Habari za Punde

WANANCHI WASHAURIWA KUFUGA SAMAKI KWA KUCHIMBA MA BWAWA KATIKA MAENEO YAO WANAYOISHI.

Mmoja wa vijana anayefanya kazi katika kituo cha ufugaji samaki katika skimu ya umwagiliaji Mwamapuli  Julius Mussa aliyekodiwa kuvuna samaki wa bw. Anthony Marco ambaye akiwa ndani ya bwawa ameshika samaki. 
Afisa mfawidhi kituo cha ukuzaji viumbe majini wilaya ya Igunga mkoani Tabora Joachim John(Kushoto), akiwa na Anthony Marco (kulia) ambaye pia ni afisa biashara wilaya ya Igunga wakiwa na samaki waliowavuna na kuwapima kwenye  mzani katika eneo lake la makazi ambamo ndani yake kuna bwawa la samaki hao.   

Na Lucas Raphael,Tabora

Katika kuunga mkono juhudi za serikali za kujiongezea kipato wananchi wa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wameshauriwa kufuga samaki kwa kuchimba mabwawa ya kufugia samaki katika maeneo yao ili waweze kujikwamua kiuchumi pasipo kutegemea ajira serikalini.

Ushauri huo umetolewa na afisa mfawidhi kituo cha ukuzaji viumbe majini katika skimu ya umwagiliaji Mwamapuli wilaya ya Igunga Joachim John wakati wa zoezi la uvunaji wa samaki aina ya Kambale katika bwawa la samaki la afisa biashara wilaya ya Igunga Anthony Marco.

Alisema zao la samaki halina gharama kubwa katika kuwatunza samaki wakiwa katika bwawa huku akibainisha kuwa endapo kila mwananchi atatenga eneo la kuchimba bwawa la samaki katika eneo analoishi ndani mwaka mmoja anaweza kujipatia mamilioni ya fedha.

Alibainisha kuwa kituo cha ukuzaji viumbe majini kilichopo katika skimu ya umwagiliaji Mwamapuli kuna vifaranga vya samaki vya kutosha ambapo kuna aina mbili Kambale na sato na kifaranga kimoja kinauzwa kuanzia sh. 100 hadi 150.

Hata hivyo alisema kituo chao kimekuwa kikitoa elimu bure kwa waliofuga samaki na kuwashauri wananchi wengine kuchangamkia fursa hiyo ya kufuga samaki na kuachana na utaratibu wa kutegemea kazi moja ya kilimo.

Nae mmoja wa vijana anayefanya kazi katika kituo cha ufugaji samaki katika bwawa hilo Julius Mussa alisema ufugaji wa samaki ni mzuri sana kwani kwa muda mfupi unakipato kikubwa cha fedha lakini changamoto kubwa ni ukosefu wa mtaji, huku akiiomba serikali kuwawezesha vijana mikopo kupitia halmashauri za wilaya.

Nae mfugaji wa samaki katika bwawa hilo ambaye pia ni afisa biashara wilaya ya Igunga Anthony Marco alisema aliamua kuchimba bwawa katika eneo lake la makazi na kufuga samaki kwa kutumia maji ya ziwa Victoria baada ya kuona kwenye mitandao na majarida mbalimbali yakionyesha faida ya ufugaji wa samaki.

Alisema baada ya kuchimba bwawa nyumbani kwake mtaa wa Masanga mjini Igunga alinunua vifaranga vya samaki aina mbili ambapo Kambale vifaranga 2600 na sato 400 hata hivyo hakuweza kutaja kiasi cha fedha alichonunua kwa vifaranga vyote.

Alisema maji yanayotumika katika bwawa hilo yamekuwa yakitumika pia kumwagilia shamba la vitunguu huku akisema hivi sasa samaki hao wana mwaka mmoja tangu awanunue na kuwafuga.

Alisema hivi sasa ameanza kuwavuna samaki hao ambapo amekuwa akiwauza kuanzia bei ya sh. 3000, 5000 hadi 10,000 kwa samaki mmoja.

Anthony alisema hivi sasa ameamua kutafuta eneo kubwa vijijini ili aweze kuchimba mabwawa makubwa ikiwa ni moja ya kupanua ufugaji wa samaki kwani amebaini zao la samaki lina faida kubwa kiuchumi.

Sambamba na hayo Anthony alimshukuru afisa mfawidhi kituo cha ukuzaji viumbe majini katika skimu ya umwagiliaji Mwamapuli Joachimu John kwa elimu ambayo amekuwa akiitoa katika suala zima la ufugaji wa samaki ambapo amekuwa akitembelea bwawa hilo mara kwa mara na kutoa elimu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.