Habari za Punde

Mhe Hemed ataka mashirikiano ili malengo ya Mapinduzi Cup yafanikiwe

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Iman Duwe wakati uongozi huo ulipofika Afisini kwake Vuga kwa ajili ya kubadilishana nae mawazo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla akizungumza na Uongozi wa Kamati ya Kombe la Mapinduzi ikiongozwa na Mwenyekiti wake Iman Duwe wakati uongozi huo ulipofika Afisini kwake Vuga kwa ajili ya kubadilishana nae mawazo.
 

Na Kassim Abdi, OMPR

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ameiagiza Kamati ya Kombe la Mapinduzi (MAPINDUZI CUP) kufanya kazi kwa Kushirikiana kwa karibu na uongozi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa lengo kutoa ufanisi na kufikia malengo yaliokusudiwa.

Mhe. Hemed alieleza hayo wakati alipokutana na kamati hiyo Afisini kwake Vuga kwa ajili ya kubadilishana nae mawazo juu mashindano yanayoendelea.

Alisema  mashindano ya kombe la Mapinduzi kwa muda mrefu sasa yamekuwa yakiiletea heshima Zanzibar na Tanzania kwa Ujumla kutokana na kushirikisha timu kutoka pande zote mbili za Muungano.

Alifafanua kuwa, wasimamizi wa mashindano hayo wana jukumu la kuhakikisha wanayasimamia mashindano hayo kwa uwadilifu na uaminifu mkubwa katika kuhakikisha yanatoa tija kwa taifa.

Katika hatua nyengine, Makamu wa Pili wa Rais alimuagiza Mwenyekiti wa kamati ya mashindano hayo kuondosha muhali sambamba na kuwa na maamuzi ya pamoja yatakayosaidia kufanikisha mashindano.

Nae, Mwenyekiti wa Mashindano hayo Imane Duwe alimuahidi Makamu wa Pili wa Rais kuwa Kamati anayoisimamia itafanya kazi zake kwa uwangalifu na umakini mkubwa ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Alieleza kuwa, Kamati hiyo itahakikisha inalinda heshima ya serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuinua matarajio ya wazanzibar kwa upande wa sekta ya michezo.

Kwa Upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Fatma Hamad Rajab alimuhakikishia Mhe. Hemed kuwa wizara ya habari itashirikiana kwa karibu na Kamati hiyo kwa lengo la kufanikisha azma iliokusudiwa.

Mashindano hayo ya kombe la Mapinduzi yalianza kutimua vumbi jana kwa kuzikutanisha timu ya Meli Nne City na Namungo kutoka Mkoani Lindi.

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.