Habari za Punde

Kongamano la kupambana na na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto lafanyika Golden Tulip

Wajasirimali kutoka Jumuiya ya watu wenye ulemavu Zanzibar wakimapatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wakati alipotembelea banda lao la maonesho katika maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji zilizofanyika katika Hoteli ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.

Mhe. Hemed akipata ufafanuzi kutoka kwa mjasiriamali juu ya hatua zinazochukuliwa katika uzalishaji wa bidhaa mbali mbali.
Washiriki wa Maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi ambapo Mhe. Hemed alimuakilisha Rais Dk. Mwinyi katika maadhimisho hayo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na washiriki waliohudhuria katika Maadhimisho ya siku 16 za kupinga udhalilishaji yaliofanyika katika Ukumbi wa Golden Tulip Uwanja wa Ndege


Na Kassim Abdi, OMPR

Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema pamoja na jitihada mbali mbali zinazoendelea kuchukuliwa bado vitendo vya udhalilishaji vinaendelea kuwa jambo la aibu Nchini.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla alieleza hayo kupitia hotuba aliosoma kwa niaba ya Rais Dk. Mwinyi katika ufunguzi wa Kongamano la maadhimisho ya siku 16 za kupambana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto lililofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip Uwanja wa Ndege.

Alisema vitendo hivyo vimekuwa vikiendelea kutokea kupitia sura tofauti ikiwemo kupigwa kwa wanawake, kutelekezwa kwa watoto, talaka zisizofuata utaratibu, ndoa za umri mdogo, sambamba na ushirikishwaji wa watoto wenye umri mdogo katika biashara zisizokuwa rasmi.

Mhe. Hemed alileza kuwa, ni jambo la kushangaza katika jamii ya leo kwa baadhi ya wazazi kuacha majukumu yao ya msingi ya malezi na ulinzi wa familia hatimae kujiingiza katika vitendo vya udhalilishaji jambo ambalo linaashiria ukatili uliokithiri kwa wazazi wenye mila na desturi za kistarabu kuwafanyia watoto.

Alisema kuna kila sababu kwa wazazi wenye tabia hizo kuacha mara moja ili watoto waondokane na kadhia hiyo inayowakumba siku hadi siku na kuwanyima furaha na Amani katika maisha yao yote.

Aidha, aliwataka wazazi na walezi kubadilika kulingana na wakati katika kuangalia kwa kina malezi ya watoto kwa lengo la kuwawezesha watoto kupambanua mambo yanayofaa na yasiofaa huku akitolea mfano kitendo cha wazazi kuwaacha watoto nyumbani pekee yao na wao kujikita katika shughuli nyengine na kuacha jukumu lao la malezi.

“ Ndugu wazazi na walezi Ulezi wa namna hii umeshapitwa na wakati , Ulezi kama huu unatoa fursa kwa wahalifu kufanya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto wetu” Alisema Mhe. Hemed

Makamu wa Pili wa Rais alibainisha kwamba, kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya mtakwimu mkuu wa serikali zinaonesha kuwa vitendo vya udhalilishaji vimekuwa vikiripotiwa katika wilaya zote za Zanzibar ambapo wilaya za Mkoa wa Mjini Magharibi zinaongoza kuwa na idadi kubwa ya vitendo hivyo.

Alieleza kwa Kipindi cha mwezi Januari hadi Septemba 2021, jumla ya matukio ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia ni Mia tisa na ishirini na nane (928) ikiwa wanawake 126 na watoto 802 yameripotiwa ambapo wilaya ya Magharibi “A” ina idadi kubwa ya matukio ukilinganisha na wilaya nyengine kwa kuwa na matukio mia mbili na thelasini na tisa (239) ikifuatiwa na wilaya ya Magharibi “B” matukio mia moja na arubaini na saba (147) na wilaya ya Mjini matukio Mia moja na ishirini na Saba (127).

Mhe. Hemed alibainisha matukio hayo yanajumuisha kubakwa Mia nne na sitini na nane (468), kulawitiwa mia moja na arubaini (140), kuingiliwa kinyume na maumbile ni hamsini na mbili (52), kutorosha sabiini na tisa (79), shambulio la aibu thamanini na nane (88) na shabulio ni mia na sita (106).

Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau imendelea kuchukua jitihada mbali mbali kukabiliana na vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kuweka mahakama maalum ya kushughulikia kesi za udhalilishaji na kuongeza mahakimu ili kupunguza mlimbikizano wa kesi ambao ulikuwa ni kilio kikubwa kwa wananchi.  

Alisema tangu kuanzishwa kwa mahakama hiyo jumla ya kesi mia tatu arubaini na tano (345) zimeripotiwa kuanzia mwezi Febuari 2021 hadi Oktoba 2021 na kesi 78 zimepatiwa maamuzi na kueleza kuwa kupitia mahakama hiyo kesi zimekuwa zikichukua muda mchache kupatiwa hukumu na bado serikali inaendelea na msimamo wake wa kuhakikisha kuwa kesi hizo hazina dhamana hali ambayo inawajengea hofu wahalifu wa vitendo hivo.

“Wizara na taasisi mbali mbali wakiwemo viongozi wa Dini na wanaharakati wanaendelea kutoa taaluma kuhusu athari za vitendo hivi pamoja na kukuza uwelewa kwa jamii ili wawe na muamko wa kuripoti matukio ya udhalilishaji yanapotokea katika taasisi husika” Alieleza Makamu wa Pili wa Rais

Katika hatua nyengine Makamu wa Pili wa Rais alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote wakiwemo UNFPA,UN Women, UNICEF, Save the Children,IMO,UNDP na UNESCO kwa jihudi zao wanazozichukua ambazo kwa kiasi kikubwa zimesaidia kupiga hatua katika kupambana na tatizo la udhalilishaji Nchini.

Nae Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Jinsia Wazee na Watoto Mhe. Nassor Ahmed Mazrui alisema lengo la kuwepo kwa maadhimisho ya hayo ni kufanya kutathmini na kujadili juhudi za wadau mbali mbali juu ya masuala ya udhalilishaji na ukatili wa kijinsia pamoja na kupanga mikakati thabiti itakayoweza kutoa muongozo juu ya kupunguza matendo hayo.

Mhe. Mazrui alieleza kuwa kuwepo kwa maadhimisho hayo ni matunda ya mkutano uliofanyika nchini Colombia mwaka 1981 jijini Mogota ambapo dhamira kuu ni kujadili kwa pampja mataifa mbali mbali namna bora ya kupunguza vitendo vya udhalilishaji Duniani.

Akitoa salamu za mashirika ya Umoja wa Mataifa Bibi Jackline Mahon alisema Umoja wa Mataifa unaungana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupinga vitendo vya udhalilishaji kwa kuzingatia dira ya kupunguza umasikini ya mwaka 2050.

Katika hatua nyengine Bibi Jackline aliipongeza SMZ kwa juhudi zake hasa kutenda haki kwa waathirika wa vitendo vya udhalilishaji ikiwemo kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi za udhalilishaji hatua ambayo inarahisisha uendeshaji wa kesi hizo.

Mapema, Makamu wa Pili wa Rais ametembelea maonesho ya wajasiriamali pamoja na kugua shuhuli mbali mbali zinazofanywa na Idara za wizara ya Afya.

Kauli mbiu ya mwaka huu Tuimarishe Amani  Zanzibar, Tumalize Vitendo vya ukatili na udhalilishaji sasa.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.