Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla Aanza Kazi

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla akivishwa shada la Mauwa na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar mara baada ya kuingia ndani ya Jengo la Afisi yake kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa kushika wadhifa huo.
Makamu wa Pili wa Rais  Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akimkabidhi rasmi Ofisi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mpya Mh. Hemed Suleiman Abdalla mapema asubuhi.
Makamu wa Pili wa Rais  Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kushoto akitoa nasaha mara baada ya kumkabidhi Ofisi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mpya Mh. Hemed Suleiman Abdalla Vuga Mjini Zanzibar.
Makamu wa Pili wa Rais  Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akimkabidhi nyenzo za Kazi ikiwemo Ilani Mpya ya Uchaguzi ya CCM Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mpya Mh. Hemed Suleiman Abdalla Vuga Mjini Zanzibar.
Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed akimkabidhi ngao Maalum Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman  kama ishara ya kukaribishwa rasmi kwenye Ofisi hiyo kakiwa Kiongozi Mkuu.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdalla akizungumza na Viongozi Waandamizi wa Ofisi hiyo  mara baada ya kuwasili kuchukuwa dhamana yake kufuatia uteuzi wake wa hivi karibuni.
Picha na OMPR.

Na.Othman Khamis. OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla amewaomba Viongozi na Watumishi wa Umma wajitambue na kujitathmini katika utekelezaji wa majukumu yao waliopewa  na Taifa  ili ile kiu ya kuwatumikia Wananchi ifanikiwe vyema.

Alisema baadhi ya Viongozi ama Watendaji watakaojihisi kwamba hawaendani na kasi ya Serikali iliyoanza kazi zake muda mfupi uliopita baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu ni vyema wakaondoka kwa Heshima katika maeneo yao ya kazi waliyokabidhiwa.

Mhe. Hemed Suleiman Abdalla alitoa kauli hiyo muda mfupi baada ya kupokewa ndani ya Ofisi yake Mpya kama Mtendaji Mkuu wa Serikali wakati akizungumza na Viongozi wa Idara na Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar hapo Vuga Mjini Zanzibar.

Alisema hapendezi kuona baadhi ya Viongozi wa Taasisi na Wakuu wa Vitengo wanajifikiria maslahi yao binafsi hasa fursa za Masomo hata zile safari za nje ya Zanzibar zinazoambatana na masurufu bila ya kujali haki za Watendaji wao wa ngazi ya chini.

“ Haipendezi na haitawezekana kuona Viongozi Waandamizi na Wakuu wa Taasisi wanajipatia maposho ya safari na wasindwe kuwapatia haki zao Wafanyakazi wao wa ngazi ya chini”. Alifafanua Mh. Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitanabahisha wazi kwamba yeye akiwa Mtendaji Mkuu wa Shughuli za Serikali hatakuwa tayari kumbeba Kiongozi au Mtumishi ye yote aliyepewa dhamana na akashindwa kuitekeleza katika eneo lake la kazi.

Alionya kwamba akimgundua Kiongozi anayetumia vibaya Rasilmali za Umma aelewe kwamba atakwenda na maji kwa vile hatasita kumchukulia hatua za kinidhamu mara moja kutokana na tabia hiyo mbaya isiyokubalika katika Utumishi wa Umma

Aliwataka Watendaji hao wa Utumishi wa Umma wajisafishe  kwa vile wao ndio wanaosimamia utendaji wa Serikali na kuacha malalamiko yasiyo na msingi kwani pale vinapojitokeza kikwazo katika uwajibikaji wao taratibu ziko wazi za kuwasilisha changamoto zao zinazowakabili katika ngazi ya juu.

Mheshimiwa Hemed Sueiman Abdalla aliwashukuru Viongozi Wakuu  waliostaafu wa Serikali ya Awamu ya Saba Dr. Ali Mohamed Sheni na Balozi Seif Ali Iddi kwa ulezi wao mwema uliopelekea kumwajengea daraja ya pale walipofikia Viongozi wapya.

Aliwaomba Viongozi hao Wastaafu waendelee kuacha milango wazi kwa Viongozi Wapya ili pale watakapohitaji mawazo na busara zao katika uwajibikaji wa Utumishi wa Umma waweze kuitumia fursa hiyo adhimu.

Mapema akimkabidhi Ofisi pamoja na Nyenzo za Kazi Mtendaji Mkuu huyo Mpya wa Shughuli za Serikali Mh. Hemed Suleiman Abdalla, Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema uteuzi wa Rais wa Zanzibar kumpa dhamana Mh. Hemed unatokana na ujemedari wake katika kusimamia maslahi ya Wananchi.

Balozi Seif alisema kwa umahiri wake Mheshimiwa Hemed Suleiman hana shaka na jukumu alilokabidhiwa la Umakamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar na kuwaomba Viongozi na Watendaji wa Ofisi hiyo waendelee kumpa ushirikiano kama aliyopewa yeye wakati wa Utumishi wake.

Akitoa Taarifa ya makaribisho hayo ya Ofisi Katibu kuu Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Nd. Shaaban Seif Mohamed alisema kwa niaba ya Wafanyakazi wa Ofisi hiyo alimpongeza Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdalla kwa kuteuliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Nd. Shaaban alisema makaribisho ya Wafanyakazi hao kwake Mheshimiwa  Hemed ni ishara ya kumkubali kufanya kazi pamoja katika kuona usimamizi wa Serikali unaendelea kutoa huduma kwa Umma.

Alifahamisha kwamba Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa mujibu wa Sheria ndio msimamizi Mkuu wa shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akitoa shukrani kwa niaba ya Viongozi na Wafanyakazi wote wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Naibi Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo Nd. Abdulla  Hassan Mitawi alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kupewa ushirikiano ili jukumu walilokabidhiwa na Taifa lifanikiwe vyema.

Ndugu Mitawi alitumia nafasi hiyo kumshukuru na kumpongeza Makamu wa Pili wa Rais Mstaafu wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwa busara zake zilizochangia kuwapa Msukumo Viongozi na Watendaji na hatimae kufanikiwa katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alipokewa kwa shangwe na vigere gere na Viongozi Waandamizi pamoja na Watendaji wa Ofisi hiyo wakati alipoingia kwenye Majengo hayo kuanza jukumu lake alilopatiwa na Taifa.

Mapokezi hayo ya aina yake yaliambatana na kuvishwa shada la maua kama ishara ya kumpokea ramsi Mtendaji Mkuu huyo wa Shughuli za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Ofisini Vuga Mjini Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.