Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Akihutubia Hafla ya Semina ya Viongozi Waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Ilioandaliwa na Benki ya CRDB.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akihutubia katika hafla ya Semina Maalum ilioandaliwa na Benki ya CRDB kwa Viongozi Waandamizi na Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar iliofanyika katika viwanja Marina Hoteli ya Verde Mtoni Jijini Zanzibar jana Usiku 20/11/2020.

SERIKALI ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane imeamua kufanya Mapinduzi ya kiuchumi kwa kuendeleza Uchumi wa Buluu na kuweka mkazo katika kuziimarisha sekta za huduma, ikiwemo sekta ya utalii, ambayo ni muhimili mkuu wa uchumi wa Zanzibar.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo katika hafla iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa viongozi waandamizi na Wajumbe wa baraza la Wawakilishi, iliyofanyika katika viwanja vya Hoteli ya Verde, Mtoni nje kidogo ya Jijila Zanzibar.

Katika hotuba yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kwamba kutokana na udogo wa ardhi kila uchao zinaendelea kuibuka changamoto katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo ambapo ardhi yote ya Unguja ni kilomita za mraba 1,666 na Pemba ni kilomita za mraba 988 ambapo ukubwa huo hauendani na ongezeko la watu.

Alisema kuwa zamani ardhi ilitegemewa kwa kilimo na wananchi wengi waliweza kuendesha maisha yao kwa kutegemea shughuli za kilimo na ufugaji ambapo leo ardhi hiyo hiyo inategemewa sana kwa ujenzi wa makaazi, viwanda na shughuli nyengine za uchumi wa karne hii ya 21.

Kwa kulizingatia tatizo hilo la ardhi, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kutumia rasilimali mbadala ya bahari pamoja na kuimarisha sekta za huduma.

Alisema kuwa Serikali imelenga kuendesha na kukuza uchumi wa buluu kwa kuzitumia kikamilifu rasimali zinazohusiana na bahari, ikiwemo shughuli zinazohusu sekta ya utalii, utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi, uvuvi na bahari kuu, ufugaji na usindikaji wa samaki, ukulima wa mwani, pamoja na mazao mengine anuwai ya bahari.

Rais Dk.Mwinyi alimuahidi  Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela kumpa timu maalum  ya kushirikiana na Benki hiyo katika kufanya kazi huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Nane imeamua kutoa ushirikiano mzuri kwa  sekta binafsi ambapo imekusudia kwa dhati kuwa wadau wezeshi wa sekta binafsi kwa kuwawekea mifumo rafiki na mazingira mazuri ya uwekezaji na uendeshaji wa biashara ili waweze kuendesha shughuli zao kwa ufanisi bila ya kikwazo.

“Nimefurahishwa sana kusikia kwamba Benki ya CRDB imehamasika kutokana na mwelekeo wa maendeleo na dira yangu ya kuijenga Zanzibar mpya na kuamua kutuunga mkono katika jitihada zetu za kufanikisha malengo yetu tuliyoyakusudia, ahsanteni kwa moyo wenu huo wa kizalendo”,alisema Dk. Hussein Mwinyi.

Aidha, alisema kuwa hamu ya Benki ya CRDB ya kushirikiana na Serikali hasa katika masuala ya uchumi wa Buluu imemtia moyo na ana imani kubwa kwamba mashirikiano hayo yataongeza kasi ya uzalishaji na sekta zinazotegemea mazao ya baharini kama vile viwanda na usindikizaji vitaibuka na kuimarika.

Rais Dk. Hussein aliendelea kusisitiza dhamira ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kukifanya kisiwa cha Pemba kuwa eneo la kimkakati la uwekezaji ambapo pia, Serikali imejipanga kuendeleza utalii, kukuza biashara na viwanda na kushajiisha uwekezaji katika maeneo mapya ya uchumi.

Katika hotuba yake hiyo aliitaka Benki hiyo kuwa na ujasiri wa kuwapatia mikopo wananchi wanaojishughulisha katika sekta ya kilimo, uvuvi wa kawaida, ujasiriamali na ufugaji, wauzaji wa biashara ndogo ndogo na za kati  wanahitaji kuwezeshwa zaidi ili biashara zao ziwaletee kipato chenye tija itakayoweza kuwakwamua na umasikini.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliihakikishia Benki hiyo ya CRDB kwamba Serikali iko tayari kushirikiana na Benki hiyo na ushirikiano huo utaweza kuleta uchumi mpya hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba hio ni azma ya Serikali ya Awamu ya Nane.

Kwa lengo la kupanua wigo wa ushirikiano baina ya Serikali na Benki ya CRDB Rais Dk. Hussein alipendekeza kwamba CRDB iangalie zaidi suala la uwekezaji katika miradi mikubwa ya maendeleo hapa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Dk. Hussein  aliwataka wafanyabiashara na wananchi wote wenye fedha nje ya nchi kuzileta fedha hizo nyumbani ili waweze kuijenga nchi yao na kuwaahidi kwamba hawatahojiwa wala kubughudhiwa kwa aina yoyote. “Tunataka kuijenga nchi yetu na nchi hujengwa na wananchi wenyewe.

Alieleza haja kwa Benki ya CRDB kufikiria kufungua Tawi jengine katika mji wa Wete kwani huduma inazotoa benki hiyo katika Tawi lake ililolifungua Chake Chake mwezi Julai, 2017, zimewavutia wateja wengi kwa hivyo huu ni wakati muwafaka wa kufikiria suala hilo bila ya kuchelewa.

Aliongeza kuwa  wananchi wengi wanaamini kwamba Benki kazi yake ni kuweka fedha za matajiri tu, kumbe kuna fursa nyingi muhimu zinazowafanya wale wasiokuwa na pesa waweze kuzipata na kuzitumia kila siku katika kuwaendeshea maisha yao, kwa mnasaba huo ipi haja kwa Benki ya CRDB kuwaelimisha wananchi kuhusu huduma hiyo.

Nae Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid kwa niaba ya Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi aliahidi kutoa mashirikiano makubwa na benki hiyo  na kueleza imani yake kubwa kwamba mafanikio makubwa yatapatikana.

Waziri wa Fedha na Mipango  Jamali Kassim Ali nae kwa upande wake alisema kuwa wananchi walio wengi hasa wa ngazi ya chini wanahitajia huduma za Benki hiyo, hivyo ni vyema wakachukua juhudi za makusudi kuwafikia.

Mapema Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Abdulmajid Nsekela akiwasilisha mada juu ya shughuli za Benki hiyo na jinsi ilivyojipanga katika kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Nane na kueleza kwamba Benki hiyo iko tayari na kumuomba Rais aipe timu kwa ajili ya kufanya kaziili kuleta maendeleo ya kasi na chanya.

Alisema kwamba Benki ya CRDB imedhamiria kufanyakazi kwa karibu zaidi na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ikidhamiria kuunga mkono katika kujenga uchumi imara wenye kutegemea rasilimali za bahari yaani “Uchumi wa buluu”.

"Tunafahamu Serikali ya Awamu ya Nane imejipanga kuleta Mapinduzi katika sekta zote za maendeleo na sisi tumeweka mkakati wa ushiriki wetu kuanzia sekta ya utalii, kilimo, uvuvi, ujenzi, viwanda, miundombinu, elimu na afya” alisema Nsekela huku akibainisha kuwa uwezeshaji huo unafanyika kuanzia kwa wajasiriamali wadogo, wakati na kwa makampuni makubwa.

Alisisitiza kwamba Benki ya CRDB imejidhatiti vya kutosha katika kutoa mikopo ya maendeleo usahili wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Tabia nchi (GCF) ulioipata Benki hiyo mwishoni mwa mwaka jana umesaidia kwa kiasi kikubwa kuongeza uwezo wa benki hiyo kutoa mikopo ambapo sasa hivi inaweza kutoa hadi dola za kimarekani milioni 250 kwa mradi mmoja.

“Hizi ni fedha nyingi sana ambazo tumedhamiria kuzielekeza katika miradi ya maendeleo nchini kwa kushirikiana na Serikali na sekta binafsi,” aliongezea Nsekela.

Aidha Nsekela alisema Benki ya CRDB inaendelea na zoezi la uunganishwaji wa mfumo wa kidijitali wa malipo katika taasisi za Serikali na binafsi ili kuongeza ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.“tunafanya hivi tukiwa na uzoefu wa kuisaidia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kukusanya mapato katika sekta ya utalii ambapo zilikukusanywa fedha zinazofikia dola za kimarekani milioni 12 mwaka 2019 kutoka dola laki 4 mwaka 2014,” alisema Nsekela.

Mkurugenzi huyo alieleza azma ya Benki yake kutoa ushirikiano kwa Serikali ya Awamu ya Nane ili kuifanya Zanzibar kuwa Dubai yakesho sambambana kuonesha utayari wake kwa kusaidiana naS erikali kutafuta wawekezaji kuja kuekeza Zanzibar.

Benki ya CRDB inamatawi mawili Zanzibar ambapo moja lipo Unguja na jingine Pemba ambapo benki hiyo pia, imefanikiwa kupanua wigo wake wa huduma kupitia CRDB, Wakala zaidi ya 160 ambao wanasadia kutoa huduma kwa Wazanzibari zaidi ya 300,000 na tayari mikopo ya benki hiyo hapa Zanzibar imefikia shilingi bilioni 101 ambazo zimekopeshwa katika maeneo mbali mbali huku wadau wake kwa asilimia 80 ni Watanzania.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.