Habari za Punde

Watendaji Tume ya Kitaifa Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya watakiwa kudumisha nidhamu

Mkurugenzi Mtendaji Tume Ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za kulevya Kanal Burhani  Z. Nassor  akimkaribisha Katibu Mkuu OMKR, Dkt Omar D. Shajak kuzungumza na wafanyakazi wa Tume hiyo ofisini kwao Migombani. 
Picha Na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais

Na Raya Hamad – OMKR

Watendaji na wafanyakazi wa Tume ya Kitaifa Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya wametakiwa kudumisha nidhamu katika maeneo yao ya kazi na kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa ufanisi

Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais Dkt Omar D. Shajak ameyasema hayo kwenye kikao cha watendaji na wafanyakazi wa Tume hio ikiwa ni mfululizo wa ziara zake katika kutembelea taasisi zinazosimamiwa na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais

Amewakumbusha watendaji na wafanyakazi hao kusimamia vyema majukumu yao kama yalivyoelekezwa kwenye mpango wa majukumu ya kazi waliopewa na kuacha kufanya kazi kwa mazoea ikiwemo uingiaji kazini na utokaji wa kazini

Dkt Shajak amesema mapambano ya Dawa za kulevya yanaanzia ofisini hivyo wanawajibu wa kutunza siri, kuwa waadilifu, watiifu na wazalendo katika kuitumikia Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ambayo imewaamini na kuwaweka walipo

Amesema mapambano ya dawa za kulevya hayatakwisha iwapo hakutakuwa na mashirikiano yanayoanzia ndani ya taasisi yenyewe hivyo ni wajibu wa kila mmoja kuchukuwa tahadhari katika mapambano haya kwani ni vita ya wenye fedha wanaongalia maslahi yao pekee

“isije kufika mahali ukajiona wewe ndio mtoa habari za ndani hatutamuonea mtu muhali na iwapo mtu anaona hawezi kutunza siri haendani na sheria na taratibu za Tume hii ambayo inaelekea kuwa Mamlaka kamili basi mapema ajisalimishe milango iko wazi mapambano ya dawa za kulevya ni yetu sote hakuna aliyekuwa hajaguswa kuanzia mtumiaji mwenyewe, si wazazi, walezi , familia na hata majirani wote tunaathirika wizi umekithiri na mambo mengine yasiyo na maadili”

Katibu Dkt amewaahidi wafanyakazi hao kuwa Serikali inatambua changamoto zao na zinafanyiwa kazi kwa hatua ikiwemo ufinyu wa ofisi na uhaba wa wafanyakazi kwani ni masuala ya kiutawala

Mkurugenzi Mkuu Tume ya Kitaifa ya Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya Kanal Burhani Z. Nassor amesema Serikali ya Mapinduzi Zanziba kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais tayari imeshaandaa mswaada wa sheria na unasubiri Baraka za Serikali ili Tume hio iwe na hadhi ya kuwa Mamlaka kamili

Mamlaka ambayo itakuwa na uwezo wa Kisheria wa kuchunguza, kukamata, kupeleleza na kupeleka kesi Mahakamani ambapo sasa Tume inafanya kazi za Kuratibu na Udhibiti wa Dawa za Kulevya kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama

Aidha Kanal Burhan amesema Tume imejipanga vyema kulishughulikia na kudhibiti  uingizwaji wa dawa za kulevya na ameiomba jamii kutoa mashirikiano kwa kuwafichuwa wanaojihusisha na dawa za kulevya ambapo ameahidi Tume kutoa ushirikiano kwa kudhibiti siri za mtoa habari

“Jamii ikithubutu kushirikiana na kubadilisha mifumo ya maisha ambayo tunaishi ya usasa ni wazi suala la matumizi ya madawa ya kulevya hapa kwetu litakuwa ni historia, nawaomba wazazi na walezi pia muwe wadadisi wa watoto wenu na kufatilia mwenendo wao, mtoto anakuja na vespa au pikipiki mzazi huulizi anarudi usiku huulizi anavitoa wapi vitu vya thamani hizi ni dalili mbaya na turudi kwenye malezi ya asili”alisisitiza Kanal Burhani

Ziara na ya Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais ni muendelezo na utaratibu uliopangwa ili kuona utekelezaji kwa vitendo wa majukumu ya taasisi zinazosimamiwa na Ofisi hio zikiwemo Baraza la Taifa la Watu wenye Ulemavu, Tume ya UKIMWI, Mamlaka ya Usimamizi wa Mazingira na Idara ya Mazingira na Afisi kuu Pemba.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.