Habari za Punde

Zantel yazindua duka jipya lililopo Michenzani Mall-Unguja. Mkuu wa Wilaya aipongeza kwa kuboresha huduma za Mawasiliano Unguja.

Mkuu wa Wilaya ya Mjini-Unguja, Rashid Msaraka akikata utepe kuzindua duka jipya la Zantel lililopo eneo la biashara la Michenzani Mall.Kulia ni Mkuu wa Zantel-Zanzibar Mohammed Khamis Mussa na Emmanuel Joshua, Mkuu wa Mauzo, Usambazaji na Huduma kwa wateja.Duka hilo ni la tatu kwa Unguja na la tano kwa Zanzibar litakalosaidia kusogeza huduma karibu na wateja.


Katika kuhakikisha wateja wanapata huduma kwa urahisi, Kampuni ya Zantel imezindua duka jipya la huduma kwa wateja lililopo michenzania Mall mjini unguja.

Uzinduzi wa duka hilo ulifanyika jana na Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Msaraka na kushuhudiwa na wadau mbalimbali.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mkuu wa Zantel-Zanzibar Mohammed Khamis Mussa alisema duka hilo litasaidia kuongeza huduma za mawasiliano karibu na wateja kwani duka hilo lipo katikati ya mji.

“Duka hili litakuwa msaada mkubwa katika kuongeza kasi ya utoaji huduma kwa wateja wetu hapa Unguja.Eneo hili la Michenzani ni rahisi zaidi kufikika kwa wateja wote wa maeneo ya karibu na wanaotembelea eneo hili,” alisema Mussa.

Duka hilo ni la tatu kwa Unguja ambapo mawili yapo maeneo ya Vuga na Mlandege.Pia, duka hilo ni la tano kwa Zanzibar ambapo mawili mengine yapo Pemba katika eneo la Chake na Wete.

 Mkuu wa Wilaya ya Mjini, Rashid Msaraka aliipongeza Zantel kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuhakikisha inaboresha huduma za mawasiliano visiwani Zanzibar.

 “Huduma za Mawasiliano ni kiungo muhimu katika kuchochea ukuaji wa uchumi wa nchi yetu.Zantel imekuwa mfano bora katika kuboresha huduma za mawasiliano kwa kujenga miundombinu kama minara pamoja na maduka kama hili tunalozindua leo,” alisema

Zantel imekuwa ikifanya uwekezaji mkubwa katika kujenga miundimbinu mipya na kuboresha iliyopo ili kuhakikisha Zanzibar yote inakuwa na Mawasiliano ya uhakika.

Hadi mwaka huu, zaidi ya asilimia 65 ya Zanzibar ilikuwa imeunganishwa na mtandao wa 4G jambo linalotoa fursa kwa wananchi kupata na kuzitumia fursa za kiuchumi na kijamii kwenye ulimwengu wa kidigitali.

Hivi karibuni, Kampuni hiyo imekuwa ikiendesha kampeni ijulikanayo kama Pasua Anga Ki Zantel 4G ambayo ililenga kuelimisha umma juu ya umuhimu wa mtandao wa 4G kwa manufaa ya kijamii na kiuchumi.

 “Tumeona mabadiliko chanya kupitia kampeni hii, ambapo tumeona watu wakianza kutumia mtandao kwa manufaa yao.Wapo waliofungua biashara mitandaoni na kuongeza ubunifu kwenye kazi zao kwa kutumia intaneti,” alisema Mussa.

Huduma zitakazopatikana kwenye duka hilo ni pamoja na usajili wa namba za simu, bidhaa za simu kamavile Smarta, huduma za 4G pamoja na huduma ya kifedha ya Ezypesa.

Uzinduzi wa duka hilo umekuja mara tu baada ya kufunguliwa kwa maduka (mall) ikiwa ni fursa kwa kampuni mbalimbali kusogeza huduma karibu na wateja wao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.