RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali
Mwinyi amesema kwamba maendeleo na ibada haviwezi kufanyika iwapo hapatakuwa na amani.
Alhaj Dk. Mwinyi ameyasema hayo leo alipokuwa akitoa salamu zake kwa Waumini wa Dini ya Kiislamu pamoja na wananchi wote mara baada ya Sala ya Ijumaa huko katika Msikiti wa Wireless, Kikwajuni, Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi.
Katika salamu hizo,Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa amani ni ajenda ya kudumu, hivyo, kila mmoja anawajibu wa kuhakikisha amani inadumishwa hapa nchini.
Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza kwamba jamii yote ina wajibu ya kuidumisha amani huku akieleza kwamba katika kuimarisha na kudumisha amani lazima misukusuko itakuwepo lakinini vyema jamii inapiga hatua na inavuka.
Alisema kwamba hakuna jambo lisilozungumzika pindi mitihani inapotokea hivyo, ni vyema pale mitihani inapotokea jamii ikakaa chini na kuzungumza kwa azma ya kupata muwafaka kwa lengo la kudumisha amani, mshikamano na umoja uliopo.
Alisema kwamba hatua hiyo ndiyo itakayosaidia kwa kiasi kikubwa kuweza kupata maendeleo na mafanikio hapa nchini na duniani kwa ujumla.
Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alisisitiza umuhimu wa kufanya kazi na kusema kwamba hilo lisionekane ni jambo la viongozi pekee yao bali ni la kila raia ambaye ana wajibu wa kufanya kazi.
Alhaj Dk. Miwnyi alisema kwamba kila mmoja ana wajibu wa kufanya kazi pale alipo na iwapo jamii itaamua kufanya kazi maendeleo hayatapatikana zaidi.
Aliongeza kuwa jamii yote ikiamua kufanya kazi kwa bidii maendeleo yanayotakiwa yatapatikana huku akitolea mfano wahudumu katika sekta ya afya na elimu wakitoa huduma zao mafanikio makubwa yatapatikana katika sekta zote hata wale walio kuwa hawako katika ajira rasmi nao wana wajibika kufanya kazi ili kujikwamua na umasikini uliopo.
Alisema kwamba ni muhimu kwa kila mmoja kufanya kazi na kuwajibika katika kazi kwani wale wote waliopewa majukumu iwapo watawajibika yale yote yanayotakiwa zikiwemo huduma za afya, maji, barabara, umeme na nyenginezo zitapatikana.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alisisitiza haja kwa waumini kuwa wamoja bila ya kutofarikiana na kugombana na kueleza haja ya kuendeleza amani, umoja na mshikamanomiongoni mwao ili kupata rehema za Mwenyezi Mungu.
Mapema akisona hotuba ya Sala ya Ijumaa, Sheikh Abdallah Swaleh aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuendeleza ibada hasa katika mwezi huu wa Dhulhijjah.
Aidha, Sheikh Abdallah Swaleh alieleza kwamba si vyema kukawepo mivutano katika muwandamo wa mwezi na kuwataka waumini wasikwazane na wala asitokee mmoja wao miongoni mwao na kujifanya ni bora zaidi kuliko mwengine.
Alisema kuwa hakuna haja ya kuwepo kejeli kwa walimu na wanawazuoni kwa sababu ya kutafautiana katika muandamo wa mwezi.
Alisema kuwa teknolojia imekuja hivi sasa na hapo zamani haikuwepo teknolojia hiyo hivyo, ni vyema waumini wakajiuliza Wazee, Mashekhe na Mtume wao Muhammad (S.A.W) wote hao walifanya vipi ibada wakati huo huku akisisitiza kwamba wapo watu wenye mamlaka waliopewa kazi ya kusimamia hilo hivyo, ni vyema wakafuatwa.
Sheikh Abdallah alisema kwamba dini ya Kiislamu haiwezi kuendeshwa na teknolojia na badala yake itabaki kama asili yake ilivyokuwa na kueleza kwamba ni vyema kuwafuata Masheikh na Walimu waliopita ambao walitegemea zaidi hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024
2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk.
No comments:
Post a Comment