Habari za Punde

Uzembe Idara ya Fedha Wawakera Madiwani.

Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Mkoani Tabora Bi.Fatma Latu (aliyesimama) akiongea katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kilichofanyika jana mjini humo. Picha na Lucas Raphael.

Na Lucas Raphae,Igunga


MADIWANI wa halmashauri ya wilaya ya Igunga Mkoani Tabora wamemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri Fatma Latu kuchukua hatua stahiki ili kukomesha uzembe uliopo katika idara ya fedha.

 

Ushauri huo umetolewa na madiwani katika kikao cha robo ya nne ya baraza hilo kilichofanyika jana katika ukumbi wa mikutano wa halmashauri.

 

Jidashema Lukeleja, diwani wa kata ya Bukoko alisem kuwa Ofisi ya Mweka Hazina wa halmashauri (DT) imeshindwa kudhibiti mapato ikiwemo kusimamia timu ya wakusanya mapato na kibaya zaidi hata taarifa ya fedha hawasomewi. 

 

Alibainisha kuwa pasipo usimamizi makini na watendaji waaminifu mapato ya halmashauri yataendelea kupotea hivyo kukwamisha utekelezaji miradi ya maendeleo.

 

Diwani wa kata ya Nanga Robert Jidai alisema licha ya Watendaji kupewa mashine za kielektroniki (POS) kwa ajili ya kukusanyia ushuru wamekuwa sio waaminifu huku wengine wakikaa na fedha hizo nyumbani kwao.

 

Alisisitiza kuwa mapato yanayokusanywa ni lazima kila siku ijulikanae nani kakusanya sh ngapi na ziko wapi, na kila aliye na mashine ya POS atoe taarifa ya makusanyo yake kila siku.

 

Akifafanua hoja hiyo Mwenyekiti wa halmashauri hiyo Lucas Bugotta ambaye ni diwani wa kata ya Mbutu alisema ofisi ya Mweka Hazina imekuwa haiwasilishi taarifa za fedha katika vikao vya baraza licha ya kutakiwa kufanya hivyo ndiyo maana kumekuwa na maswali mengi.

 

Alisisitiza kuwa taarifa ya mapato inapaswa kuwasilishwa katika vikao vyote vya baraza ili mapungufu yaliyomo yajadiliwe na kutolewa maamuzi, lakini hilo limekuwa halifanyiki. 

 

Alibainisha kuwa waliagiza taarifa za fedha zikaguliwe na Mkaguzi wa ndani na tupewe taarifa juu ya mapungufu yaliyopo ikiwemo majina ya wale wote waliopewa mashine za POS na taarifa zao kutoonekana lakini hadi sasa hakuna utekelezaji wowote. 

 

‘Mapato yanayokusanywa yanapaswa kujulikana ni kiasi gani na yako wapi na kila mwenye mashine ya POS anapaswa kuwasilisha mapato hayo benki na sio kuficha mashine, hapa kuna kitu kinafichwa’, alisema.

 

Bugotta aliagiza kila diwani kusimamia ipasavyo vyanzo vya mapato katika kata yake na kuhakikisha kila anayelipa ushuru au kodi anapatiwa risiti.

 

Alimwagiza Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuchukua hatua stahiki ili kukomesha tabia hiyo ikiwemo kuwachukulia hatua wale wote waliozembea au kutumia vibaya fedha za ushuru walizokusanya kwenye vyanzo mbalimbali.

 

Ili kukomesha hali hiyo diwani Matikiti Masala wa kata ya Sungwa alishauri Ofisi ya Mkurugenzi kufumua timu yote ya ukusanyaji mapato ikiwemo kuondolewa DT ili kuharakisha maendeleo ya halmashauri hiyo.

 

Naye Alfred Gedy, diwani wa kata ya Nguvumoja alibainisha kuwa taarifa ya fedha ya halmashauri ina mapungufu mengi sana na walishaagiza ikaguliwe lakini hakuna kilichofanyika, hivyo akashauri Mkurugenzi wa halmashauri hiyo na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kuchukua hatua stahiki ili kumaliza sintofahamu hiyo kwani inarudisha nyuma ya wilaya hiyo. 

 

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo Fatma Latu alikiri kukuta mapungufu makubwa ya kiutendaji  katika halmashauri hiyo hivyo akaomba ushirikiano ili kurekebisha hali hiyo, aidha aliahidi kusimamia ipasavyo suala zima la mapato ambalo limekuwa likilalamikiwa. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.