Habari za Punde

Watumishi wa Serikali Mkoani Tanga Waaswa Kutowadharau Wazee Wanapofuata Huduma.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martin Shigela akizindua Baraza la Wazee la Mkoa wa Tanga. 

Na Hamida Kamchalla, TANGA.

WATUMISHI wa ngazi zote mkoani Tanga wameaswa kuacha kudharau na kuwanyanyapaa wazee pindi wanapofuata huduma kwenye ofisi zao badala yake kuwanyenyekea na kuwapa kipaumbele ili kupata Baraka na kuondokana na balaa.

Hayo yalisemwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe.Martin Shigela wakati akizindua baraza la wazee la mkoa huo ambapo aliwataka watumishi popote watakapokuwa kuwaheshimu na kuwanyenyekea wazee kwani ndiyo hazina pekee inayoleta Baraka ndani ya Taifa.

Shigela alibainisha kwamba serikali ya awamu ya tano ina dhamira ya dhati ya kuwathamini na kuwaenzi wazee na ndiyo sababu mojawapo ya kuamua kuunda mabaraza ya wazee nchini.

“Niwaase watumishi wa serikali, muwape heshima wazee maana ipo zana ya kuwazarau na kuwaona ni wasumbufu, tukiwakuta wazee kwenye ofisi zetu wanataka kutuona, tuwape kipaumbele kuwasikiliza, tukifanya hivi tutaendelea kupata amani na baraka kwenye Taifa letu” alisema Shigela.

Aidha Shigela aliwataka wanaohusika na usajili wa mabaraza hayo kufanya jitihada za kuwafikia wazee wote hata walioko vijijini ili kuwawezesha kupata huduma stahiki na msingi hasa wale wanaotakiwa kupata pensheni zao.

“Mamlaka zinazohusika na usajili zihakikishe zinapata taarifa sahihi za wazee wote hasa kule vijijini, wapo wazee wengi ambao hawajiwezi kutokana na matatizo ya ugonjwa au kukosa misaada ya kufikishwa mahala husika” alieleza.

“Ndani ya mkoa wetu tumeambiwa takribani asilimia 59 ya wazee wamesajiliwa, sasa niagize kwa wahusika kwenda kumalizia kuwasajili hao waliobaki ambao ni sawa na asilimia 49 ili wapate vitabulisho” aliongeza Shigela.

Hata hivyo aliwaonya TASAF kuacha tabia ya kuwaandikisha watu ambao hawahusiki na misaada inayotolewa kwenye mfuko huo kwani ni kinyume cha utaratibu na endapo itabainika hatua stahiki zitafuatwa.

“Kuhusu pesa ya TASAF, tunajua wapo wazee waliosajiliwa kwa ajili ya kupatiwa misaada lakini wengi wao waliosajiliwa ni ambao siyo wazee na hawahitajiki kupata misaada hiyo, ikibainika mtu amefanya hivyo tutamshuhulikia.

Naye mwenyekiti wa baraza hilo Hashim Shekilindi alimshukuru mkuu wa mkoa kwa ushirikiano wake hadi kuwezesha uzinduzi wa baraza hilo mkoani hapa ikiwa ni pamoja na kutoa ushirikiano kwa viongozi wa ngazi zote.

Aidha Shekilindi aliahidi kutoa ushirikano kwa mkoa katika kuhakikisha maendeleo ya wazee yanapatikana na kuimarika na kutoa shukurani zake kwa wazee wenzake kwa kumpadhamana ya kumchagua kuwa mwenyekiti wa baraza hilo.

“Kwanza nikupongeze wewe mkuu wa mkoa na kukushukuru kwa kuja kutuzindulia baraza letu, nikiwa mwenyekiti wa baraza hili nitahakikisha nashirikiana na mkoa ili kuleta maendeleo ya wazee ndani ya mkoa wetu” alisema Shekilindi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.