Na Raya Hamad – OMKR 06/10/2021. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak amehimiza mashirikiano katika kutekeleza majukumu ya kazi jambo ambalo litasaidia kutoa maamuzi sahihi ya kiutendaji hasa kwenye masuala yanayohusu ukaguzi wa hesabu za ndani
Dkt Omar D. Shajak ameyasema hayo wakati akizindua
kamati ya Ukaguzi wa ndani ya Ofisi hio iliyofuatiwa na mafunzo kwa wajumbe
hao, kwenye ukumbi wa mkutano wa Migombani na kuwataka wajumbe wa kamati hiyo
kuhakikisha wanatoa ushauri unaofaa kwenye masuala ya matumizi ya fedha
Amewakumbusha wajumbe hao kuwa lengo la kuundwa kwa
kamati hiyo ni kuzipitia kwa kina na kuzifanyia kazi hoja zitakazojitokeza
kwenye taarifa ya mkaguzi na kufanya maamuzi sahihi ya taarifa hio kwa vile
moja kati ya jukumu lao ni kumshauri msimamizi mkuu wa fedha ndani ya Ofisi ya
Makamu wa Kwanza wa Rais
Dkt Shajak amesema Kamati ya ukaguzi imeundwa kisheria
ili kuhakikisha matumizi yote yanafanyika kama ilivyokusudia “nyinyi mtasaidia
kunyoosha utaratibu na kama kuna dosari muweze kuzianisha ili kuepusha kukiuka
taratibu zilizowekwa” alisisitiza Dkt Shajak
Aidha amewasisitiza fedha ya serikali inatakiwa
kutumika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa ili kuepusha matumizi yaliyo nje na
utaratibu pamoja na kuhakikisha hoja zitakazoibuliwa na mkaguzi wa ndani
zinapatiwa ufumbuzi wa haraka
Akitoa sifa za mjumbe wa Kamati ya Ukaguzi mkufunzi wa
mafunzo Bi Safia Zubeir kutoka Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi amesema
wajumbe wa Kamati ya ukaguzi ili waweze kufanya kazi vyema na kutoa maamuzi sahihi
anatakiwa kuwa muadilifu, muwajibikaji, mwenye uwezo wa kupima na kushauri.
Pia amesema uadilifu unakufanya kuwa mwaminifu na
kuaminika katika majukumu ya kazi, kujali muda mambo ambayo yanasaidia kuifanya
kamati kuwa imara na kuwa tayari muda wote kufanyakazi kwa ajili ya kumsaidia
Katibu Mkuu ili kuwezesha kufanikiwa majukumu na malengo waliyojipangia kwa
wakati
Wajumbe wa Kamati hio wamejifunza maadili ya kazi na majukumu
ya kamati, sifa zake, faida ya kuwepo kamati ya ukaguzi na changamoto ambapo
mkufunzi huyo amesisitiza haja ya wajumbe wa kamati hio kujengewa uwezo ili
kuelewa vyema majukumu yao na kuyatekeleza kitaalamu zaidi
Kwa upande wake Mkaguzi wa ndani wa Ofisi ya Makamu wa
Kwanza wa Rais Bi Maryam Rajab Baraka na kwa niaba ya kamati hio ametoa
shukurani kwa Katibu mkuu kufuatia kuunda kamati ambayo ipo kwa mujibu wa
utaratibu wa sheria.
No comments:
Post a Comment