Habari za Punde

ZECO yasikitishwa na matukio ya wizi wa nyaya za umeme

 

Na Takdir Suweid

Uongozi  wa shirika la umeme Zanzibar (Zeco) umesikitishwa na matukio ya wizi wa nyaya za umeme yaliotokea maeneo mbalimbali katika mwezi huu na kusababisha hasara kubwa kwa shirika hilo na wananchi.


Akizungumza na waandishi wa habari  kuhusiana na kuibiwa nyaya za umeme Afisa Mawasiliano wa shirika hilo, Haji Juma Chapa amesema kwa kipindi cha Januari mwaka huu zaidi ya matukio 5 yametokea katika maeneo mbalimbali.

Amesema matukio hayo ni miongoni mwao hujuma za makusudi zinazofanywa na Watu wasiopenda maendeleo ya zeco na serikali kwa ujumla.

Aidha amewaomba wananchi kufahamu kuwa shirika la umeme ni shirika la serikali hivyo washirikiane na zeco katika kulilinda na kuwatolea ripoti wanaowakuta wakifanya hujuma katika miundombinu ya umeme.


Kwa upande wake Diwani wa wadi ya Bambi, Said Kheir Mtumwa ameuomba uongozi wa Shirika la Umeme Zanzibar kuweka vidhibiti maalumu ili kuweza kuwafahamu waofanya vitendo hivyo na kuwachukulia hatua kwani wanadhorotesha maendeleo ya Wananchi, Wafanyabiashara na Serikali kwa ujumla.

Nao wafanyabiashara na wananchi wa maeneo yalioathirika na hujuma hizo  wamesema wamepata hasara kubwa katika biashara zao na kuiomba serikali kuwachukulia hatua Kali watakaowabaini kuhusika na vitendo hivyo ili iwe fundisho kwao na wengine wenye tabia kama hiyo.

Maeneo yaliofanyiwa uharibifu wa wizi wa nyaya za umeme ni pamoja na   Bumbwisudi na Umbuji ambapo gharama iliopatikana ni  zaidi ya sh.milioni 3 kwa makisio.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.