Habari za Punde

Naibu Waziri Atua Same Mashariki Kutatua Changamoto za Mawasiliano ya Simu, Data na Redio.

 

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Vuje kilichopo Kata ya Vuje Wilayani Same wakati wa ziara yake ya kukagua ubora na upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika wilaya hiyo.

Na Mwandishi wetu, SAME                                                                                                                       

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Mhandisi Kundo Mathew amefanya ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma ya mawasiliano ya simu, data na redio katika kata mbili za Vuje na Bombo zilizopo katika wilaya ya Same, jimbo la Same Mashariki na kuahidi kutatua changamoto za mawasiliano kwa wananchi kwasababu ni haki yao ya msingi na sio hisani                                                                     

Katika ziara yake Mhandisi Kundo aliambatana na watendaji kutoka taasisi nne za mawasiliano zilizo chini ya Wizara hiyo ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Shirika la Posta Tanzania (TPC) pamoja na wawakilishi kutoka katika makampuni ya simu ya Airtel, Tigo, TTCL, Halotel na Vodacom

Mhandisi Kundo alisikiliza kero na malalamiko ya wananchi kuhusu kukosekana kwa huduma ya mawasiliano ya simu za mkononi na intaneti ambazo zinasababisha athari mbalimbali za kijamii, kiuchumi pamoja na watumishi wa Serikali kupata changamoto mbalimbali za kupokea na kutuma taarifa kupitia mifumo mbalimbali ya TEHAMA

Amesema kuwa Wizara hiyo inaelewa changamoto ya mawasiliano iliyopo katika eneo hilo na tayari hatua mbalimbali zimeshaanza kuchukuliwa ikiwa ni pamoja na UCSAF kutangaza awamu ya sita ya zabuni za kupeleka mawasiliano katika maeneo ya mipakani ambapo katika jimbo la Same Mashariki minara itajengwa katika vijiji vya Mbwambo, Ugwama na Mwatemi

Naye Mkuu wa Uendeshaji wa UCSAF Mhandisi Albert Richard amesema kuwa baada ya kufika katika eneo la kata ya Vuje Kijiji cha Vuje amekuta kuna mnara wa simu wa Airtel lakini bado hali ya mawasiliano sio nzuri na kuahidi kuyaomba makampuni ya simu kuweka vifaa vyao kwenye mnara wa Airtel uliopo ili huduma ya mawasiliano ya mitandao mingine iweze kupatikana

Aliongeza kuwa kulingana na jiografia ya eneo hilo ambalo lina vilima na mabonde linahitaji mnara zaidi ya mmoja ili kupatikana kwa huduma bora za mawasiliano ambapo kwa hatua za awali ni vizuri kuboresha mnara uliopo ili angalau wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano wakati taratibu za Serikali za kujenga minara katika maeneo hayo zikiendelea kwa awamu

Akizingumzia upande wa malalamiko ya kuwa na redio yao Mkuu wa TCRA Kanda ya Kaskazini Mhandisi Imelda Salum amesema kuwa TCRA imeshatenga masafa kwa ajili ya Wilaya ya Same na ndani ya mwezi wa saba masafa hayo yatatangazwa ili wawekezaji wajitokeze kwa ajili ya kuanzisha redio ambayo itafikisha mawasiliano ya redio katika wilaya ya Same

Aidha, wawakilishi wa makampuni ya simu walioambatana nae katika ziara hiyo wameahidi kushughulikia changamoto za mawasiliano katika eneo hilo ambalo linaonekana kuwa na mvuto kibiashara ikiwa ni pamoja na kupeleka huduma ya laini za simu na vocha kwa upande wa kampuni ya Halotel

Naye Mbunge wa Same Mashariki Mhe. Anne Kilango Malecela ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Miundombinu amezungumza na wananchi wake na kuwaambia kuwa Serikali inajali na kushughulikia kero na malalamiko ya wananchi wake kwa kuboresha upatikanaji wa huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na huduma ya mawasiliano

 

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.