Habari za Punde

Ziara ya Makamu wa Pili wa Rais Mhe.Hemed Abdalla Suleiman Kisiwani Pemba.

Wizara ya Elimu na na Mafunzo ya Amali imetakiwa kusimamia majengo yanayojengwa yawe na vigezo sahihi vya kitaalama.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla ametoa agizo hilo wakati akiendelea na ziara ya kukagua Miradi inayojengwa kwa fedha za kupunguza athari za Uviko 19 katika Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amesema baadhi ya Miradi ya maendeleo inaanzwa ujenzi wake kwa nguvu za wananchi ambao wana lengo la kuisaidia Serikali kupunguza changamoto zinazozowakabili ambapo Serikali inaamua kuendeleza miradi hiyo iweze kukamilika na  ameelekeza uongozi wa Wizara ya Elimu Zanzibar kukagua majengo hayo ili yawe katika vigezo na viwango vinavyokubalika. 

Amesema hatua ya Serikali kuwakabidhi vikosi Miradi mbali mbali ni Operesheni Maalumu na kuutaka uongozi wa Kikosi Maalum cha kuzuwia Magendo (KMKM)  kuongeza kasi ya utendaji ili madarasa yakamilike kwa wakati na kwa ubora pamoja kuondoa changamoto ya uhaba wa madarasa hasa katika kipindi hichi cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Aidha Mhe. Hemed ameeleza kuwa Serikali imeshamaliza changamoto ya ukosefu wa mabati na kueleza kuwa mabati yatakayoezekwa yawe na viwango na kuwa Serikali haitoebeba dhamana kwa mabati yatakayochukua chini ya miaka kumi.

Akigusia Miradi ya ujenzi wa Hospitali za Wilaya Mhe. Hemed amefurahishwa namna Miradi hiyo inavyoendelea katika Mkoa huo na kueleza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Afya itahakikisha Hospital zote hizo zinakuwa na vifaa na wataalamu ili wananchi watakaofika Hospitali kupata huduma bora.

Katika Ziara hiyo Mhe. Hemed ametembelea ujenzi wa maeneo ya kufayiakazi wajasiriamali wadogo wadogo na kueleza kuwa kukamilika kwa maeneo hayo kutasaidia wananchi kuweza kujiajiri na kujikwamua kimaisha sambamba na Halmashauri na mabaraza ya miji kuweza kukuza mapato yao na kukuza uchumi wa Nchi.

Nae Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Mhe. Salama Mbaruk Khatib ameeleza kuwa ujenzi wa miradi ya maendeleo inayojengwa kwa fedha za Ahueni ya uviko 19 inaendelea vizuri ndani ya Mkoa huo na kuahidi kuendelea kuisimamia ili ikamilike kwa wakati na kwa kiwango kinachohitajika.

Aidha Mhe. Salama ameeleza kuwa Mkoa wa Kaskazini Pemba katika fedha za Uviko 19  umebahatika kupata madarasa Mia Mbili na Nane (208) ambayo yatapunguza kilio cha muda mrefu cha wananchi wa Mkoa huo.

Nae Mkuu wa Kikosi Maalum cha Kuzuwia Magendo Zanzibar (KMKM)  Komodoo Azan Msingiri amemueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kuwa hadi sasa jumla ya madarasa sitini na Moja yamekwisha ezekwa na kumuahidi ndani ya kipindi cha wiki moja kukamilisha kuezeka Madarasa Tisini na Tisa na kuendelea  kukamilisha kwa hatua zinazofuata.

.................................
ABDULRAHIM KHAMIS
OFISI YA MAKAMU WA PILI WA RAIS WA ZANZIBAR
16/04/2022

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.