Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi aendelea na ziara yake Falme za Kiarabu ashuhudia utiaji saini mradi mkubwa wa uwekezaji

 

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Hussein Ali Mwinyi ameendelea na ziara yake katika nchi za Falme za Kiarabu.

Baada ya kuwasili Abu Dhabi jana usiku kwa ziara ya siku tatu katika nchi za Falme za Kiarabu, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dokta Hussein Ali Mwinyi leo hii alishuhudia utiaji saini wa miradi mikubwa ya uwekezaji baina ya Serikali ya Zanzibar na Kampuni ya Eagle Hills Regional Properties ya Umoja wa Falme za Kiarabu-UAE  

Kwa upande wa Zanzibar, utiaji saini huo ulifanywa na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar-ZIPA na kwaupande wa Kampuni ya Eagle alikuwa Mheshimiwa Mohammed Ali Rashid Alabar 

Mwekezaji huyo alimueleza Dokta Mwinyi kuridhishwa kwake na mazingira ya uwekezaji Zanzibar tofauti na alivyotembelea mataifa mengine duniani ambako nako amewekeza miradi mikubwa.

Alimshukuru pia Rais Dokta Hussein Mwinyi kwa kumuunga mkono na kuahidi atafanya kila linalowezekana kuhakikisha uwekezaji anaotarajia kuufanya unafanikiwa.

Miradi inayotarajiwa kujengwa na mwekezaji huyo ni Hoteli ya nyota tano eneo la Kizingo ambapo pia mwekezaji huyo anatarajiwa kujenga nyumba Zanzibar kwa ajili ya maeneo ya makaazi.

Vilevile chini ya mradi huo eneo jingine litakalonufaika na uwekezaji huo ni Matemwe Mkoa wa Kaskazini Unguja ambako kutajengwa hoteli yenye hadi ya nyota tano na vilevile nyumba za kuishi zenye hadhi ya juu kwa ajili ya soko la watalii na watu wenye uwezo.

Ziara hii ya Rais ilianza kuonesha dalili nzuri mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Abu Dhabi ambapo baada tu ya kutoka ndani ya ndege mvua ya wastani lianza kunyesha.

Mapema nyakati za asubuhi Rais Dokta Hussein Mwinyi alihudhuria sherehe za kuwatunuku vyeti washindi wa  mpango endelevu wa Abu Dhabi unaojikita kuendeleza masuala ya afya; chakula; nishati; maji na  maendeleo ya elimu duniani sherehe iliyofanyika Dubai.

Rais Dokta Mwinyi katika shughuli nyingine aliyoifanya leo ni kutembelea banda la Tanzania katika maonyesho ya kimataifa ya Dubai yanayojulikana expo 2020.

Rais anaendelea na ziara yake katika nchi za Falme za Kiarabu ziara inayotarajiwa kumalizika Jumatano tarehe 19 Januari.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.