Habari za Punde

CCM Zanzibar : Maalim Seif ni msingi wa maendeleo ya sasa ya Zanzibar

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Ndugu Abdallah Mabodi akizungumza na Makamo M/kiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar Babu Juma Duni Haji katika Ofisi kuu za Chama cha ACT zilizopo Vuga Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Maneno hayo yamesemwa jioni ya leo tarehe 28/02/2021 na Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar  Ndugu Abdallah Mabodi, alipofika na ujumbe wa Sekretarieti ya Chama hicho kwa upande wa Zanzibar, kutoa mkono wa pole kwa Uongozi wa Chama cha ACT Wazalendo katika Ofisi kuu za Chama cha ACT zilizopo Vuga Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Mabodi amesema msiba wa Maalim Seif ni msiba wa Taifa zima na sio chama cha ACT Wazalendo pekee kwakusema,

"Ukweli utabaki wazi kwamba Maalim Seif ameyafanya mengi katika Nchi hii ikiwemo suala la kupigania Maendeleo ya Uchumi wa Nchi, jambo ambalo tunaona matunda yake leo".

Kwa upande wa Chama chake Mabodi amesema, CCM pia  itaendelea kumkumbuka Maalim Seif sana kwani mchango wake aliouacha katika Chama hicho enzi za uwanachama wake ni mkubwa sana.

Mabodi alimalizia kwa kusema kitendo cha Maalim Seif kutafuta Miafaka ya kisiasa ni dalili ya wazi kwamba alikuwa na dhamira ya kweli ya kuwaunganisha Wazanzibari sambamba na kuleta maendeleo katika Nchi, Mabodi amesema wao Chama cha Mapinduzi, Zanzibar wapo tayari kukaa meza moja na Chama cha ACT Wazalendo kujadili maendeleo ya Nchi na kwamba watahakikisha wajumbe wa baraza la Wawakilishi watayatekeleza na kuyasimamia.

Nae Naibu Katibu mkuu wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar Ndugu Nassor Ahmed Mazrui amesema kwa niaba ya Chama cha ACT wamepokea mkono wa pole na wamefarijika kuona kwamba mchango mkubwa wa maridhiano ulioachwa na Marehemu Maalim Seif umeanza kumea vyema.

Mazrui amewaeleza wageni hao kwamba Viongozi na Wanachama wa ACT Wazalendo wote hawana chembe ya unafiki katika suala la Maridhiano na wameahidi kuendelea kuyaenzi kama alivyoyaasisi Marehemu Maalim Seif.

Akitoa neno la shukran Makamo M/kiti wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar Babu Juma Duni Haji amesema n ikweli kwamba, kifo cha Maalim Seif kimewagusa wengi lakini ni wazi kabisa kwamba chemichemi ya umoja na mshikamano aliouanzisha kiongozi huyo imenza kutoa faida kwani hata waliombeza wameanza kuona dhamira yake ya kweli aliyokuwa nayo kwa Taifa la Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.