Habari za Punde

Makamu wa Kwanza wa Rais : Siasa zimetuchelewesha sana kuyafikia maendeleo ya Nchi yetu ya Zanzibar


Na OMKR

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mh. Othman Masoud Othman  ameyasema hayo leo tarehe 08/03/2021 alipokuwa anazungumza na Watendaji wa Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Mh. Othman amezungumza na watendaji hao ikiwa ni mara ya kwanza baada ya kuwasili ofisini hapo rasmi kuanza majukumu yake ya kiofisi katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais  iliyopo Migombani Mkoa wa Mjini Magharib Unguja.

Mh. Othmana alipokelewa na watendaji wa ofisi hio wakiongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh. Sada Mkuya.

Baada ya kutembezwa kwa lengo la kutambulishwa watendaji na vitengo vya Ofisi yake Mh. Othman pia alipata fursa ya kuzungumza na watendaji hao.

Akifungua kikao hicho Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Mh. Sada Mkuya amesema Binafsi ana matumaini makubwa na Mh. Othmani juu ya utendaji wake kazi kwamba hatoiangusha Serikali na hatowaangusha Wazanzibari.

Mh.Sada amewataka Watendaji wa Ofisi hio kuhakikisha wana wajibika vyema katika majukumu yao,  na pia amewataka viongozi wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza   kuhakikisha wanawawajibisha watendaji wasiofata misingi ya utumishi sambamba na kuwapongeza wale wanaofanya vyema.

Makamu wa Kwanza wa Rais  alianza mazungumzo yake kwakusema kwamba  Mh. Rais wa Zanzibar Dr. Mwinyi ana matumaini makubwa sana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais hivyo tunatakiwa tuwe na ufanisi ili tusimuangushe.

Katika kusisitiza hilo Mh. Othman amesema  baadhi ya Watendaji katika Ofisi ya Makamu sio wageni kwake anawafahamu na utendaji wao anaujua hivyo anatarajia utendaji mwema katika kuwatumikia Wananchi.

Makamu wa Kwanza wa Rais amesisitiza uwajibikaji kwa kusema, "Kikubwa zaidi ni Uwajibikaji kwa watendaji na kujua majukumu yao kwani taasisi ikijua majukumu na ufanisi utapatikana"

Mh.Othman amewataka viongozi wa Idara katika Ofisi ya Makamu wa Kwanza kuhakikisha wanazipitia upya Sheria zilizopo ili ziweze kuwa sheria rafiki na zenye kumsaidia Mwananchi wa chini.

Mh. Othman amewataka pia Watendaji hao kuacha kufanya kazi kimazoea na badala yake wawajibike kwamujibu wa mahitaji ya Serikali na Jamii kwa ujumla.

"Idara zetu ziwe rafiki kwa jamii na zisiwe sababu ya kukwamisha maendeleo"  amesema Mh.Othman.

Kutokana na umuhimu na uhitaji wa huduma kwa Wananchi kutoka katika Idara zilizopo chini ya Ofisi ya Mamaku wa Kwanza, Mh. Othman amesema ipo haja mahususi kuwepo kwa huduma za kimtandao (Digital platform) ambazo zitawawezesha Wananchi wenye uhitaji kutokusumbuka na badala yake kupata huduma hata wakiwa maeneo ya mbali na ofisi.

Makamu wa Kwanza wa Rais pia amewataka Viongozi wa Idara ya Mazingira kuhakikisha wanakuwa Washauri wa Jamii juu ya Majanga yanayoweza kuepukika, ili kuweza kujiepusha mapema, na badala yake wasisubirie tatizo litokee ndio wajitokeze kutoa tahadhari.

Mh. Othman amewataka Watendaji kuhakikisha yeyote mwenye mawazo mazuri ya kujenga ayafikishe katika ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais kwaajili ya kufanyiwa kazi.

Mwisho kabisa amewaeleza watendaji wake kwamba,  " Siasa zimetuchelewesha sana kuyafikia maendeleo ya Nchi yetu ya Zanzibar, hivyo sasa ni muda wakuacha siasa nyuma ili tujenge Nchi yetu kwa pamoja.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.