Habari za Punde

Serikali Yaongeza Bajeti ya Utafiti Kukuza Sekta ya Kilimo-Bashe

Na. Mawazo Kibamba –MAELEZO Machi 7, 2022.

Waziri wa kilimo Mhe. Hussein Bashe amesema kuwa Serikali katika kipindi cha mwaka mmoja wa Rais Samia Suluhu Hassan madarakani imefanikiwa kuongeza  bajeti ya utafiti katika sekta ya kilimo ili kukuza sekta hiyo.

Ameyasema hayo Jijini Dar Es Salaam katika mkutano maalum na waandishi wa habari akielezea mafanikio ya Wizara ya Kilimo katika kipindi cha mwaka mmoja wa serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Bashe amebainisha  kuwa serikali imeongeza bajeti ya utafiti  kutoka Sh. Bilioni 7.35 hadi Sh. Bilioni 11.63 ambapo jumla ya shilingi Bilioni 3.63 zimetolewa kuwezesha taasisi zinazosimamia sekta ya kilimo zikiwepo za TARI, TORITA, TRIT, TPHPA, na TACRI kufanya   utafiti wa mazao ya kilimo ikiwemo mchikichi, zabibu, mkonge, ngano, alizeti, kahawa chai na tumbaku.

Ameongeza kuwa Wizara imefanikiwa kufungua masoko mapya ya mazao nje ya nchi ikiwemo soko la parachichi nchini India na Afrika Kusini na soko la Ndizi nchini Kenya, baada ya kukidhi viwango vya ubora ambapo Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko Tanzania (CPB) imefungua vituo vya mauzo katika miji ya Juba (Sudani Kusini) na Lubumbashi (DR Congo) na kukodi maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 5,000.

“Serikali katika kipindi hiki tuliangalia mazao gani ambayo yananunuliwa sana na masoko yanayotuzunguka  kwenye Jumuiya ya Afrika Mashariki ama SADC, serikali iliamua kwenda kujenga maghala katika nchi ambazo ndizo  tunazouza mazao yetu ambapo mpaka sasa tumefungua maghala katika nchi za Sudani Kusini, Congo (Lubumbashi), na haya maghala yote yanafunguliwa na serikali ya Tanzania ili  wafanya biashara wa Tanzania waweze kupeleka na kuuza mazao” Amesema Bashe

Aidha Mhe. Bashe Ameeleza kuwa Wizara imesaini hati ya makubaliano ya miaka mitano na Kampuni ya Smart Import and Export ya Misri, kwa ajili ya ununuzi wa mahindi ya njano, na rasimu ya makubaliano ya kuiuzia India mazao ya jamii ya mikunde hususan mbaazi, ambapo taratibu nyingine zinaendelea.

Akielezea malengo mahususi ya wizara ya kilimo amesema serikali imejipanga kuongeza ukuaji wa Sekta ya kilimo kutoka asilimia 5 za sasa na kufikia asilimia 10, kuongeza mchango wa Sekta ya kilimo kwenye GDP kutoka asilimia 25 hadi kufikia 35 ifikapo mwaka 2030 na kupunguza umasikini kwa zaidi ya asilimia 50 kutoka asilimia 26.4 za sasa na kufikia asilimia 13 ifikapo mwaka 2030, lakini pia kuongeza thamani ya mauzo ya mazao ya kilimo nje ya nchi, kutoka Dola za Marekani Bilioni 1.2 za sasa kufikia Dola za Marekani Bilioni 5 ifikapo mwaka 2025.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.