Habari za Punde

Mbunge na Mwakilishi wa Jimbo la Welezo Washiriki Katika Maulid ya Kuzaliwa Mtume (S.A.W) Yalioandaliwa na Wazee wa Kituo cha Welezo Zanzibar.

MBUNGE wa Jimbo la Welezo Mhe.Maulid Saleh Ali wa pili kulia na Mwakilishi wa Jimbo hilo Mhe. Hassan Khamis Hafidh wa pili kushoto wakisikiliza nasaha za mmoja wa Wazee wanaoishi katika Kituo cha uangalizi wa Wazee Welezo mara baada ya kukamilika Hafla ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyoandaliwa na Wazee hao.
BAADHI ya Wazee wa Kituo hicho wakiwa na Mbunge wa Jimbo la Welezo Mhe.Maulid Saleh Ali, Mwakilishi wa Jimbo hilo Hassan Khamis Hafidh mara baada ya kukamilika Hafla ya Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yaliyoandaliwa na Wazee hao.


NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

MBUNGE wa Jimbo la Welezo Mhe.Maulid Saleh Ali amesema maendeleo yaliyofikiwa nchini yametokana na juhudi za kiutendaji zilizoasisiwa na wazee ambao hivi sasa wanahitaji uangalizi wa karibu katika maisha yao ya kila siku.

Kauli hiyo ameitoa wakati akizungumza mara baada ya kufanyika kisomo cha Maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W) yanayofanyika kila mwaka katika kambi ya uangalizi wa Wazee wasiojiweza Welezo Unguja.

Alisema pamoja na majukumu waliyonayo viongozi hao wa jimbo hilo bado wanajukumu la msingi la kuwa karibu na wananchi wa makundi mbalimbali hasa wale wenye mahitaji maalum.

Aliwapongeza wazee hao kwa maamuzi yao ya kuendeleza utamaduni wa kusoma maulid hayo kila mwaka jambo ambalo linatakiwa kuigwa na vituo vingine nchini.

Katika maelezo yake mbunge huyo, aliahidi kuendelea kuwa karibu na kituo hicho cha uangalizi wa Wazee sambamba na kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili ili nao wapate mahitaji muhimu kama walivyo wazee wengine nchini.

'' Nafurahi sana kujumuika nanyi katika mkusanyiko huu muhimu katika imani ya dini ya kiislamu wa kisomo cha Maulid ya Mtume Muhammad
(S.A.W), kwani hii ni ishara toka ya kudumisha upendo na umoja wenu katika eneo hili mnaloishi pia nakuahidi nitakuwa nanyi bega kwa bega endeleeni kuniombe dua njema na zenye kheir ili Allah aendelee kuniongoza kwa yaliyomema nami niendelee kukutumikieni kwa uadilifu uliotukuka.'', aliwambia Wazee hao.

Naye Mwakilishi wa jimbo hilo Mhe. Hassan Khamis Hafidh, alisema kuwa wazee hao ni kundi muhimu katika jamii kwani busara,ushauri na maono yao yanachangia uwajibikaji katika hatua mbalimbali za kimaendeleo.

Mhe.Hassan, alisema viongozi wa jimbo hilo wamejipanga vizuri kwa kuhakikisha wazee hao wanatatuliwa changamoto zao na kutunzwa kwa heshima zote.

Kwa upande wake Diwani wa Wadi ya Welezo Ramadhani Ali Juma, aliwashukru wazee hao kwa ushirikiano wao wa kuwaalika viongozi hao wajumuike pamoja katika hafla hiyo ya maulid ya Mtume Muhammad (S.A.W), na kuongeza kuwa ni kielelezo cha kuendeleza mahusiano mazuri baina ya viongozi na wananchi wao.

Wakizungumza kwa wakati tofauti Wazee hao wamewapongeza viongozi wa jimbo hilo kwa utamaduni wao wa kushirikiana na wananchi katika masuala mbalimbali ya kimaendeleo.

Walieleza kwamba wana imani kubwa na uongozi huo ambao kwa kipindi kifupi toka wamepewa dhamana ya uongozi wameonyesha ushiriki mkubwa katika mambo ya kijamii na ustawi wa kijamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.