Habari za Punde

Rais Dk Hussein Mwinyi apongeza kurejeshwa mahusiano na ushirikiano kati ya Ujerumani na Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza katika hafla ya Uhuwishaji wa Mahusiano baina ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Ujerumani pamoja na Uzinduzi wa Taasisi ya Maendeleo ya Ujerumani,uliofanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 26-1-2022.(Picha na Ikulu)

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi amepongeza hatua za Serikali ya Ujerumani za kujesha uhusiano na ushirikiano wa kimaendeleo kati yake na Zanzibar.

Rais Dk. Mwinyi aliyasema hayo leo katika salamu zake za shukurani kwa Serikali ya Ujerumani kwa hatua yake ya kurejesha uhusiano na ushirikiano wake na Zanzibar wa muda mrefu utakuwa wa kimaendeleo, uhusiano ambao ulisitishwa na nchi hiyo ya Ujerumani tokea mwaka 2015.

Alisema kuwa kurejesha mashirikiano na uhusiano kati ya Zanzibar na Ujerumani kutaimarisha maendeleo hapa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba nchi hiyo ni mdau mkubwa wa maendeleo ya Zanzibar katika visiwa vyake vyote vya Unguja na Pemba. 

Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Ujerumani ina historia kubwa ya kuunga mkono maendeleo ya Zanzibar na pia, ni nchi ambayo ilianzisha uhusiano wake na kusaidia Zanzibar tokea mwaka 1965 ikiwa ni pamoja na kujenga nyumba za makaazi, maarufu nyumba za Mjerumani zilipo Kikwajuni Mjini Zanzibar, nyumba za maendeleo za Bambi, kusaidia maendeleo ya Mji Mkongwe Zanzibar pamoja na kusaidia huduma mbali mbali za kijamii.

Aidha, Rais Dk. Mwinyi, alisema kuwa kurejesha uhusiano huo wa maendeleo haupo kimaneno badala yake uko kivitendo kwani tayari Ujerumani imeshakusudia kusaidia kuimarisha huduma za kijamii ikiwemo miradi kadhaa ya maendeleo kama vile miradi ya maji, afya, michezo pamoja na kuunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu.

Kwa upande wa sekta ya afya, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa Ujerumani imekusudia kuiunga mkono Zanzibar katika kutoa huduma za bima ya afya kwa wote ambapo utaratibu maalum utawekwa.

Pia, kwa upande wa maji, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua ya nchi hiyo kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya upembuzi yakinifu, kuchimba visima vipya, vyanzo vipya vya maji  pamoja na vifaa kutasaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa huduma hiyo kutokana na kuwepo changamoto katika upatikanaji wake.

Kwa vile Ujerumani imeahidi kuisaida Zanzibar katika sekta ya michezo, Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa hatua hiyo itasaidia kukuza michezo hasa ikifahamika kwamba michezo ni ajira, afya na pia, michezo huondoa vitendo viovu kwa vijana sambamba na kueleza hatua za kuwepo uongozi makini kwenye sekta hiyo.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alitoa shukurani kwa Serikali ya Ujerumani pamoja na Ubalozi wa Ujerumani kwa hatua yake hiyo ya kurejesha upya uhusiano na ushirikiano na Zanzibar hali ambayo itaweza kusaidia katika Mpango wa miaka mitano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Ameeleza kwamba hatua ya Ujerumaini kujitokeza hadharani na kuahidi kurejesha uhusiano na ushirikiano na Zanzibar ni jambo la kupongezwa na kuungwa mkono kwani Zanzibar bado inahitaji wadau wa maendeleo zikiwemo nchi kama Ujerumani pamoja na washirika wengine zikiwemo sekta binafsi.

Nae Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Jamal Kassim kwa upande wake alitoa shukurani kwa Ubalozi wa Ujerumani kwa jinsi ulivyoonesha ushirikiano na hatimae kurejesha uhusiano wake kwa vitendo.

Mapema Balozi wa Ujerumani hapa nchini Regine Hess alieleza kufarajika kwake na hatua hiyo na kusisitiza kwamba nchi yake inaimani kubwa na uongozi wa Rais Dk. Mwinyi pamoja na serikali yake anayoiongoza ya Umoja wa Kitaifa hatua ambayo imepelelea Zanzibar kendelea kuwa na amani na utulivu mkubwa.

Aliahidi kwamba miradi yote iliyoahidiwa na Ujerumani itatekelezwa ipasavyo kwani nchi hiyo ina historia kubwa ya kuisadia Zanzibar katika miradi mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Nao viongozi wandamizi wa Ubalozi wa Ujerumani walieleza azma ya nchi hiyo ya kurejesha uhusiano na ushirikiano na Zanzibar pamoja na kueleza mikakati iliyowekwa na Ujerumani katika kuisaidia Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo maji, afya, michezo, elimu, kuwawezesha wananchi kiuchumi pamoja na kuiunga mkono Dira ya Uchumi wa Buluu.

Rais Dk. Mwinyi pamoja na Balozi Regine Hess walifungua pazia maalum kuonesha ishara ya uzinduzi wa kurejesha ushirikiano na uhusiano huo wa kimaendeleo kati ya Ujerumani na Zanzibar.

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari

Ikulu Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.