Habari za Punde

Mama Mariam Mwinyi azindua rasmi Kampeni ya AMKA MWANANGU Soma kwa Bidii


Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi akizungumza na kuzindua Mradi wa Amka Mwanangu Soma kwa Bidii wa Jumuiya ya Rafiki wa Wanawake na Watoto Zanzibar, hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip Malindi Jijini Zanzibar.

MKE wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi ameitaka Jumuiya ya “Rafiki wa Wanawake na Watoto Zanzibar” (RAWWAZA) kupitia kampeni yake ya “AMKA MWANANGU” kuendelea kushirikiana na Serikali katika mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa watoto na unyanyasaji wa kijinsia.

Mama Mariam Mwinyi aliyasema hayo wakati akiizindua rasmi Kampeni ya “AMKA MWANANGU” iliyoanzishwa na Jumuiya ya “Rafiki wa Wanawake na Watoto Zanzibar” (RAWWAZA), hafla iliyofanyika huko katika ukumbi wa Hoteli ya “Golden Tulip”, Malindi, Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake, Mama Mariam Mwinyi alieleza haja kwa Jumuiya hiyo kuwapa elimu watoto kuhusu njia bora ya kujikinga na vitendo hivyo sambamba na kuwafundisha taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa katika kutoa taarifa za matukio ya udhalilishaji na upatikanaji wa ushahidi.

Mama Mariam Mwinyi aleleza kwamba juhudi za Jumuiya hiyo zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa malengo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ya kuimarisha haki, usawa pamoja na kuongeza fursa za kiuchumi, kijamii na kisiasa kwa wanawake wa Zanzibar na Tanzania kwa jumla.

Aliwasihi wazazi kuwa wananafasi kubwa sana katika kuhakikisha wanawalinda watoto na wanazungumza nao vizuri na kuacha kutopokea zawadi ama rushwa baada ya mtoto kuathirika kwani vitendo hivyo vinawaharibu watoto kisaikolojia.

Alieleza kwamba kutokana na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Serikali ya Awamu ya Nane anaimani kwamba vitendo hivyo vitakuwa historia  huku akisisitiza mashirikiano ya pamoja.

Akitoa nasaha zake kwa viongozi na wanachama wa Jumuiya hiyo, Mama Mariam Mwinyi aliwataka kuhakikisha kwamba wanaongeza nguvu ili kuweza kutekeleza kwa ufanisi dira na dhamira ya Jumuiya yao pamoja na malengo ya KAMPENI YA “amka mwanangu” katika kipindi chote cha mwaka mmoja cha utekelezaji wake.

Aliwataka kuongeza ari na hamasa katika kuimarisha na kutetea maslahi ya wanawake na watoto pamoja na kuwa wabunifu kwa kuweza kuibua miradi mbali mbali yenye tija ili hatimae isaidie kuongeza kipato cha wananchi.

Aidha, Mama Mariam Mwinyi aliwataka kuendelea kushirikiana na Serikali, Mashirika na asasi za kiraia za ndani na nje ya nchi katika kutafuta njia na nyenzo zitakazosaidia kuviwezesha kiuchumi vikundi mbali mbali vya ujasiriamali vinavyoendelea kuanzishwa hapa nchini.

Alieleza furaha yake kwa kuzinduliwa Kampeni ya “AMKA MWANANGU” ambayo inakwenda sambamba na maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani (Machi 08).

Mama Mariam Mwinyi alipongeza malengo pamoja na shughuli mbali mbali zinazofanywa na Jumuiya ya RAWWAZA katika kuimarisha maendeleo ya wanawake na watoto katika sehemu mbali mbali za Unguja na Pemba, tangu kuanzishwa kwake mwaka 2016.

“Nimevutiwa sana na dhamira na malengo ya RAWWAZA kuimarisha elimu na malezi bora kwa watoto wetu kupitia kampeni hii ya “AMKA MWANANGU”, ni wazi kwamba kampeni hii inatukumbusha na inatuhimiza utekelezaji wa jukumu letu la msingi la kuhakikisha tunawapa malezi na elimu bora watoto wetu,tuitekeleze kwa kuzingatia maneno yasemayo mwana umleavyo ndivyo akuavyo”.alisema Mama Mariam Mwinyi.

Pamoja na hayo, mama Mariam Mwinyi alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuendelea kuteua wanawake katika nafasi mbali mbali za uongozi.

Alieleza kuwa kuna uwakilishi mzuri katika Baraza la Mawaziri, baraza la Wawakilishi, makatibu Wakuu, Wakuu wa Mikoa na Wilaya na kuahidi kufikisha salamu kwa Rais kwamba bado wanawake wanataka nafasi nyengine zaidi, kwani uwezo na uzoefu wanao.

Nae Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Tauhida Cassian Gallos alieleza mafanikio makubwa yaliopatikana katika Jumuiya hiyo ambayo yanatokana na malezi mazuri kutoka kwa walezi wa Jumuiya hiyo pamoja na mapenzi na mashirikiano ya Wajumbe wote wa Jumuiya.

Mwenyekiti huyo alitumia fursa hiyo kueleza shughuli mbali mbali zinazofanywa na Jumuiya hiyo zikiwemo zile za kijamii hasa kwa upande wa wanawake na watoto.

Katibu wa Jumuiya hiyo, Tatu Hussein Abdalla akisoma risala ya Jumuiya hiyo alisema kwamba Jumuiya hiyo imesajiliwa mwaka 2026 chini ya kifungu namba 6 ya mwaka 1995 na kupewa namba ya usajili ambapo makao makuu yake yapo Dole Mkoa wa Mjini Magharibi Wilaya ya Magharibi “A”, Unguja na ina takriban wanachama 49.

Alieleza kwamba kampeni ya “AMKA MWANANGU” matarajio yake makubwa ni kuleta tija, hamasa na kuweza kujitambua kwa ujumla kupitia walengwa ambapo itafanyika kwa Unguja na Pemba kwa nyakati tofauti katika kipindi cha mwaka mmoja.

Pia, Jumuiya hiyo ilitoa taarifa ya shughuli zilizopangwa na fedha zitakazotumika katika kampeni hiyo ya “AMKA MWANANGU”,ambapo inakisiwa kutumia jumla ya TZS. Milioni 133,792,000.

Alieleza kwamba ili kampeni hiyo iweze kufikia pale walipokusudia wamedhamiria kukutana  na wanafunzi kwa njia ya kupitia mashuleni kazi ambayo itafanyika kwa kila Wilaya, wamekusudia kuwaelemisha wazazi kupitia njia ya vipindi kwenye vyombo vya habari pamoja na kukutana na walimu kwa njia ya makongamano kwa mikoa yote ya Zanzibar.

Katika hafla hiyo pia, mashuhuda waliokumbwa na kadhia mbali mbali ikiwemo udhalilishaji wa kijinsia pamoja na matumizi ya dawa za kulevya walipata fusra ya kueleza maswahiba hayo yaliyowakumba kwa nyakati tofauti.

Sambamba na hayo Jumuiya hiyo pia ilitoa zawadi kwa Mama Mariam Mwinyi pamoja na zawadi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Mwinyi huku wakimpongeza Mgeni rasmi huyo kwa kuungana na Jumuiya hiyo katika hafla hiyo muhimu.

Hafla hiyo ilikwenda sambamba na burudani ya nyimbo za taarab kutoka kikundi cha “Zanzibar One Modern Taarab”chini ya uongozi wake Abdulla Ali (Du) pamoja na nyimbo maalum zilizoimbwa na vijana kuhusiana na maendeleo ya Jumuiya hiyo ambayo imeanzishwa kwa dhamira ya kukuza na kuimarisha uwezo wa wanawake na watoto katika masuala ya mipango, utetezi na mapambano dhidi ya unyanyasaji, ukatili, ubakaji, mimba za utotoni na mengineyo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.