Habari za Punde

Serikali kurudisha nidhamu kwa viongozi na watumishi wa umma

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla akizungumza na waumini wa Dini ya Kiislamu mara baada ya sala ya Ijumaa katika Masjid As’ silm uliopo Bububu Kihinani Wilaya ya Magharibi “A” Unguja.
Mkurugenzi wa Jumuiya ya Al - Fataah Ustadhi Rashid Salum akitoa shukrani zake kwa Mhe. Makamu wa Pili wa Rais kwa niaba ya waumini wa Masjid Al-Silm huku akielezea faraja walionayo wananchi juu ya serikali ya awamu ya nane katika kuimarisha ustawi wa watu wake
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdalla akisalimiana na Watoto wanaopata mafunzo yao ya Madrasa katika Masjid Al’ Silm Bububu Kihinani.

 Baadhi ya Watoto wanaopata mafunzo yao ya Madrasa katika Masjid Al’ Silm wakimsikiliza Mheshimiwa Hemed kabla ya kuondoka katika viunga vya msikiti huo.

Picha na – OMPR – ZNZ.

Na OMPR

Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya Awamu ya Nane imekusudia kurejesha nidhamu kwa viongozi na watumishi, wa Umma itakayosaidia kuweka heshima katika matumizi sahihi ya fedha ya serikali.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliyasema hayo wakati akitoa salamu kwa waumini wa dini ya Uislamu baada ya kukamilika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa, katika Masjid As Silmi Bububu Kihinani.

Alisema siku mia moja za uongozi wa Rais Dr. Hussein Ali Mwinyi zimeonyesha muelekeo wa kurejesha heshima na nidhamu hiyo Serikalini ambayo ilipungua kwa muda mrefu.

Alisema mchakato wa Serikali Kuu umekusudia kufikiria kuanzisha Mahakama ya wala Rushwa ili kutekeleza kwa vitendo Azma yake ya kukomesha suala la uhujumu wa uchumi kwa baadhi ya Viongozi na watumishi wa Taasisi za Serikali.

Mheshimiwa Hemed Suleiman alibainisha kwamba Dr. mwinyi aliomba ridhaa kwa Wazanzibari ili kuwatumikia na kuweza kuwaletea maendeleo kupitia fursa mbali mbali zilizopo nchini, hasa suala zima la ajira kwa vijana.

Alitolea mfano mikataba miwili iliyosainiwa hivi karibuni ya ujenzi wa bandari mbili, zitakazoweza kusaidia kutoa fursa za ajira kwa vijana, hivyo aliwaomba waumini hao kuendelea kumuombea Dua katika uongozi wake, ili malengo yaliyokusudiwa yaweze kutimia.

Aidha Mheshimiwa Hemed aliwaasa wafanyabisahra nchini kulipa kodi kwa utaratibu, na kueleza kuwa fedha inayopatikana katika ukusanyaji wa kodi hizo, zinarudi kwa wananchi katika maeneo mbali mbali ya maendeleo.

Akigusia suala  la kupinga udhalilishaji Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaasa wazazi na walezi kila mmoja wapo kuanza kulipinga suala hilo kwa kusimamia familia zao, na kuongeza kuwa Taifa linahitaji vijana wachapakazi ambao wamo katika familia hizo.

Mheshimiwa Hemed alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na Wananchi ambao kuripoti kwao pale wanaposhuhudia changamoto zilizomo ndani ya maeneo yao waelewe kwamba wameshaisaidia Serikali.

Mapema akitoa khutba ya Sala ya Ijumaa ustadh Khamis Shaaban, alisema uislamu umehimiza suala zima la  kuombeana Dua kwa lengo la kumtaka Mwenyezi Mungu kuzidisha Baraka zake, hivyo amewataka waumini kuwaombe Dua Viongozi wa Awamu ya nane kuanzia Rais pamoja na wasaidizi wake, ili dhamira yao ya kuleta maendeleo ipatikane.

Sheikh Khamis aliwatanabahisha Waumini wa sasa kuendelea kufuata matendo yaliyokuwa yakifanywa na Masahaba wa Kiongozi wa Waumini hao wa Dini ya Kiislamu ili kuleta utulivu, raha na furaha miongoni mwao katika dhana nzima ya kupata radhi za dini na kufuata sharia za Dini.

Akisalimiana na watoto wa Mtaa huo wa kihinani walioshiriki ibada hiyo ya sala ya Ijumaa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed aliwanasihi waendelee kupenda Elimu zote mbili zitakazokidhi mahitaji yao.

Mheshimiwa Hemed alisema Taifa hili linawategemea Zaidi Vijana waliopata misingi sahihi ya Taaluma ambao miongoni mwao ndio  wanaobeba dhima ya kuwaongoza pamoja na kuwahudumia wenzao.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.