Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Awahutubia Wafanyakazi Siki ya Wafanyakazi Duniani Katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Husseiun Ali Mwinyi akihutubia Wafanyakazi katika Maadhimisho ya Siki ya Wafanyakazi Duniani Mei Mosi katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ina azma ya kutekeleza utaratibu wa kuimarisha viwango vya mishahara kwa wafanyakazi wa ‘Kada ya kati’, pale hali ya uchumi utakapozidi kuimarika.

Dk. Mwinyi amesema hayo leo katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, yaliofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni Jijijini Zanzibar.

Amesema wafanyakazi wa eneo hilo ni muhimu katika maendeleo ya Taifa kwa vile ndilo lenye wataalamu, ikiwemo walimu, wafanyakazi wa afya na wengineo ambapo hivi sasa wamekuwa wakilipwa mishahara duni.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, awamu ya saba ilikuwa na nia njema ya kuimarisha  mishahara kwa wafanyakazi wa ngazi zote kwa awamu tatu, hata hivyo hatua hiyo ilishindwa kukamilika kutokana na kuibuka kwa ugonjwa Corona na kuathiri ukusanyaji wa mapato na hivyo hivyo utaratibu huo kuishia kwa kuimarisha viwango vya mishahara ya kima cha chini hadi kufikia shilingi 300,000/-

Aidha, alisema Serikali inalenga kuangalia upya utaratibu wa malipo ya kiunua mgongo kwa wafanya kazi waliostaafu (maarufu kwa jina la vikokotoo) ikiwa na lengo la kuwanufaisha wafanyakazi, wakati huu ambapo wafanyakazi na wastaafu wengi wanalalamikia utaratibu huo.

Akigusia upande wa wastaafu na  wazee, Dk. Mwinyi alisema Serikali itaendelea na juhudi za kuimarisha maslahi yao, kwa kuhakikisha malipo ya viinua mgongo kwa wastaafu na pencheni jamii kwa wazee waliofikia umri wa miaka 70 zinazendelea kutolewa kwa wakati na bila usumbufu.

Alisema Serikali inaangalia uwezekano wa kupunguza umri huo wa wazee pamoja na kuongeza kiwango cha posho, pale hali ya uchumi itakapoimarika.

Akizungumzia juu ya changamoto mbalimbali zilizoelezwa katika Risala ya Wafanyakazi, ambapo nyingi zinahusiana na maslahi yao, alisema Serikali inazifahamu changamoto hizo na tayari imeanza kuzichukulia hatua, hivyo akawataka wafanyakazi kuendelea kuvuta subira kwa imani ya kupatiwa ufumbuzi hatua kwa hatua.

Alieleza kuwa taratibu na tathmni za miundo ya Utumishi Serikalini inaendelea kushughulikiwa ili kuhakikisha watumishi wote wanapata haki zao pamoja na kujengewa mazingira bora ya kufanyakazi ili kuongeza ufanisi.

Alisema kipindi kifupi cha Uongozi wa Awamu ya nane, Serikali imeanza vyema utekelezaji wa malengo yake kwa mujibu wa Mipango mikuu, ikiwemo ilani ya Uchaguzi muu wa CCM wa 2020-2025, MKUZA 11, Dira ya Zanzibar (2020-2050) pamoja na mingine ya kisekta na kimataifa.

Alisema hali ya nidhamu na uwajibikaji kwa watumishi serikalini inaendelea kuimarika, huku kukiwepo nidhamu katika matumizi ya fedha za umma kwa kiasi kikubwa.

Alisema kumekuwepo ufanisi katika utumishi wa umma katika kuwahudumia wananchi katika sehemu mbali mbali za utoaji huduma, ikiwemo hospitali, vituo vya Afya na Ofisi za Seriklai.

“Lazima tuendelee kujenga mazingira bora zaidi ya kuwafanya wananchi wajenge imani na wanufaike vizuri na huduma zinazotolewa serikalini pamoja na kuwaondolea urasimu na usumbufu usio na lazima”, alisema.

Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kutoa shukurani kwa sekta binafsi kwa kushirikiana na serikali na kutumia fursa za uwekezaji ziliopo nchini, huku akiwakumbusha umuhimu wa kuzingatia sheria na wajibu wa kulipa kodi na tozo mbali mbali, kuwapa mikataba wafanyakazi pamoja na kuwawekea fedha zao katika Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF).  

Aidha, aliwakumbusha wafanyakazi kutekeleza wajibu wao ipasavyo na kufanyakazi kwa bidii na nidhamu ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kukuza uchumi na kuimarisha huduma za kijamii, akibainisha mafanikio ya serikali yanategemea mchango mkubwa kutoka kwao.

Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa ushirkiano mkubwa inaotoa, sambamba na kuupongeza Uongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa kushirikiana vyema na Wizara ya Nchi (OR) Kazi, Uchumi na Uwekezaji, sambamba na kutoa shukurani kwa wafanyaakzi waliotunukiwa zawadi mbali mbali.

Mapema, Waziri wa Nchi (OR), Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mudrik Ramadhan Soraga alisema janga na ugonjwa wa Corona liloikumba Dunia, limeathiri ukuaji wa ajira Zanzibar, huku akiwashauri waajiri wote waliofunga Ofisi zao kutoka na ugonjwa huo kutafakari upya kwa kigezo kuwa wafanyakazi ni kiungo muhimu katika Taifa.

Aidha, alisema Wizara hiyo itaendelea kuimarisha ushirikiano na Idara mbali mbali ili kuona sekta ya kazi inaimarika na kukuza ajira.

Nae, Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyaakzi (ZATUC) Mwalim Ali Mwalim aliiomba Serikali kuliangalia kwa makini suala la Vikokotoo, kwa msingi kuwa limekuwa likilalamikiwa na wafanyakazi na wastaafu wengi kutokana na athari zake.

Katibu Mkuu ZATUC, Mwatum Khamis Othman, alisema  pamoja na mafanikio makubwa yaliofikiwa katika kuleta ustawi wa haki za wafanyakazi, alizitaja changamoto kadhaa zinazowakabili, ikiwemo kimya cha Serikali katika kupandisha mishahara na viinua mgongo kwa wastaafu.

Alisema kuna changamoto ya kukosekana utaratibu mzuri wa upandishaji wa madaraja na nyongeza za mwaka pamoja na upatikanaji wa posho mbali mbali za wafanyakazi, ikiwemo mazingira magumu.

Alieleza kuwa kuna changamoto kwa baadhi ya viongozi ya kutofuata taratibu za ajira pamoja na ucheleweshaji wa malipo ya madeni ya wafanyakazi, ikiwemo nauli.

“Kuna changamoto ya wafanayakzi wa mikataba ambao hufanyakazi kwa muda mrefu katika Halmashauri za wilaya”, alisema.

Vile vile, Mkurugenzi wa Jumuiya ya Vyama vya Waajiri Zanzibar (ZANEMA), Salah Salim salah aliwataka wafanyakazi kubadilika kwa kutoa huduma bora  katika maeneo yao ya kazi, kwa kigezo kuwa Dunia hii ni ya ushindani.

Katika hatua nyengine, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idrisa Kitwana Mustafa akiwasilisha salam za wafanyakazi wa Mkoa huo, alitoa pongezi kwa hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali katika usimamizi wa stahiki na haki za wafanyakazi, hususan katika sekta binafsi ikiwemo biashara ndogo ndogo.

Alisema pamoja na changamoto mbali mbali zilizojitokeza ikiwemo Ugonjwa wa Corona, Serikali imeweza kulipa mishahara ya wafanyakazi kwa wakati muafaka.

Maadhimisho hayo yalioambatana na kauli mbiu ya “Uwajibikaji na Haki ndio msingi wa maendeleo ya Zanzibar”, yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa kitaifa, akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdalla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Mawaziri, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Mhandisi Zena Ahmeid Said, ,Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama pamoja na Viongozi wa Vyama vya Siasa/ Dini.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.