Habari za Punde

Rais Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Wananchi wa Uzini Katika Sala ya Ijumaa na Kumuombea Dua Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban..

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi  akizungumza na kuwasalimia Wananchi wa Uzini baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Uzini leo. 

Wananchi wa Uzini Wilaya ya Kati Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa ilioyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Uzini leo.
Wananchi wa Uzini Wilaya ya Kati Unguja wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na kuwasalimia baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa ilioyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Uzini leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua baada ya kumalizika kwa Ibada ya Sala ya Ijumaa iliyofanyika katika Msikiti wa Ijumaa Uzini Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja. 


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amesema ugonjwa wa UVIKO-19 ulioikumba Dunia  mbali ya kuathiri kiafya lakini umesababisha matatizo makubwa ya kiuchumi.

Alhaj Dk. Mwinyi amesema hayo wakati alipozungumza na waumini wa dini ya Kiislamu wa kijiji cha Uzini pamoja na vitiongoji vyake, mara baada ya kukamilisha Ibada ya Sala ya Ijumaa, iliofanyika katika Msikiti Mkuu wa Ijumaa Uzini, Wilaya ya Kati, Mkoa Kusini Unguja.

Amesema ugonjwa wa UVIKO 19 umesababisha baadhi ya nchi kufunga mipaka yao pamoja na kusimamisha shughuli za uzalishaji katika sekta mbali mbali za viwanda na hivyo kusababisha kupanda kwa gharama za bidhaa pamoja na gharama za usafirishaji.

Katika salamu zake kwa waumini wa kijiji hicho, Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa ugonjwa huo umeathiri jamii kiafya na kiuchumi, hivyo akawataka waumini kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu  ili kuliondoa janga hilo.

Alhaj Dk. Mwinyi aligusia kuwepo kwa matukio mbali mbali yanayoiathiri jamii hapa nchini, ikiwemo vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia na kubainisha hatua mbali mbali zinazochukuliwa na Serikali katika  kukabiliana na vitendo hivyo ikiwemo kutunga sheria kali kwa washtakiwa.

Aidha, Alhaj Dk. Mwinyi alikubali ombi la wananchi wa kijiji cha Uzini la kuifanyia matengenezo  barabara yao inayoingia ndani kuelekea msikiti mkuu wa Ijumaa Uzini.

Alisema barabara hiyo itaingizwa katika mpango wa matengenezo ya  barabara za ndani  zenye jumla ya urefu wa kilomita 270 zitakazojengwa kwa kiwango cha lami na  hivyo, akawataka waumini hao kuielimisha jamii juu ya muhimu wa kujenga nyumba zao masafa marefu kando ya barabara, ili kuipesha Serikali na gharama za ulipaji wa fidia.

Nae, Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khalid Ali Mfaume alimpongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi kwa utaratibu aliojiwekea wa kuungana na waumini kupitia Ibada za  sala za Ijumaa katika misikiti mbali mbali Mjini na Vijijini.

Alisema utaratibu huo unampa fursa ya kuonana na wananchi na kusikia changamoto mbali mbali zinazowakabili wananchi.

Mapema, Khatibu wa Msikiti Mkuu wa Ijumaa Uzini Maalim Ali Vuai alisisitiza wajibu wa waumini kutekeleza Ibada ya sala tano, kuambatana na masharti yake, ikiwemo wakati.

Alisema Sala ni miongoni mwa Ibada kubwa  na akabainisha kauli ya Mtume Muhammad (SAW) juu ya utekelezaji wa ibada hiyo kuwa ndio nguzo kubwa ya Dini ya Kiislamu na kusema kwa yule ataeiacha atakuwa amevunja dini hiyo.

Aidha, Maalim Vuai alimuomba Mwenyezi Mungu kuijaalia Zanzibar kuwa nchi ya amani pamoja na kuondokana na matatizo mbali mbali, ikiwemo ya udhalilishaji wa kijinsia, rushwa pamoja na  matumizi ya dawa za kulevya.   

Wakati huo huo, Alhaj Dk. Mwinyi mara baada ya salamu zake hizo aliungana na viongozi wengine wakiwemo wa msikiti huo katika dua maalum ya kuwaombea marehemu waliozikwa pembezoni mwa msikiti huo akiwemo mwanasiasa maarufu Marehemu Ramadhan Abdalla Shaaban.

                                                                  

Imetayarishwa na Kitengo cha habari,

Ikulu Zanzibar.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.