Habari za Punde

Wananchi Muleba Waiomba Serikali Kuwafikishia Mawasiliano ya Redio na Simu.

 

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akizungumza alipotembelea na kukagua mnara wa mawasiliano wa Vodacom katika Kijiji cha Kyamyorwa Kata ya Kwasharunga Wilayani Muleba. Wengine ni watendaji alioambatana nao.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (wa pili kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF)  wakati wa ziara yake ya kukagua hali ya upatikanaji wa mawasiliano katika kijiji cha Kakoma kilichopo Wilayani Muleba.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Mhandisi Francis Mihayo akielezea utaratibu wa kufuata ili kupata leseni ya kuanzisha redio.

Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew (kulia)  akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila kipeperushi cha huduma kwa mteja cha Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kabla ya kuanza ziara yake ya kikazi ya kukagua hali ya upatikanaji wa huduma ya mawasiliano katika Wilaya hiyo

Na Faraja Mpina, MULEBA.                                                                                                                                    

Wananchi wa Wilaya ya Muleba wameiomba Serikali kuwafikishia huduma za mawasiliano ya redio na simu wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Kundo Mathew wilayani humo

Kwa nyakati tofauti wananchi wamezungumzia hisia zao za kukosa mawasiliano ya redio za Tanzania hasa redio ya Taifa TBC na matokeo yake wanasikiliza redio za nchi jirani ya Rwanda hivyo kushindwa kuelewa nini kinaendelea ndani ya nchi yao

Wakati huo huo Mkuu wa Wilaya ya Muleba Mhe. Toba Nguvila amesema kuwa Halmashauri ya Wilaya hiyo imeshaanza mchakato wa kuanzisha redio ya jamii lakini mchakato umekuwa mrefu kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) hivyo kumuomba Naibu Waziri huyo kuingilia kati suala hilo ili redio hiyo ianzishwe na kuanza kuwahudumia wananchi wa Muleba

Mhandisi Kundo alifanya ufuatiliaji wa hatua iliyofikiwa kupitia Mkuu wa Kanda ya Ziwa Mhandisi Francis Mihayo aliyeambatana nae katika ziara hiyo ambapo alimpigia simu Afisa anayeshughulikia maombi hayo wa TCRA Makao Makuu ambaye alitolea ufafanuzi kuwa maombi rasmi bado hayajafika katika ofisi hizo lakini Afisa wa Halmashauri ya Muleba alifika akiwa na mshauri wake na akamuelekeza namna ya kuandaa andiko la maombi hayo na mpaka sasa bado hayajawasilishwa

Mhandisi Mihayo alitolea ufafanuzi wa suala hilo kwa kuzungumzia umakini wa TCRA katika mchakato mzima wa kutoa leseni ya kuanzishwa kwa redio yeyote nchini ambapo alisema kuwa Afisa wa Halmashauri hiyo alitakiwa kufika kwenye ofisi za TCRA Kanda ya Ziwa ili kupata ushauri na huduma ya kuanzisha redio hiyo badala ya kwenda moja kwa moja Makao Makuu ya TCRA Dar es Salaam

Aidha, Mhandisi Kundo ametoa maelekezo kwa Mamlaka hiyo kuhakikisha inaharakisha mchakato wa kutoa leseni ya kuanzishwa kwa redio hiyo pindi maombi rasmi yakiwafikia kwa sababu Serikali inapokwamisha maombi ya usajili ni kumhujumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anaamini watendaji wake wapo kwa ajili ya kumsaidia

Katika hatua nyingine Mhandisi Mihayo amesema kuwa taratibu za kuweka mitambo ya kuongeza usikivu wa redio ya TBC katika maeneo ya Kanda ya ziwa hasa mipakani zinaendelea ikiwa ni pamoja na maeneo ya Wilaya ya Muleba ikiwemo Kijiji cha Kakoma ifikapo Oktoba 2021

Kwa upande wa mawasiliano ya simu Mkuu wa Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Mhandisi Albert Richard amesema kuwa amepokea mahitaji ya wananchi wa Muleba na Mfuko huo utavijumuisha vijiji vyenye changamoto ya mawasiliano katika zabuni zao ikiwa ni muendelezo wa kufikisha mawasiliano maeneo ya vijijini na mipakani

Imetolewa na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote

Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.