Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi Amejumuika na Wananchi Katika Maziko ya Sheha wa Kwahani Marehemu Machano Mwadini Omar Katika Kijiji cha Chaani Masingi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alh Dk.Hussein Akli Mwinyi akijumuika na Wananchi katika kisoma na dua kumuombea Marehemu Mchano Mawadi Omar Sheha wa Kwahani, maziko yaliofanyika Kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na kutowa mkono wa pole kwa Familia ya Marehemu Machano Mwadini Omar  aliyekuwa Sheha wa Kwahani, alipofika Kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akiitikia dua ya kumuombea Marehemu Machano Mwadini Omar , baada ya kutoa mkono wa pole kwa famalia ya marehemu alipofika kijiji kwao Chaani Masingini Mkoa wa Kaskazini Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amejumuika pamoja na wanafamilia, wananchi pamoja na viongozi mbali mbali katika sala na dua ya kumuombea marehemu Mzee Machano Mwadini Omar, Sheha wa Shehia ya Kwahani, huko kijijini kwao Chaani Masingini, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

 

Aidha, Rais Dk. Mwinyi alitumia fursa hiyo kuipa pole familia ya Marehemu Mzee Machano Mwadini Omar mara baada ya kufika kijijini hapo, na kuinasihi familia kuwa na subira katika kipindi hichi cha msiba pamoja na kuendelea kumuombea dua marehemu.

 

Alhaj Dk. Mwinyi alimuelezea Marehemu jinsi alivyomfahamu na jinsi alivyokuwa nae karibu katika kazi wakati akiwa Mbunge wa Jimbo la Kwahani tokea marehemu nae akiwa Diwani na hatimae kuwa Sheha wa Shehia ya Kwahani, nafasi ambayo alikuwa nayo hadi mauti yanamfika.

 

Akitoa pole, Alhaj Dk. Mwinyi alimuomba Mwenyezi Mungu ailaze roho ya  Marehemu Mzee Mwadini Omar mahala pema peponi,  Amin.

 

Mapema, Alhaj Dk. Mwinyi aliungana na waumini wa dini ya Kiislamu katika sala ya Ijumaa katika msikiti wa Mwembenjugu (Masjid Iman), ambapo mara baada ya sala hiyo alitoa salamu kwa waumini na kuwanasihi kuitumia misikiti kwa masuala mbali mbali ya kijamii.

 

Alhaj Dk. Mwinyi alisema kuwa misikiti isitumiwe kwa kusali pekee bali itumike pia kwa masuala ya kijamii ikiwa ni pamoja na kuwasaidia mayatima, wajane, wasiojiweza na kutoa elimu juu ya matumizi ya dawa za kulevya pamoja na kupambana na udhalilishaji.

 

Aliwanasihi waumini kujikinga na mambo mbali mbali katika jamii pamoja na kujikinga katika afya zao ikiwa ni pamoja na kuwa na mfumo mzuri wa kula kama alivyofundisha Mtume Muhammad (S.A.W), kufanya mazoezi huku akisisitiza haja ya kujikinga na maradhi ya UVIKO-19, majanga ambayo mbali ya kuathiri afya pia yameathiri uchumi kwa kiasi kikubwa.

 

Sambamba na hayo, Alhaj Dk. Mwinyi alikubali ombi la uongozi wa msikiti huo la kusaidia ujenzi wa msikiti wao ambao hivi sasa haukidhi haja kutokana na kuwa mdogo, ombi ambalo Alhaj Dk. Mwinyi amelipokea na kuahidi kulifanyia kazi.

 

Imetayarishwa na Kitengo cha Habari,

Ikulu Zanzibar

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.