Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinti Amekutana na Kuzungumza na Mabalozi Walioteuliwa wa Tanzania Walioteuliwa Hivi Karibu Kuiwakilisha Tanzania Nje.

Rais wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipokuwa akizungumza na Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tanzania katika Nchi mbali mbali Duniani wakati walipofika kuonana na Mhe.Rais Ikulu Jijini Zanzibar.[Picha na Ikulu] 20/09/2021.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nje ya nchi walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuitekeleza Sera ya Diplomasia ya Uchumi kwa vitendo ili kuiletea maendeleo zaidi Tanzania.

Rais Dk. Mwinyi alieleza hayo leo Ikulu Zanzibar wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, walioteuliwa hivi karibuni kwenda kuiwakilisha Tanzania nje ya nchi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba Sera iliyopo hivi sasa katika Jamhauri ya Muungano wa Tanzania ni Diplomasia ya Uchumi, hivyo ni vyema Mabaozi hao wakaitekeleze kwa vitendo katika vituo vyao walivyopangiwa.

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa miongoni mwa hatua za utekelezaji wa Sera hiyo ya Diplomasia ya Uchumi ni kuitangaza Tanzania ikiwemo Zanzibar katika sekta ya uwekezaji kutokana na fursa mbali mbali ziliopo hivi sasa.

Aliongeza kuwa kwa upande wa Zanzibar sekta ya utalii ni miongoni mwa seka iliyopewa kipaumbele kikubwa kwani imekuwa ikisaidia kwa kiasi kikubwa katika kuongeza pato la Taifa hivyo ni vyema wakaiwekea kipaumbele cha pekee.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba sekta hizo ni miongoni mwa sekta zilizowekewa mikakati maalum na Serikali ya Awamu ya Nane katika kuimarisha Uchumi wa Buluu zikiwemo uvuvi, bandari, mafuta na gesi asilia ambazo zinahitaji msukumo wa viongozi hao kuzitafutia wawekezaji katika vituo vyao.

Rais Dk. Mwinyi alieleza kwamba mbali na uwekezaji bado Tanzania ikiwemo Zanzibar imekuwa ikiagiza kwa kiasi kikubwa bidhaa nje ya nchi kuliko kuzalisha wenyewe bidhaa zake hivyo, alisisitiza haja ya kuimarisha sekta ya biashara ili Tanzania nayo iweze kuuza nje bidhaa zake sanjari na kupanua soko la ajira na kuongeza kodi.

Akizungumzia suala la kuimarisha amani na utulivu, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa ni vyema mashirikiano ya kuhakikisha amani na utulivu vinaimarishwa kwa pamoja hasa kwa nchi zilizopakana na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ikiwemo Rwanda.

Amesema kuwa miongoni mwa nchi ambazo hivi sasa zimeonesha nia na kuamsha ari kubwa ya kuja kuekeza nchini ikiwemo Uturuki, ni vyema mashirikiano, na uhusiano ukaimarishwa zaidi ili wawekezaji kutoka nchi hiyo wazidi kuongezeka hapa nchini.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi alieleza haja kwa Mabalozi hao kuendelea kuitangaza Tanzania hasa Marekani ambako inaonesha bado Tanzania haijatangazwa zaidi kiutalii kutokana na watalii wanaokuja kuitembelea Tanzania kuwa wachache.

Hata hivyo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza Mabalozi hao kwamba kutayarishwa kwa kipindi cha “The Royal Tour” ambacho kimemuhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kwa ajili ya kuitangaza Tanzania hasa katika sekta ya utalii kutaitangaza zaidi Tanzania katika nchi za Marekani, Ulaya, Asia na Afrika.

Rais Dk. Mwinyi aliwapongeza Mabalozi hao wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania akiwemo Balozi Elsie Sia Kanza anaekwenda Marekani,Balozi Luteni Jenerali Yakob Hassan Mohamed anaekwenda nchini Uturuki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo anaekwenda nchini Italia, Balozi Hoyce Anderson Temu anakwenda nchini Switzerland, Balozi Meja Jenerali Richard Mutayoba Makanza anaekwenda nchini Rwanda na Balozi Grace Alfred Olotu anaekwenda nchini Sweden.

Nao Mabalozi hao kwa upande wao walimuhakikishia Rais Dk. Miwnyi kwamba watahakikisha wanatekeleza kwa vitendo Sera ya Diplomasia ya Uchumi hasa kwa kutambua kwamba hiyo ndio dira ya Tanzania hivi sasa.

Wakizungumza kwa niaba ya Mabalozi wenzao waliofika Ikulu Balozi Mahmoud Thabit Kombo na Balozin Else Sia Kanza walimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kuwapa maelekezo na kueleza matarajio waliyonayo wananchi wa Tanzania kwao katika kuyatekeleza majukumu waliyopewa ambayo wameahidi kuyafanyia kazi kwa mashirikiano ya pamoja.

Imetayariswha na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.