Habari za Punde

RUWASA WIayani Muheza katika kutimiza malengo yake, vijiji 72 kupelekewa Maji

Na Hamida Kamchalla.

VIJIJI vipatavyo 72 wilayani Muheza mkoani Tanga havijafikiwa na huduma ya maji na kuwafanya wakazi takribani asilimia 31 kukosa huduma hiyo kabisa huku wakitegemea maji kutoka kwenye visima vifupi na kwenye madimbwi.

Meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) wilayani humo Injinia Cleophate Maharangata  aliyasema hayo jana kwenye kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Muheza na kueleza kwamba kwa kuwa wapo kwa ajili ya kutekeleza malengo makuu matatu, RUWASA watahakikisha malengo hayo yanatimia na kila Mtanzania atapata na kutumia maji safi na salama.

Maharangata alifafanua lengo kuu la RUWASA wanayotekeleza kuwa ni kuhakikisha kwamba miradi ya maji vijijini inakuwa endelevu na jamii inapata maji wakati wote, lakini pia RUWASA ina malengo matatu katika utekelezaji wake ambapo moja wapo ni kutekeleza ilani ya Ccm ya mwaka 2020/ 2025.

"Muheshimiwa mwenyekiti lengo la pili ni kuhakikisha dira ya maendeleo ya Taifa inafikiwa ambapo inasema mpaka kufikia 2025 huduma ya maji vijijini iwe asilimia 95, lakini pia RUWASA imepanga kuhakikisha malengo ya milenia yanafikiwa ambapo kufikia mwaka 2030 kila mtu awe na uhakika wa kupata maji safi na salama" alieleza.

"Wakala wa maji na usafi wa mazingira RUWASA imeanzishwa kwa mujibu wa kifungu namba 42 cha sheria ya huduma za maji na usafi wa mazingira namba 5 cha mwaka 2009, ikiwa na jukumu la kupanga, kusanifu, kujenga na kusimamia uendeshaji wa shughuli za maji na usafi wa mazingira vijijini" alibainisha.

Aidha alieleza kwamba RUWASA katika kutimiza malengo yake imejipanga kutekeleza katika maeneo matatu ambayo ni kuhakikisha kujenga miradi katika maeneo ambayo hayana huduma ya maji kabisa, kuongeza huduma ya upatikanaji wa maji kwenye maeneo ambayo kuna miradi ambapo katika ongezeko la watu wakajikuta maji hayawatoshi pamoja na kusimamia kutoa huduma ya maji kwenye miradi iliyopo na ambayo inaendelea kujengwa.

"Ifahamike kwamba zoezi la kujenga miradi ni la muda tu, hivi sasa tumejipanga kujenga miradi lakini vyanzo vitakapopata maji basi suala la kujenga miradi litakoma, lakini kazi yetu kubwa ni kuhakikisha sasa utoaji wa huduma ya maji safi na salama na yenye kuwatosheleza inaendelea" alifafanua.

"Katika kuhakikisha tunayakamilisha hayo tumejipanga kufanya mambo matatu, kwanza ni kutafuta vyanzo, sisi RUWASA hatutaweza kujenga mradi kwenye eneo ambalo hakuna chanzo cha maji, na kama eneo lina chanzo cha maji basi tunasanifu mradi na baadae tunafanya ujenzi" aliongeza.

Hata hivyo M alibainisha kutengwa kwa bajeti ya RUWASA kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022 ambapo zaidi ya shilingi bilioni 1.17 zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi wikayani humo ambapo miradi 13 itatekelezwa kupitia mfuko wa maji.

Vilevile Maharangata aliendelea kufafanua kwamba kwa sasa RUWASA ina vyanzo vitatu vya fedha ambavyo ni mfuko wa maji, fedha ambazo zinakusanywa kutokea kwenye mafuta ya petrol na diezel ambayo kila lita moja inachukuliwa shilingi hamsini na kuingizwa kwenye mfuko huo ambao uko chini ya Wizara ya Maji.

"Hizo ndio fedha tunazopata kwenye mfuko wetu, lakini pia tuna chanzo kutoka serikali kuu moja kwa moja, lakini fedha nyingine tunapata kutoka kwa wadau wetu wa maendeleo, kuna DFID wenyewe wanatusaidia programu moja inaitwa 'malipo kwa matokeo' hii programu yetu naomba madiwani mtambue lengo lake lilikuwa ni kuhakikisha wanafanya ukarabati wa miradi ambayo ilikuwepo" alisema.

"Kwa maana ya kwamba miradi hiyo ilijengwa halafu ikawa haitoi huduma, sasa badala ya kuendelea mbele na kujenga miradi tu huku mingine ikiwa imekwisha haribika, tukaona sasa ipo haja ya kuifufua, ndiomaana tunafanya hivyo kwa miradi yote ambayo ipo na haitoi huduma" aliongeza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.