Habari za Punde

Kampuni ya Vault kutoka Marekani yatia nia kuwekeza kwenye mradi mkubwa wa utalii ukanda wa Micheweni kisiwani Pemba

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla wa Tatu kutoka Kushoto akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Vault yenye mastakimu yake Nchini Marekani ukiwa na Tawi lake Nchini Tanzania wenye nia ya kuwekeza Mradi Mkubwa wa Utalii Micheweni Pemba.
Mwakilishi wa Kampuni ya Kimataifa ya Vault Tawi la Tanzania Bwana Said Ally Said wa kwanza kushoto akielezea changamoto za uchelewaji wa kupata kibali cha kuendeleza Mradi wa Bare foot Micheweni Pemba.
Mwakilishi wa Kampuni ya Vault Bwana Hirsi Divir wa Tatu kutoka Kulia akifafanua Mradi mkubwa wa Sekta ya Utalii uliokusudiwa kuanzishwa Micheweni Pemba ukiwa na Awamu Tatu katika utekelezaji wake.
Meneja wa Taasisi ya Kizalendo ya Big Tahfif Pemba, Nd. Mohamed Makame Mohamed akisisitiza umuhimu wa kuanzishwa kwa Mradi huo katika Ukanda wa Micheweni utakaosaidia kipato cha Waananchi wa eneo hilo.

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kati kati akiwa katika Picha ya pamoja na Uongozi wa Kampuni ya Vault pamoja na ile Taasisi za Kizalendo ya Big Tahfif ya Micheweni.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Uongozi wa Kampuni ya Kimataifa ya Vault yenye mastakimu yake Nchini Marekani ukiwa na Tawi lake Nchini Tanzania umeiomba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuwapatia kibali kitakachowapa fursa ya kutekeleza Mradi mkubwa kwenye Sekta ya Utalii katika Ukanda wa Micheweni Kisiwani Pemba.

Mwakilishi wa Kampuni hiyo Bwana Hirsi Divir akiiongoza Timu ya Viongozi wa Kampuni hiyo iliyoambatana na wenyeji wao Taasisi ya  Kizalendo ya Tahfif ya Micheweni alitoa ombi hilo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla Vuga Mjini Zanzibar.

Bwana Divir alisema Kampuni yake tayari imeshafanya maombi ya kuanzisha mradi Mkubwa wa Bare foot katika ukanda wa Micheweni iliopangiwa kutekelezwa kwa Awamu Tatu na kuwasilishwa Serikalini kwa hatua za utekelezaji.

Mwakilishi huyo wa Kampuni ya Vault alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Mradi huo wa Bare foot umekusudia kujenga Mkahawa wa Kimataifa, Nyumba za Kulala Watalii na wageni na kumalizia Awamu ya Tatu ya uimarishaji wa Misitu katika eneo hilo.

Alisema Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} imepitia maombi yao na kuridhia kile walichokusudia kukitekeleza lakini baadhi ya Taasisi tokea Mwaka 2017 yalipowasilishwa maombi hayo hadi sasa bado hazijatoa Baraka zake.

Bwana Divir alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Wananchi wa Ukanda wa Wilaya ya Micheweni tayari wamesharidhia uwepo wa Mradi huo ambao utatoa nasafi kubwa za ajira kwao pamoja na kukuza Pato la Taifa.

Naye Mwakilishi wa Kampuni hiyo Tawi la Tanzania Bwana Said Ally Said  alisema Wawekeza wa Mradi huo wameingia Nchini muda mrefu lakini bado wanaendelea kuzunguushwa.

Bwana Said alisema inasikitisha kuona Kampuni hiyo tayari imeshaanza kulipa kodi kwa eneo la Ardhi  walilopata la Hekta Saba pamoja na Misitu licha ya kutokamilika kwa upatikanaji wa Leseni ya kuanza Miradi hiyo.

Kwa upande wake Meneja wa Taasisi ya Kizalendao ya Big Tahfif Pemba Nd. Mohamed Makame Mohamed alisema Wananchi wa Ukanda wa Micheweni Pemba wameupokea kwa moyo mkunjufu Mradi huo wanaoutazamia kuwa kichocheo cha muelekeo wa mafanikio yao Kiuchumi.

Nd. Mohamed kwa niaba ya Wananchi wa Micheweni wameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nan echini ya Jemedari wake Rais wa Zanzibar Dr. Hussein Ali Mwinyi kwa umakini wake wa kutoa fursa kwa Wawekezaji katika mwendo wa uharaka.

Akitoa masikitiko yake kutokana na usumbufu mkubwa uliopata Uongozi wa Kampuni hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alionya kwamba Serikali kamwe haitaruhusu kuendelea kufanyika uzembe wa aina hiyo wakati tayari imesharidhia kukaribisha Wawekezaji kuanzisha miradi yao.

Mh. Hemed alisema haipendezi kuona Muwekezaji ameonyesha nia ya kutaka kuwekeza Vitega Uchumi Nchini baada ya kushawishika lakini anaendelea kupata usumbufu na vikwazo vinavyochelewesha kuanza kwa Mradi husika kwa utashi wa ubinafsi wa Mtendaji.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwahakikishia Viongozi hao wa Kampuni ya Vault kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itachukuwa hatua za haraka katika njia ya kukwamua tatizo hilo kwa vile Jamii ya Wananchi wa Ukanda wa Micheweni imeshapata matumaini ya kujikomboa kiustawi kutokana na Mradi huo.

Alisema Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Hussein Mwinyi katika kuona Sekta ya Uwekezaji inapata ufanisi ameshaamua Mamlaka ya Uwekezaji Vitega Uchumi Zanzibar {ZIPA} itaimarishwa na kufanywa Kituo Rafiki kwa Wawekezaji { One stop Centre } ili kupata huduma zote zinazohusu masuala yote ya Uwekezaji.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.