Habari za Punde

Dkt.Kijaji Azungumza na Wakuu wa Taasisi Baada ya Wiki Tatu Tangu Kuapishwa Kwake*Asema Wizara yake ni Wezeshi kwa maendeleo ya Taifa *Awataka watumishi wawe wazalendo *Watekeleze Mkataba baina ya CCM na Serikali kwa kuhudumia wananchi

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Ashatu Kijaji akizungumza na wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo katika ukumbi wa Ofisi za Wizara hiyo zilizopo Mji wa Serikali Mtumba, Dodoma. Kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew na Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula.

Na.Prisca Ulomi na Faraja Mpina

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Ashatu Kijaji amekutana na  Wakuu wa taasisi zilizo chini ya Wizara katika kikao kazi kilichofanyika jana tarehe 04/10/2021 katika ofisi za Wizara hiyo zilizopo mji wa Serikali Mtumba, Dodoma baada ya wiki tatu tangu  alipoteuliwa na kuapishwa kuongoza Wizara hiyo

Dkt. Kijaji amesema kuwa kikao hicho kilikuwa na lengo la kufahamiana, kukumbushana na kutambua majukumu yao katika Taifa kwa kuitumikia Serikali iliyopo madarakani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo iliingia Mkataba mahsusi na wananchi kupitia Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020 – 2025

“Wizara hii ni sehemu ya Serikali na tuna jukumu la kuhakikisha Mkataba ambao chama cha CCM kiliingia na wananchi unatekelezeka ipasavyo katika tasnia za Habari, Mawasiliano na TEHAMA kwa kutekeleza jukumu kubwa la kuwawezesha watanzania kupata mawasiliano na habari ambazo zina athari chanya kwenye maisha yao kijamii na kiuchumi”, amezengumza Dkt. Kijaji

Amesema kuwa Wizara hiyo ni Wizara wezeshi lakini imekuwa ikichangia pato la Taifa kwa asilimia 1.5 kwa miaka minne mfululizo kitu ambacho anakiona hakijakaa sawa hasa ukizingatia kama Taifa tunaelekea kwenye uchumi wa dijitali ambapo Wizara hiyo pamoja na taasisi zake wanapaswa kuangalia upya na kuleta mabadiliko ya mchango wao kwa pato la Taifa

Ameongeza kuwa watendaji wakuu wa taasisi za Wizara yake wahakikishe wanakuwa wazalendo na kuleta tafsiri sahihi ya viti walivyoaminiwa na Serikali kuvikalia kwa kuhakikisha wanawafikishia watanzania huduma zenye viwango na ubora unaohitajika

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Zainab Chaula amezungumzia kikao hicho kuwa kilikuwa ni kikao cha Waziri kufahamiana na Wakuu wa taasisi na kukumbushana kutimiza wajibu kwa watendaji hao kuwajibika kwa matokeo ambayo ni kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa matokeo chanya zinamfikia mwananchi

Naye Kaimu Postamasta Mkuu  wa Shirika la Posta Tanzania, Macrise Mbodo amesema kuwa kikao hicho kimetengeneza uelewa wa pamoja kati ya utendaji wa taasisi na matamanio na matarajio ya Waziri huyo ya utendaji wa taasisi hizo kwa matokeo ambapo wakuu wa taasisi hizo walipata fursa ya kueleza majukumu ya msingi ya taasisi zao, zilipotoka na zinapoelekea

Kikao hicho kilihudhuriwa na wakuu wa taasisi za Wizara hizo ambazo ni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), Kampuni ya Magazeti ya Serikali (TSN), Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Shirika la Posta Tanzania (TPC), Tume ya TEHAMA (ICTC) na Baraza la Watumiaji wa Huduma za Mawasiliano (TCRA-CCC).

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,

Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.