Habari za Punde

Lukuvi Akabidhi Ofisi kwa Waziri Mpya Mhe.Dkt.Mabula.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akmikabidhiwa nyaraka za makabidhiano ya ofisi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika ofisi ya Wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza wakati wa makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika ofisi ya Wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na Menejiment ya Wizara ya Ardhi wakati wa makabidhiano ya ofisi baina yake na aliyekuwa Waziri wa Ardhi William Lukuvi katika hafla fupi ya makabidhiano ya ofisi iliyofanyika ofisi ya Wizara iliyopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dodoma.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akiagana na aliyekuwa Waziri wizara hiyo ambaye ni Mbunge wa jimbo la Isimani William Lukuvi wakati wa makabidhiano ya ofisi yaliyofanyika ofisi za Wizara zilizopo Mji wa Serikali Mtumba jijini Dar es Salaam.

Na Munir Shemweta, WANMM DODOMA

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi amemkabidhi Ofisi aliyekuwa Naibu wake Dkt Angeline Mabula ambaye sasa ni Waziri wa Wizara hiyo.

Makabidhiano ya ofisi yamefanyika leo tarehe 17 Februari 2022 kwenye ofisi za Wizara hiyo katika mji wa serikali Mtumba jijini Dodoma.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo, Lukuvi alisema ana furaha kubwa kumkabidhi ofisi mtu anayeijua Wizara na aliyekuwa akifanya kazi naye.

‘’ Dkt Angela anayajua mengi kwenye wizara, tumeshirikiana katika kushughulukia dhuluma na malalamiko ya ardhi na katika kipindi chote tumejitahidi kupunguza malalamiko na yamepungua’’. Alisema Mbunge wa jimbo la Isimani

‘’Ninaomba mumpe ushirikiano, nimefanya naye kazi takriban miaka sita na tumeelewana sana na nilimpa kazi nyingi kwa sababu ana uwezo, tofauti yangu mimi na yeye ni kuwa, mimi ni mkali ila yeye ni mpole’’ alisema Lukuvi

Kwa mujibu wa Lukuvi, wakati wa uongozi wao, Wizara ya Ardhi ilipiga hatua kubwa katika masuala mbalimbali yakiwemo mabadiliko ya mfumo wa utunzaji kumbukumbu za ardhi sambamba na uanzishwaji ofisi za ardhi za mikoa.

Ameishukuru Menejiment ya Wizara kwa kuonesha ushirikiano wakati wa kipindi chote alichokuwa Wizara ya Ardhi na kuitaka menejiment hiyo kumpa ushirikiano Waziri wa sasa Dkt Mabula.

Kwa upande wake Dkt Mabula mbali na kumpongeza mhe Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumuamini na kumteua kuwa Waziri wa Ardhi  alimshukuru Lukuvi kwa kumpa uhuru wa kufanya kazi wakati wote alipokuwa wakifanya kazi pamoja.

Alisema, katika kipindi cha uongozi wao, wizara ya ardhi imefanya mambo mengi kwa lengo la kuondoa changamoto za sekta ya ardhi na kubainisha kuwa mafanikio yote yalitokana na ushirikiano na menejiment ya wizara.

‘’Mengi yamefanyika kuondoa changamoto kwa ushirikiano na timu nzima ya Menejiment, umenilea vizuri, malezi na imani uliyokuwa nayo ni wazi nina deni kubwa la kulipa katika utendaji kazi’’

Waziri Dkt Mabula aliongeza kuwa, pamoja na mambo mengine lakini msisitizo wa wizara yake kwa sasa mbali na mambo mengine ni vipaumbele vya rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan katika masuala ya uwekezaji na mifumo ya utunzaji kumbukumbu za ardhi.  

Aliyekuwa Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambaye ni Mbunge wa jimbo la Isimani mkoani Iringa William Lukuvi aliondolewa nafasi ya uwaziri katika mabadiliko ya Baraza la Mawaziri yaliyofanyika mapema januari mwaka huu. Lukuvi aliteuliwa kwa mara ya kwanza nafasi ya uwaziri mwaka 1995 katika iliyokuwa wizara ya kazi na baadaye kuhudumu Ofisi ya Waziri Mkuu na baadaye Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi ambako alidumu kwa miaka 8 tangu mwaka 2014.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.