Habari za Punde

MAJALIWA: RAIS SAMIA ATOA SHILINGI BILIONI 16 KUBORESHA MIUNDOMBINU YA ELIMU LINDI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya shilingi bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali ya elimu mkoani Lindi.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Oktoba 5, 2021) wakati akizungumza na wananchi, madiwani na wananchi wa Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika mkoa huo.

Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kutoa wito kwa watumishi wa mkoa huo wahakikishe kuwa fedha hizo zinatumika katika kazi iliyokusudiwa na asitokee mtumishi hata mmoja kuzitamani kwani zitamuunguza.

Waziri Mkuu amesema watumishi hao wanawajibu mkubwa wa kuwatumia Wana-Mtama na kwamba Serikali inataka kuona mabadiliko makubwa ya kiutendaji katika maeneo yao. “Tunahitaji kuona wananchi wakiendelea kuhudumiwa.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa amesema watumishi wa halmashauri hiyo wanatakiwa kubuni vyanzo vipya vya mapato ili kuiwezesha iwe na makusanyo ya kutosha na wahakikishe fedha zote zitakazopatikana zinaingia kwenye mfumo sahihi.

“…Halmashauri hii hatuna mapato mengi lakini pale kwenye kituo chetu cha mabasi fedha haziingi kwenye mfuko sahihi. Mkurugenzi fanya mabadiliko pale kwa kuwaondoa watu wote na kuwapeleka wengine ambao ni waaminifu ili fedha zinazopatikana pale ziingie katika mfuko wa halmashauri.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amemuagiza Mweka Hazina wa Halmashauri hiyo, Aisha Msangi afanye maboresho katika maeneo yote ya makusanyo na ahakikishe fedha zote zinazokusanywa zinaingia katika mfuko wa halmashauri na si vinginevyo.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amekagua ujenzi wa tanki la kusambaza huduma ya maji na kuzungumza na wananchi katika eneo la Mitwero Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, ambapo amesema Serikali itahakikisha wananchi wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Manispaa ya Lindi (LUWASA), Mhandisi Juma Soud amesema mradi huo wa maji wa Mitwero ambao unagharimu shilingi bilioni 2.9 unatarajiwa kunufaisha wananchi wapato 40,000 baada ya kukamilika.

 

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

JUMANNE, OKTOBA 5, 2021.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.