STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE OF THE PRESS SECRETARY
PRESS RELEASE
Zanzibar 23.11.2021
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Hussein Ali Mwinyi amesema kuwa hatua za
makusudi zinapaswa kuchukuliwa ili kuzuia na kupunguza madhara yatokanayo na
maafa, ingawa ni vigumu kuzuilika moja kwa moja.
Rais Dk. Mwinyi
ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa nyumba za maafa katika kijiji cha Nungwi
kiliopo Mkoa wa Kaskazini Unguja pamoja na zile zilioko Tumbe Mkoa wa Kaskazini
Pemba zilivyojengwa kwa ajili ya wananchi walioathiriwa na mvua za masika za
mwaka 2017, ambapo hafla ya uzinduzi huo ilifanyika huko Nungwi Mkoa wa
Kaskazini Unguja.
Katika maelezo
yake, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa miongoni mwa hatua zinazopaswa kuchukuliwa
ni kuendeleza mipango miji, ambayo inabainisha sehemu za ujenzi wa makaazi,
sehemu za mabonde zisizopaswa kujengwa, maeneo ya kilimo, maeneo ya ujenzi wa
miundombinu ya barabara na maeneo ya huduma za jamii.
“Ni vyema
tukahakaikisha kwamba, tunakuwa na Master plan ya kila mji tunaoujenga ili
kuweka mifumo na taratibu nzuri za kupambana na maafa” alisema Rais Dk. Mwinyi.
Aidha, Rais Dk.
Mwinyi alieleza kuwa ujenzi wa nyumba hizo umelenga kuimarisha maisha ya
wananchi baada ya kupatwa na maafa.
Rais Dk. Mwinyi alisema
kuwa maafa na majanga yamekuwa yakijitokeza katika nchi zote duniani kwa namna
mbali mbali ambapo hakuna hata nchi moja iliyoweza kuwa na teknolojia ya kuzuia
majanga na maafa yasitokee.
Alisema kuwa hata
nchi zilizoendelea hupata taharuki kubwa pale zinapokumbwa na maafa kama vile
Vimbunga, Sunami, Matetemeko ya ardhi, Mafuriko, Moto na mengineyo.
Alisisitiza kwamba
yanapotokea majanga na maafa ya aina hiyo, baadhi ya wakati hata nchi
zilizoendela nazo huomba misaada, ili kuhami wananchi wake ambapo kwa lengo la
kujikinga au kupunguza athari za maafa nchi nyingi duniani hivi sasa zimekuwa
na mifumo ya utabiri na tahadhari dhidi ya maafa na kuanzisha taasisi na sheria
za maafa.
Kwa upande wa
Zanzibar, Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua zinaendelea kuchukuliwa ikiwa ni pamoja
na kuanzisha Kamisheni ya kukabiliana na maafa kwa lengo la kupunguza athari za
maafa kwa maisha ya watu na mali zao kwa kuchukua hatua madhubuti za kujikinga,
kujitayarisha, kukabiliana na kurudisha hali ya kawaida ya maisha ya wananchi
baada ya maafa kutokea.
Aliongeza kuwa
Kikosi cha Zimamoto pamoja na Kikosi cha Uokozi Zanzibar vimepewa mafunzo
maalum ya kukabiliana na kutoa misaada wakati wa maafa sambamba na kuwepo kwa
mifumo ya utabiri wa hali ya hewa inayosimamiwa na Mamlaka ya Hali ya Hewa
Tanzania ambayo ni taasisi ya Muungano.
Pamoja na hayo,
Rais Dk. Mwinyi aliwahimiza wananchi waliobahatika kupewa nyumba hizo wazitunze
vizuri, wadumishe usafi katika eneo lote hilo na waishi kwa kuzingatia misingi
ya upendo, udugu na ujirani mwema.
Rais Dk. Mwinyi
alitoa shukurani kwa Ofisi ya Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu nchini
Tanzania na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na Balozi Khalifa Abdulrahman
Almarzouqi, Balozi wa (UAE) nchini pia, alitoa shukurani kwa Meneja wa Mradi
huo kwa kazi nzuri aliyoifanya pamoja na kumpongeza Mshauri elekezi na Mkandarasi
kwa kufanikisha mradi huo.
Sambamba na hayo,
Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi wa kijiji cha Nungwi azma ya Serikali
anayoiongoza katika kuwaondoshea changamoto iliyopo na kuwapelekea huduma
muhimu ya maji safi na salama pamoja na ujenzi wa barabara za ndani katika
kijiji hicho.
Nae Kaimu Waziri
wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi
Saada Mkuya alisema kuwa jumla ya
familia 54 ambazo zinaidadi ya watu 261 kwa Unguja na Pemba wanaishi katika
vijiji hivyo ambapo pia, wanafunzi wa
Maandalizi na Msingi 277 wanasoma katika vijiji hivyo wakiwemo 151
Nungwi na 126 Tumbe.
Alisema kuwa kwa
upande wa vituo vya afya tokea vifunguliwe tayari wananchi 954 wamepatiwa
matibabu na huduma mbali mbali za kiafya wakiwemo 230 Tumbe na 724 Nungwi
ambapo pia, kuna msikiti ambao unachukua waumini 200 ambao unahusisha sehemu ya
kusalia kwa akina mama.
Waziri Mkuya alisema
kuwa wananchi waliopata nyumba hizo kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja wanatoka katika
Shehia za Gamba, Mkwajuni Kidombo na Mkadini na kwa upande wa nyumba za Tumbe wanatoka
katika Shehia ya Mtemani, Tumbe Mashariki, Tumbe Magharibi, Mtemani, Timba,
Kipange na Shumba viamboni na Wingwi Mapofu na hakuna mtu aliyekuwa hausiki
ambaye amepewa nyumba hizo.
Naibu Katibu Mkuu
wa Mwezi Mwekundu alieleza jinsi taasisi hiyo ilivyofarajika katika kuunga mkono
juhudi hizo za Serikali pamoja na kuwataja viongozi wakuu wa (UEA) ambao nao
wameonesha kuunga mkono juhudi hizo.
Mapema Katibu Mkuu
wa Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Sera, Uratibu na Baraza la Wawakilishi
Thabit Idarous Faina alisema kuwa ujenzi wa nyumba hizo unatokana na athari za
mvua za masika zilizonyesha mwaka 2017 ambapo nyumba zipatazo 6005 ziliathirika
Unguja na Pemba.
Alisema kwamba hali
hiyo ndio ilipelekea taasisi ya Mwezi Mwekundu kutoka Falme za Kiarabu (UAE)
kujitokeza kusaidia juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar za kunusuru maisha
ya wananchi kwa kujenga makaazi bora na yalio salama ambapo jumla ya nyumba 15
zenye kuishi familia 30, kituo cha afya, skuli, maabara, msikiti na maduka 15
vyote vimejengwa katika vijiji vya Nungwi na Tumbe kisiwani Pemba.
Kitengo cha Habari
Ikulu Zanzibar.
No comments:
Post a Comment