Habari za Punde

Serikali kuzidi kuliimarisha zao la karafuu

Na Issa Mzee  - Maelezo    03/02/2022.

Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Omar Said Shaaban amesema lengo la Serikali ni kuimarisha zao la karafuu na kuhakikisha uzalishaji wa zao hilo  unaongezeka kwa wingi nchini ili Serikali iendelee kuwanufaisha wananchi kupitia zao hilo.

Alisema karafuu ni biashara kubwa Zanzibar lakini pia ni miongoni mwa kilimo cha biashara ambacho kimeweza kuwanufaisha wananchi kiuchumi na kuengeza pato la serikali.

Alisema hayo katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika ukumbi wa Baraza la Leseni  Malindi Mjini Zanzibar, uliolenga kuwajuulisha wananchi utekelezaji wa mambo mbalimbali ya maendeleo ya Wizara hiyo.

Alieleza kuwa, mafanikio makubwa yamepatikana kupitia Shirika la Taifa la  Biashara  (ZSTC ) mwaka huu ikiwemo kuwalipa wakulima kwa wakati na kununua karafuu kwa bei nzuri licha ya kuwa bei ya karafuu ilishuka katika soko la dunia.

Akizungumza kuhusu uzalishaji wa sukari nchini alisema serikali inaendelea na jitihada za kuwahamasisha wananchi kulima kilimo cha miwa ili kiwanda cha sukari kiweze kuzalisha sukari ya kutosha kwa lengo la kuhakikisha sukari ya kutosha inazalishwa nchini.

Alifafanua kuwa, kiwanda cha sukari kina uwezo mkubwa wa kuzalisha sukari ijapokuwa kutokana na uhaba wa zao la miwa unapelekea kiwanda hicho kuwa na uzalishaji mdogo.

Aidha alisema  ipo haja kwa wakulima kuitumia fursa hiyo ya ukulima wa miwa ili wanufaike na kilimo hicho na kukiwezesha kiwanda hicho kuzalisha sukari kwa wingi.

Akizungumzia kuhusu ongezeko la  bei za bidhaa mbalimbali hasa za vyakula, alisema serikali inaendelea kuchukuwa  jitihada  mbalimbali za kuhakikisha bei elekezi inaendelea kutumika ili kuwawezesha  wananchi  kumudu mahitaji ya kila siku.

“Nawataka wananchi waelewe kuwa, bidhaa zote ambazo tuliweka bei elekezi bado bei ile inaendelea kutumika, baadhi ya bidhaa zilizopanda bei zinaendelea kutafutiwa ufumbuzi kwa namna mbalimbali ili tupunguze ukali wa maisha kwa wanachi wetu” alisema Waziri.

Katika kurahisisha upatikanaji wa Leseni za Biashara Waziri Shaaban alisema hivi sasa Wizara imefanikisha kuweka mfumo wa kielekrotiniki wa utoaji leseni pamoja na kuziweka karibu taasisi zote zinazohusika na utoaji wa leseni hizo, ili kuwarahisishia wafanya biashara kupata leseni na kuondoa usumbufu.

Akizungumza kuhusu mafanikio ya Tamasha la Biashara la mwaka huu alisema mafanikio makubwa yameweza kupatikana mwaka huu kwani wafanya biashara wengi kutoka nchi mbalimbali afrika wamekuja Zanzibar.

Alisema hilo mwakani linatarajiwa kufanyika Nyamanzi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar, katika eneo la kudumu ili Serikali iweze kuingiza mapato na kukuza biashara, pamoja na kujenga kituo kikubwa cha mikutano cha kimataifa katika eneo hilo.

Mkutano baina ya Waziri wa Biashara na waandishi wahabari unatarajiwa kufanyika kila mwanzo wa mwezi kwa lengo la kuwapa taarifa wananchi  kuhusu maendeleo yanayofanywa na wizara hiyo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.