Habari za Punde

Anglogold Ashanti, Tanzania Zakubaliana Kuendeleza Ushirikiano.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akizungumza na Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Bw. Sicelo Ntuli wakati walipokutana kwa mazungumzo leo jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) akiongoza kikao chake na Kampuni ya Madini ya Anglogold Ashanti ya Afrika Kusini kilichofanyika leo jijini Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar

Kampuni ya Madini ya Anglogold Ashanti ya Afrika Kusini imeahidi kuendeleza ushirikiano na Serikali ya Tanzania katika sekta ya madini na kuhakikisha kuwa sekta hiyo inakuwa mstari wa mbele kuchangia uchumi.

Ahadi hiyo imetolewa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti – Afrika, Bw. Sicelo Ntuli wakati alipokutana kwa mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula (Mb) leo Jijini Dar es Salaam.

Akiongea mara baada ya mazungumzo hayo Balozi Mulamula amesema kuwa, Anglogold Ashanti ni wadau wakubwa katika sekta ya madini na wameonesha utayari wao wa kushirikiana kwa karibu na Serikali katika kukuza na kuendeleza sekta ya madini. 

“Leo hii nimekutana na uongozi wa Kampuni ya Madini ya Angogold Ashanti na tumejadili pamoja na mambo mengine, utayari wa Kampuni hiyo kushirikiana na Serikali katika kukuza sekta ya madini hapa nchini,” Amesema Balozi Mulamula

Balozi Mulamula ameongeza kuwa kitendo cha kukutana na wadau wa madini kama Anglogold Ashanti na kujadiliana nao masuala mbalimbali ya ushirikiano wa kukuza sekta ya madini ni sehemu ya utekelezaji wa sera ya Diplomasia ya Uchumi.

Kwa Upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Anglogold Ashanti Bw. Ntuli amesema kuwa uongozi wa Anglogold umefarijika kukutana na Mhe. Waziri wa Mambo ya Nje na kuweza kujadiliana nae mambo mbalimbali ikiwemo suala la kukuza ushirikiano baina ya Kampuni hiyo na Serikali ya Tanzania.

“Sisi kama Anglogold tumefarijika kuona Serikali ya Tanzania ipo tayari kuendeleza ushirikiano na Sisi…….tunaahidi kuendeleza ushirikiano huu kwa maslahi mapana ya pande zote mbili,” Amesema Bw. Ntuli

Aprili 16, 2021 Kampuni ya Anglogold Ashanti iliingia ubia na Kampuni ya BG Umoja ya nchini Tanzania kwa ajili ya kuchimba madini katika miradi ya Nyankanga na Geita Hill. Anglogold ni Kampuni mama ya Geita Gold Mine (GGML) imeipatia BG Umoja mkataba wenye thamani ya Dola za Marekani Milioni 186 kwa miaka miwili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.