Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Hemed Suleiman Atembelea Hoteli Zilizopata Ajali ya Moto.Pwani Mchangani.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiwa pamoja na Viongozi wa Serikali wakikagua maeneo mbali mbali yaliyoathirika na Moto uliozuka katika Hoteli ya Ocean Paradise na Tu Blue Bahari za Pwani Mchangani Mkoa Kaskazini Unguja.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mheshimiwa Leila Mohamed Mussa akielezea hatua zilizochukuliwa na Taasisi za Utembezaji Watalii Zanzibar za kuwatafutia Makaazi Mapya wageni waliokuwa katika Hoteli mbili zilizopata janga la Moto za Ocean Oaradise na Tui Blue Bahari.




Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akikipongeza Kikosi cha Zimamoto na Uokozi pamoja na Viongozi wa Mahoteli kwa kufanikiwa kuudhibiti Moto uliozuka kwenye Hoteli za Ocean Paradise na Tui Blue Bahari.

Timu ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi kilichohusika kupambana na Moto uliozuka katika Hoteli za Ocean Paradise na Tui Blue Bahari Pwani Mchangani.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na.Othman Khamis OMPR.

Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar kwa kushirikiana na Viongozi, Wafanyakazi wa Mahoteli na Wananchi wa maeneo jirani wamefanikiwa uuzima moto mkubwa uliozuka usiku wa  Manane na kuteketeza baadhi ya Majengo ya Hoteli za Ocean Paradise na Tui Blue Bahari zilizopo Pwani Mchangani Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Askari wa Kikosi hicho kutoka Vituo vya Mahonda na Kigunda walifika eneo hilo ndani ya muda wa Dakika 18 baada ya kuibuka tukio hilo liloripotiwa kuanza kutokea majira ya saa 8.33 za Usiku.

Harakati za kuuzima moto huo zilianza mara moja zikishirikisha pia Wafanyakazi wa Mahoteli jirani yanayozunguuka Hoteli hizo mbili na kufanikiwa kukamilika zoezi hilo Majira ya saa Tatu asubuhi kwa kupata nguvu za ziada kutoka Makao Makuu ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Kilimani Mjini Zanzibar.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla akiambatana na Viongozi tofauti wa Serikali na Wadau wa Sekta ya Utalii walifika eneo hilo la tukio kujionea hali halisi ya hasara iliyotokana na janga hilo pamoja na kuwapa pole Viongozi na Wafanyakazi wa Ocean Paradise na Tui Blue Bahari kwa vile ni wadau wakubwa katika kuchangia Pato la Taifa.

Akitoa Taarifa za awali kuhusiana na tukio hilo Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Mh. Ayoub Mohamed Mahmoud alisema Wageni wote waliokuwemo kwenye Hoteli hizo mbili wako salama wakati Moto huo ulipoanza kuibuka katika Jengo la Ufundi la Hoteli ya Ocean Paradise.

Mheshimiwa Ayoub alisema kasi ya Moto huo ilianza kuenea katika Tangi la Mafuta, Mkahawa ndani ya Hoteli ya Paradise na baadae kusambaa katika Hoteli ya Tui Blue Bahari ulioathiri sehemu ya Mapokezi, Utawala pamoja na vyumba vya kulala Wageni vipatavyo 96.

Naye Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mh. Leila Mohamed Mussa alisema Wageni 208 wa Hoteli ya Ocean Paradise yenye Wafanyakazi 170 na Wageni 129 wa Hoteli ya Tui Blue Bahari yenye Wafanyakazi 300 Wazawa wamehamishiwa Hoteli za Jirani.

Mheshimiwa Leila Mohamed alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba hatua hiyo ya hifadhi ya Wageni hao  ilikwenda sambamba na ule  utaratibu wa maombi mapya ya Wageni wanaotaka kuitembelea Zanzibar kipindi hichi.

Waziri huyo wa Utalii na Mambo ya Kale amewapongeza Viongozi na Wafanyakazi wa Taasisi zinazosimamia utembelezaji Watalii Nchini kwa kazi kubwa waliyoifanya kusimamia zoezi hilo licha ya changamoto ya baadhi ya Wageni kuamua kuendelea kubakia katika maeneo hayo.

Akitoa shukrani zake kutokana na kazi kubwa ya kizalendo iliyotekelezwa ya kukabiliana na athari hiyo ya Moto chini ya Kikosi cha Zimamoto na Uokozi Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema jamii imeshuhudia faida kubwa ya umuhimu wa kuwahi mapema kwenye matukio ya majanga.

Mheshimiwa Hemed aliwahakikishia Wawekezaji hao wa Sekta ya Utalii Nchini kwamba Serikali Kuu itaendelea kutoa ushirikiano wa kina katika kuona uhalisia wa Majengo ya Hoteli hizo mbili yanarejea na kuanza kutoa huduma kama kawaida.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar ameipongeza Taasisi ya Bima ya Jubilee kwa uharaka wale iliyoonyesha ya Wataalamu wake kuanza tathmini ya hasara iliyotokea katika Hoteli ya Tui Blue Bahari ili walipe Bima katika kipindi kati ya Mwezi Mmoja na Miwili baada ya Ripoti husika.

Mheshimiwa Hemed Suleiman amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja kuifuatilia Taasisi ya Bima inayohudumia Hoteli ya Ocean Paradise kuanza Tathmini mara moja baada ya tukio hili ili kuwarejeshea Imani wateja wao.

Alisema uwepo wa Hoteli hizo mbili zinazolipa Kodi kwa zidi ya Bilioni Mbili kila Moja kwa Mwaka lazima uthaminiwe kwa vile unachangia mapato ya Taifa yanayoendelea kutumiwa katika huduma mbali mbali za Kijamii na Miundombinu tofauti ya Serikali.

Kwa upande wao wakielezea faraja walioipata ndani ya nyoyo zao kutokana na ujio wa Viongozi hao wa Serikali ikiwa ni njia ya kuwapa pole Meneja Mkuu wa Hoteli ya Tui Blue Bahari Bwana Reda Sweed na mwenzake wa Hoteli ya Ocean Paradise Bwana Burnt walisema ushirikiano wa pamoja uliofanikisha kukabiliana na janga hilo wataendelea kuukumbuka katika maisha yao ya baadae.

Bwana Reda na Bwana Burnt walimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba athari ya moto uliyoikumba Miradi yao ya Hoteli na kuacha doa kwao kutokana na hasara hiyo licha ya kwamba imewekewa Bima lakini pia itawaathiri Wanyakazi wao ambao wengi wao ni Wazawa wa hapa Nchini

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.