto) akitoa ufafanuzi kuhusu visima vya maji vinavyojengwa eneo la Ihumwa wakati wa kikao kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge. Wengine ni watumishi kutoka Wizara ya Maji.
Mojawapo ya eneo la Ihumwa linalojengwa kisima chenye kitakachokuwa na mita za ujazo elfu tatu kwa siku zitakazosaidia kupunguza tatizo la maji maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dodoma.
Mojawapo ya eneo la Ihumwa linalojengwa kisima chenye kitakachokuwa na mita za ujazo elfu tatu kwa siku zitakazosaidia kupunguza tatizo la maji maeneo ya pembezoni mwa jiji la Dodoma.
Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga (kushoto) akikagua uchimbaji wa kisima kinachojengwa eneo la Ihumwa alipofanya ziara katika eneo hilo jijini Dodoma.
 

Na Happiness Shayo- Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Maji imeipatia Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) kiasi cha shilingi bilioni 1 ili kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji katika maeneo yenye changamoto ya huduma hiyo jijini Dodoma.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga alipotembelea kisima kimojawapo kati ya visima vinavyochimbwa katika eneo la Ihumwa jijini Dodoma.

“Hili linafanyika kutokana na ongezeko la mahitaji ya huduma ya maji katika maeneo mbali mbali ya jiji la Dodoma hasa maeneo ya pembezoni” Mhandisi Sanga amesema. 

Aidha, amefafanua kuwa kuhamia kwa Serikali jijini Dodoma ni fursa kwa taasisi za maji zilizoko Dodoma kutatua changamoto za huduma ya maji wanazozipata wananchi wa Dodoma.

Mhandisi Sanga amongeza kuwa Serikali ina mipango ya muda mfupi, ya kati na ya muda mrefu ya kutatua changamoto za upatikanaji wa huduma ya maji.

“Mipango ya muda mfupi ni kama ujenzi wa visima vya dharula katika eneo la Ihumwa na mipango ya muda wa kati ni ujenzi wa bwawa la Farkwa na muda mrefu ni kutoa maji kutoka ziwa Victoria” amefafanua Mhandisi Sanga.

Naye, Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Mhandisi David Pallangyo ameongeza kuwa ujenzi wa kisima hicho eneo la Ihumwa ni moja wapo ya visima kadhaa vitakavyo weza kuzalisha maji na kuyatoa kuyapeleka hadi mjini ili kupunguza tatizo la maji eneo la mjini.

“Vitachimbwa visima vinavyozalisha si chini ya mita za ujazo elfu tatu kwa siku zitakazo saidia kupunguza tatizo la maji maeneo ya pembezoni kama Mwangaza, Njedengwa, Ihumwa na maeneo mengine ya mjini.

Mhandisi Pallyangyo amesema mradi wa ujenzi wa visima eneo la Ihumwa utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 2.4.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Bilinith Mahenge ameupongeza uongozi wa DUWASA kwa kutatua changamoto za maji jijini Dodoma na kuwataka kuongeza ushirikiano ili kufikia malengo.

Lengo la juhudi zote za Serikali ni kuhakikisha huduma ya maji safi na uondoshaji wa maji taka zinakuwa zauhakika zinazoendana na hadhi ya jiji la Dodoma ambalo ndio makao makuu ya nchi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.