Habari za Punde

Dc Atoa Maagizo, Atakaeshiriki Kumtorosha Mwanafunzi Atakamatwa Kupelekwa Shule Akasome

Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Ndg.Kalisti Lazaro akizungumza na Wananchi wa Wilaya hiyo wakati wa ziara yake.

Na Hamida Kamchalla, LUSHOTO.

MKUU wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro amemuagiza Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya hiyo kuhakikisha umaliziaji wa shule ya msingi Gare B unakamilika kwa wakati ili ifikapo januari 2022 wanafunzi waanze kupokelewa katika shule hiyo.Lazaro alitoa agizo hilo juzi wakati walipofanya ziara ya jimbo katika kata ya Gare akiambatana na mbunge Shabani Shekilindi ambapo walikagua miradi mbalimbali ya ujenzi.

Aidha aliagiza kutafutwa na kuhojiwa kwa wote waliohusika kwenye usimamizi wa mradi na matumizi mabaya ya fedha za mradi baada ya kuwepo na utata katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu kujengwa tofauti na thamani ya fedha iliyoidhinishiwa."Wale wote waliojenga mradi huu watafutwe, wahojiwe na hatua stahiki zichukuliwe dhidi yao, kulingana na maelezo yaliyotolewa, ni kwamba nyumba hii imejengwa tofauti na fedha, hapa thamani ya fedha haipo" alisema.
Hata hivyo mkuu huyo alipiga marufu tabia ya baadhi ya watendaji wa serikali wanaowaonea wananchi huku akiwataka viongozi wa serikali kutenda haki katika kutoa maamuzi wanayoyafanya hasa katika mabaraza ya ardhi na nyumba ngazi ya kata yanayoendesha mashauri bila kuzingatia sheria na kuendekeza rushwa.

"Nikuagize mwanasheria wa Wilaya, upate muda wa kutoa elimu na mafunzo ya namna ya kuendesha mashauri ya ardhi lakini pia niwasihi na wazazi na walezi wenye watoto waliomaliza mtihani wa darasa la saba kuacha mara moja tabia ya kuwaozesha watoto wa kike au kuwatafutia kazi za ndani kwani serikali imeandaa miundombinu ya shule kwa ajili yao kupata elimu ya sekondari" alisema.

"Mzazi ambaye mtoto wake atafaulu na kupangiwa kujiunga na elimu ya sekondari, kama asipofika shule aliyopangiwa na tukibaini mzazi ameshiriki kumtorosha au kumuozesha mtoto, tutamkamata huyo mzazi ili asone kwa niaba ya mtoto wake" aliongeza Lazaro.

Awali kabla ya maagizo ya mkuu wa Wilaya, mbunge wa Lushoto Shabani Shekilindi alitoa agizo hilo baada ya kutoridhishwa na mradi wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu ambapo alisema kuwa kiasi cha fedha kilichotolewa kwa ajili ya ujenzi huo ni sh milioni 6 lakini nyumba hailingani na fedha zilizotumika.

"Mhe mkuu wa Wilaya, mradi huu wa ujenzi wa nyumba ya mwalimu ulitengewa kiasi cha sh milioni 6 tokea mwaka 2006 na fedha zilitafunwa lakini kulikuwa na kesi na mwaka 2017, fedha hizo zilirejeshwa lakini Jengo ni kama unavyoliona hapo, haieleweki hii milioni 6 ilifanya kazi gai nini" alibainisha Shekilindi. 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.