Habari za Punde

Viongozi wa Serikali Wapeni Nafasi Maafisa Habari -Msigwa

 

Mkurugenzi wa Idara ya Habari na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ametoa wito kwa Viongozi wa Wizara, Taasisi na Idara zote za Serikali kuwahusisha Wataalamu wa Habari (Wasemaji) kuhusu masuala yote yanayohusu ofisi za ili waweze kuwa na uelewa mpana utakaowawezedha kuzitangaza kwa ufanisi shughuli za utekelezaji wa Serikali. 

Msigwa ametoa wito huo leo Julai 20, 2021 wakati akizungumza katika kipindi cha asubuhi cha 360 kinachorushwa na kituo cha Televisheni cha Clouds.

“Maelekezo ya Serikali yalishatolewa kwamba hawa Maafisa Habari wanapaswa wahusishwe na kushirikishwa katika vikao vyote vya maamuzi na wapewe nafasi ya kuzisemea Wizara, Taasisi na Idara zao, na kuna kazi inayoendelea ya kuiweka vizuri  miundo hii ”, alisema Msigwa.

Aidha, amewataka Maafisa Habari kuhakikisha wana taarifa za kutosha katika maeneo yao.

Msemaji Mkuu wa Serikali ameongeza kuwa wakati mwingine tatizo si la Taasisi wala Wizara ni la Afisa habari mwenyewe kwa sababu anakuwa hana taarifa ya jambo fulani na ndiyo inapelekea yeye kutokuwa na majibu.

“Hakuna ukweli kwamba kila Waziri au Katibu Mkuu au Mkuu wa Taasisi  kamzuia Afisa Habari wake kuzungumza masuala ya eneo lake, lakini ni jambo tunaenda kulifanyia kazi”, alisisitiza Msigwa.

Hii ni mara ya kwanza tangu alipoteuliwa kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali kushiriki katika kipindi cha 360.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.