Habari za Punde

Wizara ya Elimu Yakabidhi Sare kwa Wanafunzi Waliorudi Skuli

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said akimkabidhi sare za Wanafunzi Mkurugenzi Idara ya Elimu Mbadala na Wazi Wazima Bi. Mashavu Ahmada Fakih, hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa Wizara ya Elimu mazizini Jijini Zanzibar. 

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amesema ni lengo la Serikali kuhakikisha  inawakumbuka watoto waliacha Skuli kwa kuwapatia mahitaji mbalimbali ili waweze kuendelea vizuri na masomo.

Amesema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi  sare za Skuli kwa watendaji wa Wizara ambao wanawasimamia Wanafunzi waliorudia Skuli kuanzia umri wa miaka 7  hadi 14 huko ofisini kwake Mazizini Mjini Unguja.

Amesema  kuna Wanafunzi zaidi ya elfu 11 wameweza kurejeshwa Skuli kupitia mradi maalumu,  hivyo ni vyema Wanafunzi hao kuwasadia kwa kuwapatia misaada mbalimbali ili nao wajisikie furaha kwa maamuzi yao ya kurudi Skuli .

Amesema ili watoto hao wapate haki yao ya elimu ni vyema Serikali kupitia Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na Shirika la kuhudumia watoto UNICEF  kuona wanapata mahitaji yao yote.

Aidha amewapongeza wasimamizi mbalimbali wanaohakikisha kuwa mradi wa kuwarejesha watoto skuli unafanikiwa kwa aslimia zote.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya Elimu mbadala na watu wazima bi Mashavu Ahmada Fakih amesema  upatikanaji wa vifaa hivyo huwapa faraja Wanafunzi hao kwani mara baada ya kumaliza vipimo hujiunga na madarasa ya kawaida na hivyo huondosha utofauti miongoni mwao.

Hivyo ameahidi kuhakikisha kuwa vifaa hivyo vitatumika kama vilivyokusudiwa  ili  walengwa nao  watimize ndoto zao za kupata elimu katika mazingira ya furaha na salama.

Vifaa vilivyokabidhiwa kwa ajili ya Wanafunzi hao ni pampja na sare za skuli, Kampasi, viatu na mikoba  kwa Unguja na Pemba.

Wakati huo huo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe Simai Mohammed Said amekagua vitengo mbalimbali vilivyomo ndani ya Wizara hiyo na kusema kuwa atafanya uwezekano wa  kubadilisha mifumo ya utoaji wa huduma ikiwemo ya masjala, na kalamazuu kwa kupitia mfumo wa digitali ili  kuondokana na mrundikano wa mafaili katika Ofisi zao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.