Habari za Punde

Dk Mabodi atoa onyo kali kwa wapinzani

NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.

CHAMA Cha Mapinduzi(CCM) Zanzibar, kimewaonya baadhi ya Wanasiasa kuacha tabia za kutafuta ‘Kiki’ za kisiasa kwa kuwachafua viongozi wa Serikali na Chama badala ya kusifia maendeleo yaliyofikiwa nchini.

Onyo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Mabodi, katika kongamano la kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza mwaka mmoja iliyoandaliwa na UWT iliyofanyika Amani Mkoa Zanzibar.

Dk.Mabodi ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, aliwashauri wanasiasa hao kama wameshindwa kazi za kisiasa bora watafute kazi zingine za kujiingizia kipato kwani wananchi hawahitaji siasa za kuuza maneno na porojo bali wanahitaji maendeleo endelevu.

Dk.Mabodi, alisema genge hilo la wanasiasa limekuwa likitangatanga kila kona wakibeza na kupotosha juhudi na hatua kubwa zinazofanywa na Serikali zote mbili.

Naibu Katibu Mkuu huyo Dk.Mabodi, aliweka wazi kwamba ni aibu na fedheha kubwa kwa kundi hilo kukosa uzalendo wa hata kuthamini maendeleo yanayofanywa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa ambayo wao ni Sehemu ya Serikali hiyo.

Alisema Chama Cha Mapinduzi kwa awamu mbali mbali kabla na baada ya mfumo wa vyama vingi nchini kimetatua kero na changamoto za wananchi bila kujali tofauti za kisiasa.

Katika maelezo yake Dk.Mabodi, alisema Dunia nzima inatambua kwamba CCM ni Chama Kiongozi na mwalimu wa siasa zilizokuwa hai na zinazojali utu na kutimiza mahitaji ya Wananchi.  

Kiongozi huyo aliwambia wanasiasa hao wanaotoka katika moja ya Chama cha Upinzania Zanzibar kuwa waache mtindo huo wa siasa chafu bali wajipange kushindana kwa Sera za maendeleo yaani waonyeshe mambo waliyoyatekeleza kwa wananchi kama inavyofanya CCM.

“ Tushindane kwa Sera na sio maneno na vituo, CCM ina mengi ya kujivunia kwani tumefanya na tunaendelea kutekeleza Ilani yetu ya Uchaguzi ya mwaka 2020/2025 katika sekta za Afya,Maji,Elimu na miundombinu ya barabara,anga,nchi kavu, baharini na kila sehemu tunahakikisha wananchi tunawafikia.

Tunayo mengi ya kujivunia na kutamba sasa na nyie wenzetu semeni yenu mliyowafanyia wananchi ?,,.sio mnasubiri sisi tufanye eti nyie muanze kupotosha na kukosoa twambieni Unguja na Pemba wapi mmejenga shule,hospitali,visima vya maji safi na salama hata msaada mdogo tu wa kijamii kwani ruzuku mnapata.”, alihoji Dk.Mabodi.

Dk.Mabodi aliweka wazi kwamba kwa mwenendo huo wanaokwenda nao wanasiasa hao ni kielelezo tosha cha kuonyesha Dunia kwamba Zanzibar kwa sasa hakuna Chama cha upinzania chenye maono,hoja na Sera imara za kushindana na CCM.

“ CCM tunaendelea kutamba na kusonga mbele kimaendeleo kwa kasi ya 4G huku wenzetu wakihaha na kurusha mawe kwenye kiza,  huku sisi tukitekeleza kwa wakati ahadi tulizotoa kwa wananchi kupitia uchaguzi mkuu uliopita.

Dk.Mabodi, aliwasihi wananchi wa makundi yote kuendelea kumtia moyo na kumuunga mkono Rais huyo mwenye dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo ya nchi.

Alisisitiza Wanaccm kuendelea kudumisha umoja na mshikamano,upendo na kulinda maslahi ya Chama kwa vitendo.

Alisema uongozi shirikishi ni moja kati ya sifa za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan kitaaluma.

 

Alieleza kuwa kutokana na uongozi wake huo ndio maana amekuwa akikumbukwa na jamii.

 

Hata hivyo alisema mageuzi ambayo anayafanya katika diplomasia ni kwa maslahi ya watanzania.

Aliwakumbusha Wanaccm hao kushiriki kikamilifu kwa kutoa taarifa sahihi katika zoezi la sensa ya Watu na Maakazi ili Serikali ifanikishe mipango ya maendeleo inayoendana na mahitaji ya wananchi.

Pamoja na hayo aliwataka Wana CCM kujipanga vizuri juu ya uchaguzi wa Chama unaofanyika mwaka huu kwa kuhakikisha wanapatikana viongozi imara,waadilifu na wachapakazi.

Wakati huo huo Naye Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Rais Samia amekuwa na ushirikiano mkubwa na Zanzibar katika shughuli mbali mbali za maendeleo.

Rais Mwinyi Aliyaeleza hayo alipotoa salamu zake za pongezi kwa kutimiza mwaka mmoja kwa njia ya simu katika mkutano huo.  

Alisema tangu kuwa rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania rais Samia amekuwa akiisaidia Sana serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kupeleka mbele Mipango ya kimaendeleo.

"Niseme tu kwamba nafarajika sana na uwepo wake na nitowe shukrani za dhati katika ushirikiano wake kwa SMZ", alisema.

Dkt. Mwinyi alisema misaada mengi ambayo yanaonekana kwa sasa yamepatikana kupitia kwake.

Hivyo aliwataka wanaccm pamoja na wananchi wote kwa ujumla kumuunga mkono rais Samia katika kutekeleza majukumu yake.

Nae Makamu Mwenyekiti wa UWT Thuwaiba Edington Kisasi amesema wana kila sababu ya kumpongeza kutokana na mambo mengi na makubwa aliyoyafanya kwa kipindi kifupi cha uongozi wake.

 

Aidha alisema kuendelea kudumisha Amani na utulivu no sifa kubwa ambayo rais Samia na wataendelea kuwa nae bega kwa bega katika kufanikisha Mipango ya maendeleo kwa nchi yao.


Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa mjini kichama Talib Ali Talib, alisema Safari ya mwanamke kuwa kiongozi ilianza mwaka 1964 na aliekuwa rais wa Kwanza Zanzibar marehemu Abeid Amani Karume.

 

Alisema Karume Mara tu baada ya nchi kupata uhuru kazi aliyoifanya ni kuwapa wanawake fursa za kuwa viongozi katika serikali yake.

 

Akitoa mada kuhusu mchango wa rais Samia katika kuimarisha maendeleo ya uchumi na jamii Tanzania Bara na Zanzibar  kada wa CCM dkt. Sada Mkuya amefanikiwa kurejesha mahusiano mazuri ya kimataifa ambayo yalikuwa yametetereka.

 

Mkuya ambae ni Waziri wa Nchi, Afisi ya Rais fedha na Mipango alisema kupitia hatua hiyo imepelekea kuvutia wawekezaji, kukuza biashara,kuimarisha muungano, usawa wa kijinsia, kuongezeka kwa fursa za uchumi wa Zanzibar  na kuwataka Wanaccm kutumia fursa kwa kuyafanyia kazi mazingira mazuri aliyoyaweka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.