Habari za Punde

Wizara ya Elimu kushirikiana na wadau mbali mbali wa Elimu kuhakikisha sekta ya Elimu inapiga hatua

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akisistiza jambo alipokuwa akizungumza na Mjumbe wa UNICEF Bi Maha Damaj,
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akizungumza na Mjumbe wa UNICEF Bi Maha Damaj, kwenye Ofisi za Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali alipofika kujitambulisha

Mjumbe wa shirika la Umoja wa mataifa UNICEF Bi Maha Damaj akisisitiza jambo alipofika kwenye Ofisi za Wizara ya Elimu na mafunzo ya amali alipofika kujitambulisha

Picha Na Maulid Yussuf WEMA


na Maulid Yussuf, Wema

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa Elimu ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kupiga hatua.
Akizungumza na ujumbe kutoka shirika la Kuhudumia watoto Duniani UNICEF wakati ulipofika ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja kwa ajili ya kujitambulisha amesema maendeleo ya elimu yanahitaji mashirikiano ya pamoja ili kuingeza ufaulu kwa watoto.
Mhe Simai amesema Kuna umuhimu mkubwa wa kuendelea kujenga vituo vya Amali, kuwa na walimu wenye ujuzi, kuboresha mitaala pamoja na kuwa na vitendea kazi ili kuboresha Elimu ya Amali na ufundi kwa lengo la kuwasaidia vijana kuweza kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri ajira kutoka Serikalini.
Pia Mhe Simai amesema wazazi na walezi nao wana fursa ya kuwafuatilia watoto wao kwa kushirikiana na Walimu ili kuhakikisha wanafanya vizuri katika masomo yao.
Hata hivyo ameliomba shirika la UNICEF katika kuionesha njia Zanzibar juu ya mbinu walizotumia Rwanda katika kukuza elimu hasa katika masomo ya sayansi, ili nayo iweze kupiga hatua.
Ujumbe huo umempongeza Mhe Simai kwa kuteuliwa kuwa Waziri wa Wizara hiyo ambapo wamemuahidi kumpa mashirikiano ya kutosha ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar yanafikiwa.
Kwa upande wake Mjumbe wa UNICEF Bi Maha Damaj, amesema UNICEF imejikita katika kusaidia sekta ya Elimu kwa kuhakikisha wanamaliza utoro katika Skuli za Zanzibar pamoja na kuhakikisha Wanafunzi wanapenda kusoma masomo ya sayansi.
Katika mazungumzo hayo pia alikuwepo Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Muhandisi Idrissa Muslim Hija ambae ameunga mkono mazungumzo hayo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.