Habari za Punde

Ushirikiano Ndio Siri ya Mafanikio ya Wizara Hiyi ya Ulinzi : Hussein Mwinyi.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na mgeni wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Dk.Stergomena Tax (kulia kwa Rais) alipofika Ikulu Zanzibar kwa mazungumzo yaliofanyika katika ukumbi wa Ikulu leo 23-9-2021.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuna na kufanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Lawrence Tax na kumueleza kwamba ushirikiano ndio siri ya mafanikio ya Wizara hiyo.

Rais Dk. Mwinyi alikutana na kufanya mazungumzo  na Waziri Dk. Tax leo Ikulu  Zanzibar, ambapo Waziri huyo alikuja kwa ajili ya kujitambulisha kwa Rais Dk. Mwinyi baada ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambaye pia ni  Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan hivi karibuni.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Mwinyi alimueleza Waziri Dk. Tax kwamba mashirikiano ya pamoja yaliopo katika Wizara hiyo ndio yanayoleta mafanikio hasa mashirikiano kati ya Taasisi za Ulinzi na Wizara.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Wizara hiyo ni Wizara ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ameridhika kwa kazi nzuri inayofanya huku akisisitiza kwamba mashirikiano makubwa kati ya Wizara hiyo na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni makubwa.

Pamoja na hayo, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kumpongeza kwa dhati Waziri Dk. Tax kwa kuteuliwa kushika wadhifa huo na kueleza kuwa ana imani kubwa kwamba Wizara hiyo iko salama kutokana na utendaji mzuri wa Waziri Dk. Tax.

Nae Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dk. Stergomena Lawrence Tax kwa upande wake alimpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa imani kubwa iliyooneshwa kwake na hatimae kuteuliwa kushika wadhifa huo ambao aliahidi kuufanyia kazi kwa manufaa ya pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Waziri Dk. Tax alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Mwinyi kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata maendeleo makubwa.

Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.