Habari za Punde

Amewataka Waislamu Kuendelea Kuhamasishana Kushiriki katika Mashindano mbali mbali ya Quraan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. -Alhaj Hussein Mwinyi.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk.Hussein Ali Mwinyi akimkabidhi zawadi mshindi wa kwanza wa Mashindano Makuu ya 7 ya kusoma Quran Tajweed Zanzibar  yalioandaliwa na Majlisul Quran Zanzibar, yaliofanyika katika Masjid Noor Muhammad Mombasa kwa Mchina na (kulia kwa Rais) Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh.Saleh Omar Kaab.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi amewataka waislamu kuendelea kuhamasishana kushiriki katika mashindano mbali mbali ya Quraan katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ili kuweza kupata fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dk. Mwinyi ametoa wito huo katika nasaha zake kwa washirki wa mashindano makuu ya saba ya Quraan Tajweed Zanzibar, yaliofanyika Masjid Nooor Muhammad Kwamchina, Jijini Zanzibar.

Alisema kuna umuhimu mkubwa kwa waislamu kuhamasishana  kushirki katika mashindano mbali mbali katika mwezi huu mtukufu wa Ramadhani ,ikiwemo ya tahfidh quraan na mashindano mengineyo, kwa kigezo kuwa kuna fadhila kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Aidha, aliipongeza Ofisi ya Mufti kwa kazi nzuri inayofanya ya kuratibu mashindano mbali mbali, hivyo akatoa  wito wa kuhakikisha inashirkiana na taasisi zote na kuziwezesha ili kufanikisha malengo hayo. 

Rais Alhaj Dk. Mwinyi aliishukuru taasisi ya Majlisul Quraan kwa kuandaa mashindano hayo na kutaka kuendelea na utatibu huo kila mwaka , ikiwa ni hatua ya kuwapa uzoefu vijana ili hatimae waweze kuiwakilisha Zanzibar kimataifa.

“Niwaombe muendelee kuandaa mashindano haya kila mwaka na pale mnapoanda msiache kuwaalika majaji hawa kutoka nje”, alisema.

Alisema mashindano hayo ambayo yamewahusisha majaji kutoka nchi mbali mbali za nje ikiwemo Bangladesh, Kenya na Misri yamefanikiwa sana, kwani majaji hao wameonyesha namna bora ya kuisoma Quraan, huku akisistiza umuhimu wa vijana kuendeleea kujifunza ili waweze kuliwakilisha vyema Taifa katika mashindano ya kimataifa.

Katika hatua nyengine, Alhaj Dk. Mwinyi aliwashukuru walimu  wa madrasa kwa kazi nzuri ya kufundisha kitabu cha Mwenyezi Mungu na  kasistiza umuhimu wa kuendelea kuwafunza vijana , sambamba na kuwataka waislamu kuwasaidia walimu hao ili waweze kufanyakazi katika mazingira mazuri

Aidha,  alitumia fursa hiyo kuwashukuru waandaaji wa mashindano, wadhamini  pamoja na waumini wote waliohudhuria hafla hiyo na kubainisha umuhimu  wa kuisoma na kuisikiliza Quraani, hususan katika mwezi mtukufu wa Ramadhani.

Nae, Mufti Mkuu wa Zanzibar Samahat Sheikh Saleh Omar Kaab aliwakumbusha waislamu wajibu walionao wa kuisoma , kuifahamu na kuizingatia Quraan ili iweze kuwapeleka mbele katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Aidha, Katibu wa Mufti wa Zanzibar Sheikh Khalid Mfaume, alisema hatua ya washiriki wa mashindano hayo pamoja na Majaji kutoka nje ya nchi kuisoma Quraan kwa ufasaha na sauti nzuri ni kitendo chayokufuata maelekezo ya Mtume Muhammad (SAW).

Mapema, akisoma Risala ya Taasisi ya Majlisul Quraan Sheikh Mohamed Kombo alisema taasisi hiyo ilioanzishwa mwaka 1994 imefanikiwa kupata mafanikio makubwa , lengo likiwa ni kuwawezesha waislamu kuisoma na kuifundisha Quraan kama ilivyopokelewa.

Alieleza kuwa katika kufikia lengo la kuanzishwa kwake, taasisi hiyo imefanikiwa kuendeleza mashindano hayo kila mwaka na kuiwezesha Zanzibar kutoa mshiriki katika mashindano makubwa yanayofanyika Tanzania, ambapo mwaka huu yatafanyika Jijini Dar es Salaam April 16.

“Kiu kubwa ya taasisi ni kuhakikisha Zanzibar inapata nafasi ya kushiriki katika mashindano yanayofanyika katika nchi mbali mnbali za nje, kikiwemo Iran”, alisema.

Katika mashindano hayo ambapo waislamu kutoka ndani na nje ya Zanzibar walishiriki, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Mwinyi alimkabidhi zawadi mshindi wa mashindano hayo Ust. Hamdani Juma Hamdani (kutoka Mkoa wa Mjini Magharibi) baada ya kuwashinda washiriki wengine watano kutoka mikoa mbali mbali ya Zanzibar na hivyo kupata fursa ya kuiwakilisha Zanzibar katika mashindnao mbali mbali yatakayofanyika nje ya nchi.    

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 

 E-mail: abdya062@gmail.com.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.