Habari za Punde

SMZ yatangaza bei elekezi za vyakula mwezi wa Ramadhani

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Mhe.Omar Said Shabaan akizungmza na waandish wa Habari juu ya Bei elekezi ya vyakula ikwemo Mchele, Unga wa Ngano na Sukari kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani hapo Afisini kwake Malindi  Zanzibar
  

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imetangaza bei elekezi kwa ajili ya bidhaa za vyakula vinavyotumiwa wakati wa mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unaoanza siku chache zijazo.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Unguja jana, Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Omar Said Shaaban, alisema lengo la uamuzi huo ni kuwawezesha wananchi – hasa wale wa kipato cha chini, kutimiza ibada hiyo ya kufunga kwa wepesi na gharama nafuu.

Kwa mujibu wa maelekezo hayo ya SMZ, bei elekezi ya mchele wa mapembe itatakiwa isizidi shilingi 1,600 kwa kilo, sukari isizidi shilingi 2,000 kwa kilo na unga wa ngano nao umepangwa usizidi kiasi cha shilingi 1,600 kwa kilo.

“Bei hizi zitabaki hivyo kwenye masoko mpaka hapo zitakapofanyiwa mapitio na kutangazwa vyenginevyo na serikali kama inavyoelezwa kwa mujibu wa sheria. Tunatoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi wote wazingatie bei elekezi ambayo serikali imetangaza. 

“Mimi binafsi nitazungukia katika maeneo mbalimbali ya biashara kujiridhisha kama kweli wafanyabiashara wanafuata maelekezo haya ya serikali na ijulikane kwamba ziko adhabu kali kwa wale watakaokiuka bei hizi elekezi,” alisema waziri huyo ambaye ni mmoja wa mawaziri wawili kutoka Chama cha ACT Wazalendo walio katika Baraza la Mawaziri la Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK).

Omar ambaye kitaaluma ni mwanasheria, alisema ametangaza bei hiyo elekezi kutokana na mamlaka aliyopewa kisheria chini ya kifungu cha 61 (1) cha Sheria ya Ushindani Halali na Kumlinda Mlaji Namba 5 ya mwaka 2018. Alisema bei hizo elekezi zimepatikana baada ya mchakato uliohusisha serikali na wafanyabiashara waagizaji na wauzaji wa vyakula visiwani humo pamoja na ukaguzi wa hali ya chakula visiwani humo uliyoonyesha kuna akiba ya kutosha ya chakula.

Ili kuhakikisha kwamba bei hiyo elekezi inafuatwa, Waziri Shaaban alisema wizara yake imeunda Kikosi Kazi kinachoshirikisha Tume ya Ushindani Halali wa Biashara, Idara ya Biashara na Masoko na Halmashauri za Wilaya kufuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuchukua hatua mwafaka kwa watakaokwenda kinyume cha bei elekezi.

“Kumekuwa na ada ya muda mrefu ya baadhi ya wafanyabiashara wasio na huruma wenye tamaa kutumia fursa ya mwezi mtukufu kupandisha bei kiholela hasa kwa bidhaa muhimu za chakula kama vile mchele, sukari na unga wa ngano.

“Tabia kama hizi za kutaka kuchuma faida kupitia mgongo wa wanaofunga hazikubaliki na mara nyingi husababisha wananchi walio wengi ambao hali zao ni duni kutekeleza ibada yao ya Funga katika mazingira magumu,” alisisitiza waziri huyo.

Waziri huyo alitumia nafasi hiyo, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, kuwatakia Waislamu wote nchini Mfungo mwema wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Imetolewa na Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar
11/04/2021

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.