Habari za Punde

TAFIRI Yatakiwa Kufanya Kazi Yenye Tija Kwenye Sekta ya Uvuvi.

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb), akizungumza na baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), mara baada ya kufanya ziara ya kikazi ya siku moja katika makao makuu ya taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam na kuwataka wafanyakazi hao kufanya kazi yenye tija kwa jamii kupitia sekta ya uvuvi.

 (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari - Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Na. Edward Kondela

Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI) imetakiwa kufanya kazi zenye tija kwa jamii na kutoa ushauri wa kisayansi namna ya kuhakikisha sekta ya uvuvi inakua na kusaidia watanzania katika masuala ya uvuvi

 

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (Mb) amebainisha hayo jana (06.09.2021) wakati alipofanya ziara ya kikazi ya siku moja katika makao makuu ya taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam na kubainisha kuwa TAFIRI inategemewa katika kufanya tafiti za uvuvi kwa manufaaa ya sasa na yajayo na kuwafanya wavuvi kuwa na kipato endelevu ili shughuli hiyo ifanywe kitaalamu.

 

Aidha, amepongeza Mradi wa Usimamizi Shirikishi wa Rasilimali za Uvuvi Kusini Magharibi mwa Bahari ya Hindi (SWIOFISH), ambapo umewezesha kujengwa kwa jengo la maabara ya TAFIRI ambalo litaongeza wigo katika kufanya tafiti za uvuvi hapa nchini.

 

Amefafanua kuwa SWIOFISH imekuwa ikifanya kazi ya msingi na muhimu nje ya nchi na kuhakikisha fedha ambazo zimetolewa na Benki ya Dunia katika mradi huo zinasimamiwa vyema na kufikia malengo yaliyokusudiwa.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAFIRI Dkt. Ishmael Kimirei amemwambia Waziri Ndaki juu ya changamoto mbalimbali wanazokabiliana nazo zikiwemo za vifaa vya maabara baada ya jengo la maabara kukamilika ambapo amesema vifaa hivyo vinagharimu Shilingi Bilioni 1.5.

 

Kutokana na ukosefu wa vifaa vya maabara, Waziri Ndaki amemhakikishia mkurugenzi huyo kuwa, ataliwekea uzito jambo hilo kuanzia sasa na mwaka ujao wa fedha ili vipatikane vifaa hivyo na jengo hilo lifanye kazi ya utafiti pekee badala ya kuwa na vyumba vya ofisi.

 

Naye Mratibu wa mradi wa SWIOFISH Bw. Nichrous Mlalila amesema mradi huo wa miaka sita hapa nchini unaotarajia kufikia tamati mwezi Septemba mwaka 2022, umefadhiliwa na Benki ya Dunia na lengo la mradi ni kusimamia masuala ya uvuvi kuanzia ngazi ya utawala hadi kwa wavuvi pamoja na ushirikiano kwa kikanda katika kuhakikisha unaboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya uvuvi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.