Habari za Punde

Uzinduzi wa maonyesho ya biashara kufanyika kesho viwanja vya Maisara

Na Khadija Khamis – Maelezo Zanzibar .05/12/2021.

Katibu Mkuu Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda Islam Seif Salum amesema maonesho ya sita ya viwanda vya Tanzania yanatarajiwa kufunguliwa kesho,Maisara.

Mgeni Rasmi wa Uzinduzi wa Maonesho hayo anatarajiwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla .

Hayo ameyasema huko Maisara wakati akizungumza na Waandishi wa Habari wa vyombo mbali mbali jinsi ya shughuli za maonesho ya bidhaa mbali mbali zinavyoendelea.

Amesema maonesho haya ni ya mara ya kwanza kufanyika hapa Zanzibar tokea kuanzishwa kwake mwaka 2016, kufanyika kwake ni kwa umuhimu wa pekee katika Maadhimisho ya  miaka 60 ya Uhuru wa Tanganyika .

Amewataka Wazanzibar na Watanzania kwa ujumla kuitumia fursa hii ya kupata bidhaa zenye uhalisia wa kitanzania ambazo ziko katika kiwango bora na zinazokidhi masoko .

Nae Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE)  Latifa Mohamed Khamis amesema maonyesho haya yatasaidia kuongeza ushindani wa kibiashara ambao utazalisha bidhaa zenye ubora katika Makampuni mbali mbali pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo

Amesema Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania ni kitovu cha ufanisi katika kuendeleza na kukuza uchumi wa nchi kupitia biashara .

Ameeleza dhima ya mamlaka hiyo ni kuwezesha ukuwaji wa uchumi wa Tanzania kwa kuendeleza pamoja na kukuza bidhaa na huduma mbali mbali kwa masoko ya ndani na nje ya nchi

Hata hivyo alisema mamlaka hiyo inawajengea uwezo na kuwaendeleza wazalishaji ikiwemo wajasiriamali wadogo wadogo kwa kuwapa mafunzo, klinik za biashara na huduma za ushauri kwa jamii na wafanyabiashara  na hasa wazalishaji wadogo ili waweze kushindana katika masoko ya ndani na kanda ya kimataifa

Jumla ya kampuni 113 zimeshiriki katika maonesho ya bidhaa mbalimbali pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo  ambayo wanauza bidhaa zao kuanzia tarehe tatu hadi tisa na Uzinduzi Rasmi unatarajiwa kufanyika kesho .

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.