Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais aongoza Matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman akiyaongoza Matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar yaliyoanzia Majengo ya Mahakama Kuu vuga na kumalizia Viwanja vya Maisara kwa kupitia Michenzani na Kariakoo.
 Wababe wa Shirika la Bandari wakimenyana na Wakata Maji Timu ya KMKM Kwenye Mchezo wa kuvuta Kamba uliomtoa KMKM kifua mbele kwa kushinda pambano hilo kwenye matembezi ya siku ya Sheria Zanzibar.
Timu ya Mahkama Watuka Kamba wakionyesha kushindwa nguvu baada ya kutolewa na Wababe wa Aman hawapo pichani kwenye pambano la siku ya Sheria Zanzibar hapo Maisara Suleiman.
Jaji Mkuu wa Zanzibar Mheshimiwa, Omar Othman Makungu akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman kwenye kilele cha matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar hapo Maisara.
Baadhi ya Wanamichezo walioshiriki matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar wakifuatilia matukio mbali mbali yaliyofanyika katika Viwanja vya Michezo vya Maisara Suleiman
Wababe wa KMKM wakifanya vitu vyao katika shindano ya kuvuta kamba vilivyopelekea kuibuka mshindi dhidi ya Timu ya Shirika la Bandari Zanzibar.
Wavuta Kamba wa Amani wakitunisha misuli iliyopelekea kuwalaza chali Timu ya Mahkama Kuu kwenye Mchezio wa Kuvuta Kamba ulioshuhudiwa na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman.

 Wavuta Kamba Wanawake wa Timu ya Bandari wakionyesha kuelemewa kwenye pambano lao lililowaibua Washindi Wapinzani wao Timu Maafufu katika Mazoezi ya Viungo ya Kitambi Noma.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman ametoa ushauri wa kuweka siku Maalum ya uendeshaji wa Baskeli Nchini ili ifikie wakati kila Mtu nafsi yake imlazimishe kufanya mazoezi yatakayoisaidia Jamii kuendelea kuwa na Afya bora.

Alisema licha ya uwepo wa vikundi kadhaa vya mazoezi katika maeneo mbali mbali Nchini lakini bado inasikitiosha kuona asilimia kubwa ya Wananchi haina Utamaduni wa kufanya mazoezi jambo ambalo umefika wakati kwa hadhi ya mazoezi lazima irejee kama zamani.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alieleza hayo kwenye Matembezi ya Siku ya Sheria Zanzibar yaliyoanzia Mahkama Kuu na kushirikisha Vikundi mbali mbali vya mazoezi na kupitia Benbela, Mkunazini kuekea Kariako hadi Kilimani na kumalizia katika Viwanja vya Maisara Suleiman Mjini Zanzibar.

Alisema Uongozi wa Manispaa pamoja na zile Halmashauri uzingatie kutenga  siku Maalum katika kushajiisha Wananchi wao kutembea kwa lengo la kurejesha Utamaduni wa asili wa Watu kupenda kutembea ambao kwa sasa uko hatarini kupotea kutokana na kuongezeka kwa vyombo vya Moto.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba zingatio hilo vizuri likenda sambamba na Manispaa na Halmashauri hizo kutunga sheria ndogo ndogo zitakazolinda maeneo kwa uwepo wa njia za watembeao kwa miguu bila ya kuingiliwa na shughuli nyengine.

“Si jambo baya  kwa mamlaka zetu za Miji kutunga sheria ndogo ndogo zitakazoshajiisha Wananchi kutumia baskeli pamoja na kuwalinda wapanda baskeli kiusalama". Alisema Mheshimiwa Hemed.

Alifahamisha kwamba Taifa likiendelea kubakia kuwa na Watu wenye Afya bora watakaokuwa na uwezo wa kuongeza ufanisi katika Kazi, Bajeti ya Serikali kupitia Wizara inayosimamia Sekta ya Afya ya kuagiza Dawa nje ya Nchi inayogharimu fedha nyingi za kigeni itapunguwa.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwakumbusha Watendaji wa Taasisi za Umma wakiwemo wale wa Mahakama wanaotumia muda mwingi kukaa Maofisini kutenga muda Maalum kulingana na mazingira yao ya Kazi kufanya Mazoezi kwa ajili ya kulinda Afya zao.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alipendekeza Watendaji hao kuunda vikundi vya michezo ndani ya Mahkama vitakavyotoa fursa kwa kil Mtendaji ashiriki hata kama mchezo mmoja ili kuimarisha Afya zao pamoja na majukumu waliyonayo.

Alisema mfumo huo utasaidia kuleta hamasa zaidi kwenye michezo na kwenda bega kwa bega na dhamira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliyojikubalisha kuongeza ushirikiano katika kuimarisha michezo kwenye Taasisi zake  na kuepuka maradhi ya mara kwa mara.

Mapema Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu alisema masafa  ya matembezi ya Mwaka huu yamezingatiwa kupunguzwa ili kutoa fursa ya washiriki wote kumaliza Matembezi hayo yaliyokadiriwa kuwa na umbali wa Kilomita Tatu.

Mheshimiw Omar Othman Makungu alisema Uongozi wa Mahkama Zanzibar umefikiria Wanasheria kuwa na utaratibu wa kuanza kufanya mazoezi kila Mwezi kwa vile muda mwingi wanakaa maofisini pamoja na wanafikiri sana.

Jaji Mkuu wa Zanzibar ameushukuru na kuupongeza Uongozi wa Benki ya NMB na ile ya CRDB kwa uamuzi wao wa kuunga Mkono Sekta hiyo ya Sheria hasa kwenye maandalizi ya Matembezi hayo ya siku ya Sheria Zanzibar.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman pamoja na Viongozi wengine walijumuika pamoja na Wanamichezo mbali mbali  katika mazoezi ya Viungo ili kukamilisha matembezi hayo hapo katika Viwanja vya Maisara.

Mazoezi hayo yalifutiwa na mashindano ya Mchezo wa kuvuta kamba yaliyoshirikisha Wachezaji wa Timu za Bandari iliyomenyana na Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo Zanzibar {KMKM}wakati Mahkama ikamenyana na Amani kwa Wanaume.

Washinidi ni Kikosi cha KMKM kiliibuka kideea dhidi ya Bandari na Amani wakapeperusha bendera ya ushindi dhidi ya Kiko cha Mahkama.

Kwa upande wa Wanawake shindano liliwakutanisha Mahkama dhidi ya Kitambi Noma ambapo mshindi akatangazwa Kitambi Noma mashindano yaliyoleta msisimkoa Viwanjani hapo.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.